1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gavana Joho ahukumiwa kifungo cha miezi 2 jela

Grace Kabogo
21 Mei 2021

Gavana wa Mombasa nchini Kenya, Hassan Ali Joho, amehukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani au kulipa faini ya shilingi laki mbili na nusu za Kenya kwa kukosa la kukiuka amri ya mahakama. 

https://p.dw.com/p/3tn2N
Wahlen in Kenia 2017 - Governor von Mombasa Joho
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kulingana na hakimu katika mahakama ya ardhi na mazingira Sila Munyao, Gavana Joho amepatikana na hatia ya kuubomoa ukuta wa mfanyabiashara Ashok Doshi katika eneo la Changamwe, licha ya mahakama kutoa agizo la kutovunjwa kwa ukuta huo.

Aidha, gavana huyo amekuwa hahudhuriii vikao vya mahakama licha ya kuagizwa na mahakama kufanya hivyo. 

Hakimu Munyao amesema Joho kwa hadhi aliyonayo kama gavana, ni muhimu kwake kuongoza katika kuheshhimu sheria, mengi yanahitajika kutoka kwake hasa katika kuheshimu mahakama.

''Kwa kuzingatia haya yote ninamtoza faini ya shilingi laki mbili na nusu au kifungo cha siku sitini, na pia Joho atamlipa mlalamikaji gharama zote alizopata kutokana na ubomoaji uliofanywa katika ardhi yake,'' alifafanua hakimu huyo.

Gavana Joho ni mmoja wa viongozi nchini Kenya walio na nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa hivyo basi kupatikana na hatia katika mahakama ni jambo ambalo limepokewa kwa hisia mbalimbali.

Kulingana na wakili Hamisi Mwadzogo, kiongozi katika ofisi ya umma anapaswa kutii sheria na iwapo mienendo yake itakuwa kinyume anaweza kuondolewa madarakani.