Idadi ya wakimbizi yafikia milioni 60 | Masuala ya Jamii | DW | 18.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Idadi ya wakimbizi yafikia milioni 60

Mizozo na matumizi ya nguvu inayopamba moto duniani imepelekea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaolazimika kukimbia makaazi yao na kufikia rekodi ya watu milioni sitini kufikia mwishoni mwa mwaka 2014.

Wakimbizi wa Syria wakikimbilia Uturuki,

Wakimbizi wa Syria wakikimbilia Uturuki,

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema katika repoti yake Alhamisi (18.06.2015) kwamba wakimbizi zaidi milioni 8.3 na watu waliopoteza makaazi ndani ya nchi imeongezeka katika kiwango kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa kuliko ilivyokuwa mwaka 2013 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kiongozi wa shirika hilo Antonio Guterres amewaambia waandíshi wa habari kabla ya kuzinduliwa kwa repoti hiyo ya kila mwaka kwamba wanashuhudia mabadiliko ya kielelezo,kutumbukia bila ya kudhibitiwa katika enzi ambapo kwayo kiwango cha watu wanaopoteza makaazi duniani na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo ni dhahir hivi sasa imepiku kila kitu kilowahi kushuhudiwa kabla.

Repoti hiyo imeonyesha watu milioni 59.5 wamepotezewa makaazi yao duniani kote kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 ikiwa ni matokeo ya ukandamizaji,mizozo,vitendo vya ukatili kwa jumla au ukiukaji wa haki za binaadamu.

Idadi hiyo imeongezeka kulinganisha na ile ya mwaka 2013 ya milioni 51.2 na milioni 35.5 ya muongo mmoja uliopita. Kwa mujibu wa repoti hiyo kwa jumla wakimbizi walikuwa milioni 19.5,watafuta hifadhi walikuwa milioni 1.8 na watu milioni 38.2 walikimbia makaazi yao lakini waliendelea kubakia katika nchi zao.

Zaidi ya nusu ya wakimbizi ni watoto

Wakimbizi waliopoteza makaazi kutokana na mashambulizi ya Boko Haram nchini Nigeria.

Wakimbizi waliopoteza makaazi kutokana na mashambulizi ya Boko Haram nchini Nigeria.

Zaidi ya nusu ya wakimbizi hao duniani ni watoto idadi yao ikiwa imeongezeka kutoka asilimia 41 hapo mwaka 2009 wakati jumla ya watu waliokimbia makaazi yao imeongezeka kwa asilimia 40 katika kipindi cha miaka mitatu tu.

Gutteres amesema "mambo yanashindwa kudhibitika kwa sababu tu dunia iko vitani" na kusisitiza kwamba mizozo nchini Syria na Iraq pekee imewalazimisha watu milioni 15 kukimbia makaazi yao.

Lakini hiyo sio mizozo pekee inayowalazimisha watu wayakimbie makaazi yao na kutafuta hifadhi.Katika kipindi cha miaka mitano iliopita kumezuka au kumeripuka upya mizozo 14 duniani kote na nusu ya mizozo imetokea Afrika.Kamishna huyo amesema hawana tena uwezo na rasilmali za kuwashughulikia wahanga wote.

Nchi zinazoendelea zahifadhi wakimbizi zaidi

Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Antonio Guterres.

Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Antonio Guterres.

Barani Ulaya zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 219,000 walivuka bahari ya Mediterenia hapo mwaka 2014 kiwango hicho ni mara tatu zaidi ya kiwango kilichoshuhudiwa mwaka 2011 cha 70,000.

Licha ya hofu ilioelezewa na mataifa ya Ulaya na mataifa mengine tajiri juu ya kuongezeka kwa mmiminiko wa wakimbizi na wahamiaji repoti hiyo imeonyesha nchi zinazoendelea zinawapa hifadhi asilimia 86 ya wale wote waliokimbia nchi zao kutokana na vita na ukandamizaji.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 nchi iliokuwa imepokea wakimbizi wengi ni Uturuki ambayo imewapa hifadhi watu milioni 1.59 ikifuatiwa na Pakistan iliowapa hifadhi watu milioni 1.51 na Lebanone iliowahifadhi watu milioni 1.15.

Kwa mujibu wa data za karibuni kabisa za Umoja wa Mataifa idadi ya wakimbizi wa Syria wanaomba hifadhi nchini Uturuki imezidi kuongezeka mwaka huu kufikia zaidi ya milioni 1.7. tokea vita viripuke nchini Syria hapo mwaka 2011.

Akizungumza mjini Istanbul kwa ajili ya kuizinduwa repoti hiyo Gutteres ameihimiza dunia yakiwemo mataifa ya magharibi kufunguwa mipaka yao kuiga mfano wa Uturuki katika kuwapatia hifadhi wakimbizi wa Syria.

Machafuko yachochea uhamiaji

Wakimbizi wa Syria mpakani mwa Uturuki.

Wakimbizi wa Syria mpakani mwa Uturuki.

Repoti hiyo pia imesema machafuko yanayoendelea kwa baadhi ya sehemu za Afrika Kaskazini kufuatia vuguvugu la majira ya machipuko la ulimwengu wa Kiarabu ambalo limewaangusha madikteta kadhaa yamesababisha idadi kubwa ya watu kuhatarisha maisha yao kuvuka bahari ya Mediterenia kukimbilia Ulaya.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema limepata taarifa kwamba zaidi ya wanawake, wanaume na watoto 3,500 imeripotiwa kuwa wamekufa au hawajulikani walipo katika Bahari ya Mediterenia wakati wa mwaka 2014.

Eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika idadi ya wakimbizi imeongezeka kwa mwaka wa tano mfululizo na kufikia milioni 3.7 hapo mwaka 2014 ikiwa ni ongezeko la wakimbizi 759,000 kuliko ilivyokuwa mwaka uliotangulia huo.

Ikikabiliwa na mmminiko wa wakimbizi na wahamiaji wanaohatarisha maisha yao baharini kuingia Ulaya, bara lenyewe la Ulaya hadi sasa limeshindwa kuafikiana juu ya namna ya kuwashughulikia maelfu ya wakimbizi wapya.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri :Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com