1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gesi ya Sarin ilitumika kama silaha ya kemikali Syria

Sylvia Mwehozi
30 Juni 2017

Ujumbe wa kutafuta ukweli wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuzuia matumizi ya silaha za kemikali OPCW, umehitimisha kuwa gesi ya Sarin ilitumika kama silaha ya kemikali katika shambulio la mjini Khan Sheikhun, Syria.

https://p.dw.com/p/2fgIR
UNO verlängert Untersuchung zu Chemiewaffeneinsatz in Syrien
Picha: Getty Images/AFP/F. Dirani

Matokeo ya utafiti wa shirika la kuzuia kuenea kwa silaha za kemikali OPCW sasa yatajadiliwa kwa pamoja na jopo la Umoja wa Mataifa na shirika hilo ili kubaini iwapo vikosi vya serikali ya Syria vilihusika na shambulio hilo.

"Kufuatia kazi waliyoifanya, timu ya kutafuta ukweli imehitimisha kuwa idadi kubwa ya watu ambao baadhi yao walifariki, kutokana na gesi ya sarin au kitu kinachofanana na sarin", imesema sehemu ya ripoti hiyo ambayo shirika la habari la AFP ilifanikiwa kuipata.

Watu karibu 87 wakiwemo watoto wengi waliuawa katika shambulio hilo ambalo Marekani, Ufaransa na Uingereza zinasema lilitekelezwa na vikosi vya Rais Bashar Al Assad.

Marekani ilifanya shambulio la kombora siku chache baadae dhidi ya ngome ya anga kutoka eneo ambalo linatajwa kuwa ndiko shambulio la silaha za kemikali lilitekelezwa .

Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema katika taarifa kwamba amekuwa na imani kubwa katika ripoti ya OPCW, ambayo imewasilisha hitimisho kuhusu shambulio la sarin.

"Sasa kwa kuwa tunafahamu ukweli usiopingika, tunatazamia uchunguzi huru ili kuthibitisha kabisa nani alihusika na mashambulizi haya ya kikatili ili kutafuta haki kwa ajili ya wahanga," alisema Halley.

Ahmet Uzumcu Porträt
Mkuu wa shirika la OPCW Ahmet UzumcuPicha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP/Getty Images

Mfumo wa uchunguzi wa pamoja baina ya OPCW na Umoja wa Mataifa tayari imebaini kwamba vikosi vya serikali ya Syria vinahusika na mashambulizi ya gesi ya Klorine katika vijiji vitatu mwaka 2014 na 2015 na kwamba kundi la Dola la Kiislamu pia lilitumia gesi aina ya haradali mwaka 2015.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema hii leo kuwa "hakuna shaka yoyote" kuwa serikali ya Assad ilitumia silaha za kemikali katika shambulio la mwezi wa nne."Tutaendelea na kampeni ya Uingereza ya kuweka vikwazo kwa wahusika. Marekani tayari imeweka vikwazo kwa watu 300 kutokana na hili. Watu wanaotumia silaha za kemikali dhidi ya watu wasio na hatia ni lazima wachukuliwe hatua, "alisema Johnson.

Urusi, ambayo ni mshirika wa Syria imeyapuuza matokeo hayo ikisema si ya kuaminika. Mwezi Februari, Moscow ilipiga kura ya turufu dhidi ya azimio la Umoja wa Mataifa ambalo lingeiwekea vikwazo Syria juu a matumizi ya silaha za kemikali katika vita iliyodumu kwa miaka sita.

Hayo yakijiri, nchini Syria kwenyewe vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani vimeuzingira kikamilifu mji unaoshikiriwa na kundi la wanamgambo wa IS kaskazini mwa Syria baada ya kukata mawasiliano ya barabara ya mwisho ya kutokea.

Jeshi la Syria la Democratic forces SDF limeuzingira kikamilifu mji wa Raqqa na wapiganaji walioko ndani kutoka pande zote, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kundi moja linalofuatilia hali ya mambo na chanzo kutoka ndani ya jeshi la Wakurdi. Inasadikiwa wapiganaji karibu 4000 wa IS wamesalia ndani ya mji huo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/AFP/Dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Stoltenberg in Kiew
Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW
Nenda ukurasa wa mwanzo