Hoffenheim yaizidishia matatizo Cologne | Michezo | DW | 06.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Hoffenheim yaizidishia matatizo Cologne

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Sandro Wagner aliifungia Hoffenheim mabao mawili wakati iliizaba Cologne 3-0 ikiwa ni ushindi wao wa kwanza katika mechi tano za Bundesliga

Cologne ilishindwa kuonyesha mchezo wao bora uliowasaidia kuwafunga BATE Borisov mabao matano kwa mawili kwenye Europa League katikati mwa wiki. Wanabakia katika nafasi ya mkia wakiwa na pointi mbili bila ushindi wowote katika mechi 11. Peter Stöger ni kocha wa Cologne "Tulizidiwa kabisa leo na Hoffenheim ilistahili kushinda mechi hii. Labda tulikuwa na nafasi mbili au tatu ambazo tungezitumia vyema ili kurudi mchezoni - kombora lililopioga mlingoti, lakini nnahisi kuwa Hoffenheim walikuwa wazuri zaidi kutuliko na hakika hatukuwa na mbinu leo za kuwazuia kucheza vyema kabisa na kutuangamiza"

Fußball Bundesliga VfL Wolfsburg - Hertha BSC (picture-alliance/Citypress 24/H. Hay)

Wolfsburg wametoka sare kwa mechi saba mfululizo

Katika matokeo mengine Hertha Berlin ilisawazisha katika dakika za mwisho na kuinyima Wolfsburg ushindi wa kwanza chini ya kocha Martin Schmidt, ambaye sasa na rekodi ya kutoka sare mechi saba mfululizo tangu alipochukua usukani. Wolfsburg wako katika nafasi ya 14 na pointi 11. Hertha wako mbele nafasi ya 11, na pengo la pointi tatu dhidi yao. Mario Gomez ni mshambuliaki wa Wolfsburg "Leo ulikua tu mchezo ambao hauwezi kuucheza na kutoka sare. Kipindi cha kwanza nadhani kilikuwa kizuri kwetu, kuanzia tu dakika ya kwanza. Tulikuwa na kasi na nguvu nyingi uwanjani. Tukawa kifua mbele 2-1 kufikia nusu ya mchezo kisha unadhani unapaswa kuwa na furaha au la, kwa sababu unahitaji kuongoza kwa mabao zaidi. Kipindi cha pili unaanza kwa kusinzia kiasi katika dakika chache za mwanzo. Tukapata bao na kuchukua uongozi lakini tena likasawazishwa na timu inayocheza kila baada ya siku tatu na hicho ni kitu ambacho hakifai kutokea kwetu bila shaka".

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - FC Bayern (Getty Images/AFP/P. Stollarz)

Bayern wamefufuka tena baada ya Ancelotti kufurushwa

Siku ya Jumamosi, mabingwa Bayern Munich walifungua pengo la pointi nne kileleni mwa Bundesliga baada ya kuwabwaga watani wao Borussia Dortmund kwa mabao matatu kwa moja. Bayern wameuimarisha mchezo wao tangu Jupp Heynckes alipochukua usukani baada Carlo Ancelotti kutimuliwa. Nahodha Arjen Robben alielezea kuridhika kwao na kocha Heynckes "Kama nahodha sasa, nnweza kusema nnajivunia timu yangu kwa sababu kile tulichokifanya katika wiki chache zilizopita ni kizuri sana. Bila shaka hatuko katika hali bora, kwa sababu tuna matatizo ya majeruhi, na tulivyokuwa katika wiki tatu au nne zilizopita, na ukiangalia tulipo sasa, inashangaza sana.

Bayern wana pointi 26, huku RB Leipzig wakiwa na pointi 22 katika nafasi ya pili baada ya ushindi wao wa mbili moja dhidi ya Hanover 96. Nambari tatu Borussia Dortmund wana pointi 20 sawa na Schalke 04, na Hoffenheim ni wa tano na pointi 19. Schalke ambao saa hawajashindwa mechi hata moja kati ya sita za mwisho katika mashindano yote, ilipata ushindi wa moja bila dhidi ya Freiburg. Hamburg iliondoka katika kundi la timu tatu za mkia baada ya kusajili ushindi wa tatu kwa moja dhidi ya Stuttgart. Borussia Moenchengladbach ilianguka katika nafasi ya saba baada ya kutoka sare ya moja moja na Mainz. Nazo Augsburg na Bayer Leverkusen ziligawana pointi baada ya sare ya moja moja.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman