1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya kuwafuta kazi wataalamu wa afya yakosolewa vikali

Amina Mjahid
7 Januari 2021

Chama cha madaktari na matabibu nchini Kenya kimekosoa kitendo cha kuwafuta kazi wataalam wa afya katika kaunti ya Mombasa na kutaka warejeshwe kazini mara moja

https://p.dw.com/p/3nd2P
Kenia Narobi Ärztestreik
Picha: Reuters/T. Mukoya

Chama cha matabibu na madaktari nchini Kenya, KMPDU, kimelaani hatua ya kuwafuta kazi madaktari 86 na wataalam wengine wa afya katika kaunti ya Mombasa.

Kwenye taarifa yake, chama cha KMPDU kinashikilia kuwa madaktari wamekuwa wakigoma tangu mwanzoni mwa Disemba mwaka uliopita baada ya serikali ya kaunti ya Mombasa kushindwa kutimiza makubaliano ya kurejea kazini yaliyofikiwa mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Baadhi ya waliyoafikiana kutimizwa ni kupandishwa vyeo kazini,kuimarisha mazingira ya kazi na malipo.Kwa sasa madaktari kupitia chama chao cha KMPDU wanataka wanachama wao kurejeshwa kazini na tume ya afya kuundwa kikatiba ili kudhibiti hali kwenye sekta ya afya. Baadhi ya waliofutwa kazi ni katibu Mkuu wa chama cha madaktari nchini Kenya KMPDU, Dr Chibanzi Mwachonda.

"Tatizo kubwa la ugatuzi ni kwamba, vile wafanyakazi wa afya madaktari, wahudumu wanavyoangaliwa masilahi yao ni kwamba inategemea sana sana na gavana anavyotaka tumesema suluhisho nikutengeneza hii tume iweze kushughulikia masilahi ya kazi ya wafanyakazi wote wa afya sio madaktari peke yake." alisema Dr Chibanzi Mwachonda

Kwenye waraka maalum uliotiwa saini na waziri wa afya wa kaunti ya Mombasa, madaktari hao wanalazimika kurejesha mali yote ya serikali kwa wasimamizi wao.

Baadhi ya wahudumu waliokuwa likizo waomba kurejea kazini

Kenia | Krankenschwester in Nairobi
Mhudumu wa afya katika moja ya hospitali nchini Kenya Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Wakati huohuo, kaunti ya Kisumu imewachukulia hatua wahudumu zaidi ya 400 wanaogoma na kuwazuia kuingia kwenye vituo vya kufanyia kazi kadhalika majina yao kufutwa kwenye daftari la malipo.

Kwenye taarifa yake, kaimu afisa mkuu wa afya na usafi katika kaunti ya Kisumu, Dr Gregory Ganda, alisema wahudumu hao walioadhibiwa wanalazimika kuomba kazi upya.Wahudumu wa afya walianza mgomo wao tarehe 7 Disemba iliyopita.

Kwa sasa wahudumu wote wa kaunti ya Kisumu waliokuwa likizo wameagizwa kurejea kazini katika muda wa saa 48 zijazo na watakaokiuka wataadhibiwa.

Yote hayo yakiendelea,maafisa wa afya wameingia kipindi cha lala salama cha muda wa mwisho wa kuanza kulipwa mafao yao kama walivyoafikiana na magavana. Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa hao kurejea kazini.

Hata hivyo baraza la magavana linashikilia kuwa hawajaridhia makubaliano hayo kwani serikali za kaunti hazijapokea fedha kutoka serikali kuu na wala kulijadili kwa kina tatizo lenyewe. Wycliff Oparanya ni mweyekiti wa baraza la magavana na anashikilia kuwa makubaliano hayo yalikuwa kati ya serikali kuu na vyama vya wahudumu wa afya.

Kulingana na baraza la magavana, kila kaunti imechukua hatua mwafaka kwa kuzingatia hali halisi. Wahudumu wa afya wanadai nyongeza ya mshahara kwasababu ya mazingira hatari ya kazi,bima kamilifu ya afya na mikataba ya kudumu kwa walioandikwa kazi kwa muda.

Mwnadishi: Thelma Mwadzaya DW Nairobi.