1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Haniyeh: Tuko tayari kwa mazungumzo

Grace Kabogo
28 Februari 2024

Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh amesema kundi hilo liko tayari kwa mazungumzo na Israel kuhusu vita vya Gaza, lakini wakati huo huo liko tayari kuendelea na mapigano.

https://p.dw.com/p/4czTo
Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh
Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail HaniyehPicha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Wire/IMAGO

Akizungumza Jumatano kwa njia ya televisheni, Haniyeh amesema ni wajibu wa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na jukumu la ndugu zao wa nchi jirani na Palestina inayokaliwa kimabavu kuchukua hatua ya kukomesha njama na mauwaji katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

''Tunaonesha utayari wetu wa kushiriki mazungumzo ili kuilinda damu ya watu wetu na kukomesha machungu makubwa wanayopitia katika vita hivi vya kikatili. Sambamba na hilo tuko tayari kuwatetea watu wetu,'' alifafanua Haniyeh.

Haniyeh pia amewatolea wito Wapalestina wa Jerusalem na Ukingo wa Magharibi kuandamana hadi kwenye Msikiti wa Al-Aqsa kuswali, siku ya kwanza ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Machi 10.

Wanajeshi wa Israel wakiulinda Msikiti wa Al-Aqsa
Wanajeshi wa Israel wakiulinda Msikiti wa Al-AqsaPicha: AHMAD GHARABLI/AFP/Getty Images

Siku ya Jumatatu Israel ilisema itaruhusu swala wakati wa Ramadhan katika Msikiti wa Al-Aqsa. Rais wa Marekani Joe Biden, alisema ana matumaini kwamba makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza yanaweza kuanza kufikiwa Jumatatu ijayo ya Machi 4, kufuatia mazungumzo nchini Qatar pia yenye lengo la kuwaachilia huru mateka.

Ezzedine Al-Qassam yashambulia kaskazini mwa Israel

Huku hayo yakijiri, tawi la kijeshi la Hamas, Ezzedine Al-Qassam limesema limerusha makombora kadhaa kuelekea kaskazini mwa Israel kutokea kusini mwa Lebanon. Katika taarifa yake Al-Qassam imesema ilikuwa ikiyalenga maeneo mawili ya Israel, ikiwa ni katika kulipiza kisasi mashambulizi ya Israel dhidi ya raia kwenye Ukanda wa Gaza.

Ama kwa upande mwingine familia wa watu wanaoshikiliwa mateka na wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, wanaanza maandamano ya siku nne kutoka kusini mwa Israel kuelekea Jerusalem, kushinikiza kuachiliwa huru kwa wapendwa wao.

Wapiganaji wa Ezzedine Al-Qassam katika eneo la Maghazi, Ukanda wa Gaza
Wapiganaji wa Ezzedine Al-Qassam katika eneo la Maghazi, Ukanda wa Gaza Picha: Majdi Fathi/Zuma/picture alliance

Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo mazungumzo ya kufikia makubalino kati ya Hamas na Israel, kufungua njia ya kushitishwa vita na kubadilishana wafungwa na mateka yakiendelea Qatar.

Aidha, wizara ya afya kwenye Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas imesema takribani watu 30,000 wameuwa katika vita vya Gaza. Watu wengine 91 wameuawa katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo.

Al-Sissi: Mpaka wa Rafah uko wazi

Wakati huo huo, Rais Abdel-Fattah al-Sissi wa Misri amesema Jumatano kuwa nchi yake imekuwa ikikiwacha wazi kivuko cha mpaka wa Rafah, njia pekee kuingia katika Ukanda wa Gaza ambayo haidhibitiwi na Israel.

Hata hivyo, Al-Sissi amesema Misri haijawahi kukifunga kivuko hicho, lakini ili kuweza kuchukua hatua katika hali ya mapigano, wanapaswa kuwa waangalifu ili wasisababishe shida, ndani ya mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas, kundi ambalo nchi za Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zimeliorodhesha kama kundi la kigaidi.

(AFP, AP, DPA, Reuters)