1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia Afghanistan.

Halima Nyanza6 Agosti 2009

Ghasia na mauaji yanaendelea nchini Afghanistan, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Rais nchini humo. Watu 21 wameuawa leo baada ya bomu lililotegwa ardhini kuliripua trekta walilopanda.

https://p.dw.com/p/J55A
Katibu Mkuu mpya wa NATO Anders Fogh Rasmussen atoa ahadi ya vikosi vyake kusaidia ulinzi wakati wa uchaguzi nchini Afghanistan.Picha: AP

Shambulio hilo ambalo lilitokea jana, lakini halikuwa limeripotiwa hadi leo, ni sehemu ya ghasia zinazoongezeka katika hatua za mwisho za kampeni za uchaguzi huo wa Agosti 20, uchaguzi ambao Rais anayetetea nafasi yake Hamid Karzai ambaye anapewa nafasi kushinda katika uchaguzi huo.

Kamanda wa Jeshi la Afghanistan Sher Mohammad Zazai, katika jimbo la Helmand amesema mlipuko huo umetokea katika eneo la Garmsir, sehemu ya jimbo ambalo Jeshi la Marekani mwezi uliopita ilizindua operesheni kubwa dhidi ya wapiganaji wa Taliban.

Amelielezea shambulio hilo kufanywa na wapiganaji hao wa Taliban ambao amewaita kuwa ni adui wa taifa na maadui wa amani.

Miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo ni pamoja na wanawake na watoto waliokuwa wakielekea harusini.

Wizara ya Ulinzi na ya Mambo ya ndani ya Afghanistan imethibitisha idadi hiyo ya watu waliouawa.

Ghasia zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini Afghanistan kwa sasa zimefanya kuwepo kwa wanajeshi wengi wa Marekani waliouawa, tangu Majeshi yanayoongozwa na nchi hiyo kuingia Afghanistan mwaka 2001.

Mwezi uliopita majeshi ya Marekani na Uingereza walianzisha operesheni kubwa katika jimbo la Helmand ambapo mapigano bado yanaendelea, kusalimisha eneo hilo ambalo lilikuwa likishikiliwa na wapiganaji wa Afghanistan.

Operesheni hiyo inalenga kuongeza udhibiti wa serikali katika eneo hatari la kusini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi na kama sehemu ya Marekani kuwadhibiti wapiganaji katika nchi za Afghanistan na Pakistan.

Wakati uchaguzi wa Rais ukifanyika mwezi huu nchini humo Kundi la Taliban limedhamiria kuvuruga uchaguzi huo na kutoa wito kwa Wa Afghanistan kuugomea.

Tayari kumeripotiwa matukio ya kushambuliwa kwa wagombea wenza wa Urais na misafara ya wagombea.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 1000 wameuawa kati ya mwezi Januari hadi June mwaka huu, huku katika kipindi kama hicho mwaka uliopita waliuawa raia 818.

Katika kipindi tu, cha mwezi uliopita jumla ya wanajeshi 71 wa kimataifa waliuawa ikiwa ni idadi kubwa kabisa kwa majeshi ya kigeni tangu vita hivyo kuanza.

Mwandishi: Halima Nyanza(AFPA)

Mhariri: M.Abdul-Rahman