1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Kasembeli ataka kuendeleza historia ya Muafrika

17 Agosti 2018

Waswahili huamba yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Lakini Dr. Serah Kasembeli anaamini yaliyopita humpa njia binadamu ya kusonga mbele, ndio maana akaamua kuanza uchunguzi juu ya asili ya utumwa na athari za ukoloni.

https://p.dw.com/p/33HUX
Kenia, Dr. Serah Kasembeli
Picha: DW/T.Mwadzaya

Jengo la hifadhi ya kitaifa la Joseph Murumbi liko katikati ya jiji la Nairobi, na huwezi kulipita. Wakaazi wanapigana vikumbo nje ya jengo hilo na kuendelea na hamsini zao pasina kujali yanayofanyika ndani ya jengo hilo. Pindi unapoingia ndani kelele zote hupotea na kimya kizito kinagubika kwani uko ndani ya jumba linalohifadhi mambo ya kale. Na hapo ndipo tunapokutana na Dr. Serah Namulisa Kasembeli aliyerejea nchini muda mfupi baada ya kukamilisha shahada yake ya uzamifu iliyojikita kwenye utafiti wa madhila ya biashara ya watumwa na ukoloni.

”Wanasema ukiwa mwalimu mzuri unakuwa mwanafunzi mzuri. Nilitaka kuandika historia kwa mtazamo wa Muafrika na wala sio Mzungu kama ilivyokuwa tangu awali. Nilitaka kuandika historia ambayo haijachanganyika na utawala wa ukoloni,” anasema Dr. Kasembeli.

Ijapokuwa ni muhimu kuganga yajayo, Waswahili huamba yaliyopita si ndwele. Yaliyopita yana uzito wake na uzito huo ndiyo uliomsukuma Dr. Serah Kasembeli kuchunguza hasa asili ya utumwa na athari za ukoloni.

Dr. Kasembeli ni binadamu shupavu aliyeanzia masomo yake eneo la Kilome katika Kaunti ya Makueni. Alilazimika kuwatazama wadogo zake kwa muda wa miaka miwili, baada ya kuhitimu kidato cha nne kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Nairobi alikosomea shahada ya kwanza ya elimu.

Shahada hiyo ndiyo iliyomuwezesha kuwa mwalimu wa fasihi jambo lililompa faraja kubwa kwani alipata nafasi ya kutangamana kwa karibu na vijana wa kike na kiume. Ukimtazama Dr. Kasembeli utadhani ni muoga au mwenye kuona haya ila uso wake umeficha siri nyingi. Tulipokutana kwenye jumba la hifadhi ya kitaifa la Joseph Murumbi, tulijionea mengi. Kuta zilosheheni picha, michoro na silaha za kiasili kama vile mishale na ngao.

Kwa upande mwengine sanamu na vinyago vimewekwa mezani au kusimama vyenyewe. Ukivitazama kwa karibu vinaonekana kuficha mengi mazito na kuwa na maelezo ya kina ya kilichotokea enzi zilizopita.

Dr. Kasembeli aliye na imani kubwa kuwa historia ina nafasi muhimu katika maisha ya leo anasisitiza kuwa asili yake ni utumwa.

”Asili yake ni utumwa na kama hatujayatafakari jinsi yanavyotuathiri katika maisha ya sasa hatuwezi kuendelea mbele,”

Uandishi wa tamthilia ya 'Water but Wine'

Historia ya Kenya inajikita katika ukoloni na utumwa ulioandamana na biashara wakati huo. Serah alipata kuwa mwalimu wa sekondari kwa miaka kadhaa kazi iliyompa faraja.Hata hivyo alikerwa na mpangilio wa taaluma ya elimu ulivyo ukizingatia mipango ya mwalimu na kufundisha darasani.

Kila mwalimu sharti awe na muongozo maalum wa somo la siku na kutimiza malengo maalum. Hilo lilimsukuma kutaka kujitosa kwenye ulimwengu wa utafiti ili aweze kujibu masuali aliyokuwa nayo.

Harakati zake hizo zilimuwia kuandika tamthilia ya ‘Water but Wine' yenye maana ya Maji bali Mvinyo iliyojikita katika dhulma za kijamii hasa kwa wanafunzi wa kike wanaoishi katika maeneo ya mitaa ya mabanda. Kwa wakati huo alibaini kuwa wasichana wanalazimika kupitia mengi yanayokiuka nidhamu na maadili ili waweze kupata elimu na mahitaji yao ya kila siku.Jambo hilo lilimsuta nafsi na kujiona kuwa sio mkweli kwani hakuweza kutafuta suluhu yoyote kwa hali hiyo ya kutamausha. Alijitahidi kuwaelekeza wanafunzi hao kutia bidii na kujiamini kama njia ya kufanikiwa maishani hata wanapokabiliana na changamoto za maisha. Hayo aliyafanya alipokuwa anasomea shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha Nairobi.

Die Universität in Nairobi
Chuo Kikuu cha Nairobi, KenyaPicha: CC BY-SA 3.0 Wing

Changamoto za ameneo ya pwani katika biashara ya utumwa

Unapozungumzia historia ya utumwa si rahisi kulitenga eneo la Kisauni lililoko pwani ya Kenya. Kijiji cha Frere Town kilikuwa na umuhimu mkubwa baada ya biashara ya watumwa kuangamizwa. Kanisa la St Emmanuel, Kengeleni lilikuwa sehemu muhimu ya kuwashtua watumwa kwenda amfichoni kila kengele ilipopigwa. Ingawa ilikuwa nadra kwa vijiji vya pwani ya Kenya kuvamiwa kwa ajili ya kusaka watumwa, eneo hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa katika kuwasafirisha watumwa kwani halikuwa mbali na soko kuu la kisiwa cha Unguja, huko Zanzibar.

Na kabla ya kusafirishwa kupelekwa Zanzibar, watumwa hao walihifadhiwa eneo la mapango makubwa ya Shimoni lililo kusini mwa jiji la Mombasa. Watumwa hao waliotumika kama vijakazi na wahudumu wa mashambani walihamishwa kutokea maeneo ya mataifa yanayopakana na bahari ya Hindi. Machungu hayo waliyopitia watumwa ndiyo aliyotaka kuyafanyia utafiti Dr.Kasembeli.

”Madhila yaliyotokea tupambane nayo, tuangalie historia imesema nini. Tuangalie na tuseme tumetoka hapa. Tusiyafunike na kusema tunasahau yaliyopita. Kuwe na uwiano katika historia ya jadi na ya sasa. Vyombo vya habari viweze kutangaza yaliyopo kwa hali halisi,” anafafanua Dr.Kasembeli.

Haikuwa kazi rahisi kwa Dr.Kasembeli

Dr. Kasembeli alipambana na changamoto kadha wa kadha wakati wa kufanya utafiti wake. Alibaini kuwa vizazi vya sasa havijiulizi masuali mengi kuhusu historia yao. Kwa sasa amehitimisha utafiti wake wa shahada yake hiyo ya uzamifu iliyojikita katika madhila ya biashara ya utumwa na ukoloni. Kadhalika anajiandaa kuchapisha tamthilia yake ya 'Wine But Water' ili iweze kuigizwa katika siku za usoni.

Mzaliwa wa kwanza wa watoto wanne katika familia yake, Dr. Kasembeli ana wadogo zake watatu; mmoja wa kike na wawili wa kiume. Anapendelea sana kusoma vitabu vya kila aina na mamake mzazi aliye mwalimu aliwasisitizia umuhimu wa kujifunza mengi yaliyoandikwa.

Mama yake pia aliwahi kuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi, jambo lililowafanya jamaa zake kutaka usaidizi kimasomo kwa watoto wao. Baadhi yao walipata nafasi ya kuishi kwa kina Serah ili wapate elimu ya nidhamu na uzoefu wa kupenda kusoma vitabu hata visivyokuwa vya shule. Kwa upande wa pili, baba yake ni afisa wa usalama jambo lililowawezesha kusafiri na kuishi katika maeneo kadhaa ya mikoa yote nchini Kenya. Hilo nalo lilimuwezesha Serah kuwa na hamu ya kusafiri na kujionea mataifa mengine na aliwahi kufika hadi Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini . Serah ni mmoja kati ya Wakenya wasiopungua sita kupata ufadhili wa Lisa Maskell wa taasisi ya Ujerumani ya Gerda Henkel ili kusomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha Stellen Bosch nchini Afrika Kusini.   

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Yusra Buwayhid