1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idriss Deby Itno ashinda uchaguzi Chad

10 Mei 2024

Kiongozi wa kijeshi nchini Chad Mahamat Idriss Deby Itno ndiye mshindi wa uchaguzi uliofanyika wiki hii, kulingana na matokeo ya awali yaliyotangazwa usiku wa kuamkia Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4fgaB
Mahamat Idriss Déby Itno - Rais wa Chad
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby ItnoPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Matokeo hayo yamepingwa na mpinzani wake mkuu Succes Masra. Matokeo hayo yaliyokuwa yanatarajiwa Mei 21, yametolewa wiki moja mapema, na yamemuonesha Deby Itno akiwa na asilimia 61 ya kura huku Masra akipata asilimia 18.5 ya kura hizo. Kumesikika milio ya risasi N'djamena baada ya matokeo hayo kutangazwa.

Chad ilifanya uchaguzi wake baada ya kucheleweshwa kwa muda mrefu, huku ikiwa chini ya utawala wa kijeshi kwa miaka mitatu. Wachambuzi wanasema walitarajia ushindi kwa Mahamat Deby Itno ambaye yuko madarakani.

Picha ya pamoja ya Succès Masra na Mahamat Idriss Deby Itno
Kiongozi wa upinzani Chad Succes Masra (kushoto) na Mahamat Idriss Deby Itno (kulia)Picha: ISSOUF SANOGO/DENIS SASSOU GUEIPEUR/AFP/Getty Images

Njama ya kuchakachua matokeo

Deby Itno alichukua madaraka baada ya babake aliyekuwa uongozini kwa kipindi cha miongo mitatu, kuuwawa katika mapambano na waasi mwaka 2021.

Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta na yenye idadi ya watu milioni 18, haijafanya uchaguzi huru na haki tangu ilipopata uhuru wake 1960 kutoka kwa Ufaransa.

Saa chache kabla kutolewa kwa tangazo hilo la tume inayosimamia uchaguzi wa Chad, Masra alichapisha hotuba katika mtandao wa kijamii wa Facebook, akizituhumu mamlaka nchini humo kwa njama ya kutaka kuchakachua matokeo.

Katika hotuba hiyo ya dakika 11, Masra alionekana amevalia koti la samawati akiwa amesimama kwenye jukwaa lililokuwa na bendera ya nchi hiyo nyuma yake, akidai kwamba yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi.

Ametoa wito kwa jeshi la Chad, polisi na vikosi vingine vya usalama kutofuata maagizo ya Deby Itno. Hakukuwa na jawabu kuhusiana na madai hayo ya Masra kutoka ofisi ya rais wa nchi hiyo.

Rafiki wa mwisho wa Marekani na Ufaransa eneo la Sahel

Masra ambaye ndiye kiongozi wa chama cha The Transformers Party, aliikimbia Chad mnamo Oktoba 2022.

Chad N'Djamena 2024 | Uchaguzi | Zoezi la kuhesabu kura
Maafisa wa uchaguzi wakihesabu kura ChadPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Wakati huo, serikali ya kijeshi ya Chad, ilikifungia chama chake na vyama vyengine 6 kutokana na maandamano ya kupinga uamuzi wa Deby wa kuongeza muda wake madarakani kwa miaka miwili zaidi. Zaidi ya watu 60 waliuwawa katika maandamano hayo.

Chad inaonekana na Marekani na Ufaransa kama rafiki wao wa mwisho mwenye uthabiti katika eneo zima la Sahel, kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Burkina Faso, Niger na Mali katika miaka ya hivi karibuni.

Tawala za kijeshi katika mataifa yote hayo zimewatimua wanajeshi wa Ufaransa na kuvigeukia vikosi vya mamluki wa Urusi kwa usaidizi wa kiusalama.

Vyanzo: DPA/AP