1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya kuenea kwa virusi vya Hanta yazidi kutanda

Michael Kwena
6 Mei 2026

Watu watatu, wamehamishwa kwa dharura kutoka kwenye meli ya kifahari ya kitalii baada ya kuambukizwa virusi vya Hanta. Watu hao wamepelekwa nchini uholanzi kwa ajili ya matibabu.

https://p.dw.com/p/5DNSh
Virusi vya Hanta
Damu iliyoandaliwa kwa ajili ya vipimo vya virusi vya HantaPicha: Membio/Depositphotos/IMAGO

Watu watatu, wamehamishwa kwa dharura kutoka kwenye meli ya kifahari ya kitalii baada ya kuambukizwa virusi vya Hanta. Watu hao wamepelekwa nchini uholanzi kwa ajili ya matibabu. Taarifa zinaeleza kuwa wawili kati yao wamo katika hali mbaya kiafya. Shirika la Afya Duniani, WHO limetanga mlipuko huo wa virusi vya Hanta.

Meli hiyo, kwa jina MV Hondius, ilikuwa imekwama kwa siku kadhaa katika pwani ya Cape Verde, baada ya mamlaka nchini humo kuzuia abiria kushuka kwenye nchi kavu kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi hivyo. Takribani watu 150 walikuwa kwenye meli hiyo na hadi sasa, watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na mlipuko huo.

Meli hiyo inatarajiwa kuelekezwa Uhispania wa mujibu wa Kampuni inayoiendesha, Oceanwide Expedition.

Uhamisho wa wagonjwa wapingwa

Hata hivyo, Mpango wa kuruhusu meli hiyo kusafiri hadi Visiwa vya Canary ambapo baadhi ya abiria wake wameathiriwa na virusi vya hanta umeibua upinzani wa kisiasa katika visiwa hivyo vya Uhispania.

Rais wa Visiwa vya Canary, Fernando Clavijo, amelalamikia pendekezo la serikali ya Uhispania kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuruhusu meli hiyo kutia nanga katika visiwa hivyo.

Clavijo amesema hakuna uwazi kuhusu uamuzi huo na akataka kufanyike mkutano wa dharura na Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez.

Wizara ya Afya imesema uamuzi wa kuiruhusu meli hiyo kufika kwenye Visiwa vya Canary ulifikiwa kwa uratibu na WHO pamoja na Umoja wa Ulaya, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus,imesema walioathirika kwenye meli hiyo walikuwa njiani kuelekea Uholanzi kupata matibabu.

Meli ya Hondius ilianza safari yake kutoka kusini mwa Argentina na kwa sasa imetia nanga katika Bahari ya Atlantiki karibu na Cape Verde, katika pwani ya magharibi ya Afrika, kufuatia mlipuko wa virusi vya hanta.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Hispania, meli hiyo inapangwa kutia nanga katika kisiwa cha Tenerife, ambacho ni kivutio kikubwa cha watalii na pia kinahifadhi Hospitali ya La Candelaria, taasisi ya afya inayobobea katika kushughulikia magonjwa ya milipuko.

Matibabu yashika kasi

Serikali ya Uswisi kwa upande wake,imesema mwanaume aliyerejea nchini humo baada ya kuwa abiria wa Hondius alibainika kuambukizwa virusi vya hanta na kwa sasa,anapokea matibabu mjini Zurich.

Virusi vya Hanta
Mwonekano wa virusi vya hanta katika darubini ya maabaraPicha: Imagepointfr/Depositphotos/IMAGO

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi imesema kuwa miongoni mwa waliohamishwa kutoka katika meli hiyo ni raia mmoja wa Uholanzi, Mjerumani mmoja na raia mmoja wa Uingereza. Ujerumani imesema kuwa,raia wake huyo atalazwa katika hospitali mjini Düsseldorf kwa ajili ya vipimo maalum.

WHO imesema kuwa,idadi ya jumla ya waliothibitishwa kuwa na virusi vya hanta imefikia watu wanane, watatu kati yao wakithibitishwa kwa vipimo vya maabara. Shirika hilo liliongeza kuwa linazisaidia nchi husika katika shughuli za kuwafuatilia waliokuwa kwenye mawasiliano na wagonjwa hao, ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine,Wizara ya Afya ya Afrika Kusini imesema imebaini jumla ya watu 62 waliotangamana na waathiriwa wa mlipuko huo japo hadi sasa,hakuna aliyegundulika kuambukizwa virusi vya hanta.

Shirika la Afya Duniani, WHO, tayari limeeleza kwamba,linachunguza uwezekano wa mlipuko wa virusi vya Hanta kusambaa kutoka mtu hadi mtu

Kwa kawaida, virusi vya hanta huenea kwa njia ya kuvuta pumzi chafu kutokana na kinyesi cha panya walioambukizwa.