1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ibada ya Hijja yaanza chini ya kiwingu cha COVID-19

Admin.WagnerD29 Julai 2020

Waumini wa dini ya kiislamu wanaanza ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia ambayo itashuhudia idadi ndogo kabisa ya mahujaji katika historia kutokana na janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3g5ZW
Saudi-Arabien einsame Pilger in Mekka an der Kaaba
Picha: AFP

Ibada hiyo ya kila mwaka inaanza leo katika mji mtukufu wa Makka chini ya kiwingu cha janga la virusi vya corona ambalo limesababisha waislamu wasiopindukia 10,000 pekee kuwa ndiyo wataruhusiwa kushiriki tukio hilo la kidini la siku tano.

Idadi hiyo waumini ambao wamechaguliwa kwa mchujo maalum ni sehemu ndogo sana ikilinganishwa na mahujaji milioni 2.5 waliohudhuria ibada ya hijja mwaka uliopita.

Theluthi mbili ya mahujaji waliochaguliwa mwaka huu ni wageni wanaoishi nchini Saudi Arabia na serikali imesema kuna uwakilishi wa mataifa 160 ambayo kwa kawaida waumini wake wa kiislamu kila mwaka hushiriki ibada hiyo.

Corornavirus | Saudi-Arabien Mekka vor der Hadsch
Picha: AFP/Saudi Ministry of Hajj and Umra

Hijja, moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na ambayo muumuni mwenye uwezo anapaswa kuitimiza walau mara moja katika maisha yake kwa kawaida ni moja ya mikusanyiko mikubwa sana ya kidini ulimwenguni.

Hata hivyo mripuko wa janga la virusi vya corona umeilazimisha Saudi Arabia kuzuia safari za mamilioni ya waumini na mahujaji wachache waliochaguliwa wamepimwa virusi vya corona na kwa siku kadhaa waliwekwa karantini katika hoteli mjini Makka.

Teknolojia kuchukua nafasi katika Hijja ya mwaka 2020 

Mkuu wa mipango katika wizara ya Hijja na Umra ya Saudi Arabia Amr Al-Maddah amesema wamejipanga kutumia teknolojia kurahisusha ibada hiyo na kupunguza kitisho cha kusambaa kwa virusi.

``Hivi sasa teknolojia ndiyo farasi wetu wa safari nzima ya Hijja. Tunatizama kile teknolojia inaweza kufanya kwa kurahisisha Hijja na kuifanya iwe kwa njia rahisi. Na pia kusimamia mwenendo wa watu wote hawa ambao wako kwa idadi kubwa" amesema Al- Maddah 

Mjini Makka na maeneo mengine matukufu vifaa vya kupima joto la mwili vinatumika kwa mara ya kwanza kufutilia dalali zozote za tahadhari ya kiafya kwa mahujaji.

Corornavirus | Saudi-Arabien Mekka vor der Hadsch
Picha: picture-alliance/AP/Saudi Ministry of Media

Vyombo vya Habari vya Saudi Arabia vimeonesha wafanyakazi wa afya wakipuliza dawa ya kupambana na virusi kwenye masanduku ya mahujaji huku wengine wakipatiwa mikanda maalum ya kufuatilia mahali waliko.

Saudi Arabia yalipia gharama zote za Hijja

Kadhalika mahujaji wote watatakiwa kuvaa barakoa na kuzingtia kanuni za kujitenga katika mfululizo wa ibada zitakazofanyika katika mji mtukufu wa Makka na maeneo jirani ya magharibi ya Saudi Arabia.

Pia kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, mamlaka inayosimamia ibada ya Hijja imewapiga marufuku mahujaji kuligusa ´´Ka´bah´´ jengo dogo la mraba lililo katikati ya msikiti mkuu mjini Makka.

Wakati wa ibada ya mwaka huu Saudi Arabia imesema gharama zote za chakula, malazi, usafiri na huduma ya afya kwa mahujaji zitalipwa na serikali.