Hariri awasili Paris, njiani kurudi Lebanon | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

LEBANON

Hariri awasili Paris, njiani kurudi Lebanon

Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu, Saad Hariri, amewasili Paris kwa mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, huku ikifahamika kuwa yuko njiani kurejea nchini kwake kwa ajili ya Sherehe za Uhuru.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoituma kwenye mtandao wake wa Twitter, Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema alizungumza kwa simu na Hariri mara tu baada ya kuwasili Paris, aliyemuhakikishia kuwa atarejea nyumbani siku ya Jumatano, ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu waziri mkuu huyo kujiuzulu akiwa Riyadh nchini Saudi Arabia. 

Lebanon, ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa, inachukuliwa kama uwanja wa mapambano wa mataifa mengine yanayosaka ushawishi kwenye eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba ya Arabuni, zikiwemo Saudi Arabia na Iran.

Hariri aliwasili Paris na mkewe leo (Novemba 18) akitokea Saudi Arabia, na alitazamiwa kukutana na Rais Macron kwa mazungumzo yanayotarajiwa kutoa muelekeo wa hatima yake kisiasa. 

Picha za televisheni zilimuonesha Hariri na mkewe wakiwasili bila watoto wao wawili, ambao inafahamika walikuwa nao pamoja nchini Saudi Arabia.

Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuwa watoto hao wamebakia kwa ajili ya mitihani ya skuli, ingawa wengine wanachukulia kubakia kwao kunazidisha mashaka juu ya endapo Saudi Arabia inahusika na njama za kumuondoa Hariri, mwenye pia uraia wa ufalme huo wa Ghuba.

Mzozo mpya Mashariki ya Kati?

Kujiuzulu kwa Hariri kulichukuliwa kama muakisiko wa shinikizo la Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia dhidi ya Iran na kundi la Hizbullah linaloungwa mkono na Iran ndani ya Lebanon. 

Katika tamko lake la kujiuzulu, Hariri alisema alikuwa akihofia maisha yake, akizituhumu Iran na Hizbullah kwa kuifanya Lebanon na mataifa mengine ya Kiarabu yasiwe na amani.

Hata hivyo, Aoun na Hizbullah wamekuwa wakosoaji wakubwa wa Saudi Arabia kuhusiana na hatua hiyo ya Hariri kujiuzulu uwaziri mkuu akiwa huko, wakisema kuwa ufalme wa Saudia unahusika, huku Aoun akifika umbali wa kuituhumu serikali ya Mfalme Salman kwa "kumchukuwa mateka" Hariri.

Utawala wa Saudi Arabia unakanusha kuhusika na tangazo hilo la kujiuzulu, ukidai kuwa lilikuwa la Hariri mwenyewe na kwamba mwanasiasa huyo yuko huru.  

Waziri mkuu huyo kutokea madhehebu ya Sunni amekuwa kiini cha uvumi tangu alipotangaza kujiuzulu tarehe 4 Novemba. Hatua hiyo ya ghafla imezusha mtikisiko na wasiwasi mkubwa wa kisiasa sio tu kwa Lebanon, bali pia eneo zima la Mashariki ya Kati. 

Ufaransa ilikuwa ikishinikiza Hariri aweze kurudi Lebanon na kuweka wazi endapo anataka kweli kujiuzulu au kuendelea na wadhifa wake wa uwaziri mkuu, huku kwenyewe Lebanon wenzake serikalini wakisema kwamba hawakutambui kujiuzulu kwake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa
Mhariri: John Juma

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com