1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi bado yupo Libya

22 Februari 2011

Kiongozi wa Libya Moammar Gaddafi amekanusha tuhuma kuwa ameikimbia nchi hiyo, huku maandamano yanaenea, na maafisa wa utawala wake wamejiuzulu.

https://p.dw.com/p/10Lfh
Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.Picha: AP

Vyombo vya habari nchini Libya vilikanusha tuhuma kuwa maafisa wa usalama wanawauwa waandamanaji. Hii ni baada ya kiongozi anayepigwa vita nchini humo Moammer Gaddafi, kuzungumza wazi kwa mara ya kwanza tangu kuanza mapinduzi nchini humo.

Libyen Proteste Demonstration CONTRA Regierung
Maandamano yanaenea mjini Tripoli.Picha: AP

Kiongozi huyo aliuhutubia umma baada ya kuwepo hasira katika ngazi ya kimataifa kuhusu kuzidi kwa misako mikali inayotekelezwa na vikosi vya usalama nchini humo.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa linatarajiwa kukutana hii leo kufuatia ombi la wanadiplomasia wa nchi hiyo waliojiuzulu wakipinga utawala wa Gaddafi.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 68 alihutubia umma hapo jana usiku kupitia televisheni ya taifa na kukanusha kukimbia kwake.

Alisema kuwa atakutana na vijana katika uwanja wa kijani kuwaonyesha kuwa bado yupo Tripoli na sio nchini Venezuela.

Licha ya tangazo hilo fupi, udhibiti wa Gaddafi kwa Libya ulionekana kuzidi kutetereka wakati viongozi katika utawala wake walijiuzulu huku marubani wa ndege za kivita wakisaliti amri ya kuwashambulia waandamanaji.

Unruhen in Libyen
Picha: AP

Viongozi wajiuzulu Libya

Wanadiplomasia nchini humo kutoka Umoja wa mataifa na Australia aidha walilalamika wazi au walijiuzulu pia kwa hasira, akiwemo pia balozi wa nchi hiyo nchini India, Ali al Essawi ambaye alikuwa waziri wa biashara.

Al Essawi aliliambia shirika la habari la AFP kuwa amejiuzulu kutokana na vurugu kubwa dhidi ya raia nchini mwake.

Inasemekana pia waziri wa sheria nchini humo, Mustapha Abdeljalil pia alijiuzulu katika kupinga utumiaji mkubwa wa nguvu dhidi ya raia.

Libyen Unruhen Gaddafi Bengasi 20.02.2011
Picha: picture alliance/dpa

Mapinduzi yameenea katika mji mkuu huku milio ya risasi ikisikika mjini humo ambapo waandamanaji walivishambuliwa vituo vya polisi, kuiwasha mijengo ya serikali moto, na kuzishambulia pia ofisi nyingine za shirika la kitaifa la habari ambalo hutumiwa na Gaddafi.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanasema misako inayotekelezwa na serikali imesababisha vifo vya watu kati ya 200 hadi 400.

Wakaazi wa wilaya mbili mjini Tripoli walisema kupitia njia ya simu kuwa pamekuwa na mauaji huku watu waliokuwa na bunduki wakifyatuwa risasi kila mahali katika wilaya ya Tajura.

Mkaazi mwingine katika wilaya ya Fashlum alisema helikopta zilituwa katika eneo hilo zikiwa na mamluki wa Kiafrika , waliofyatuwa risasi kwa yoyote waliyemuona barabarani na kuwauwa watu wengi.

Kituo cha taifa cha habari kilimnukuu hapo jana mwanawe Gaddafi, Seif al Islam, aliyesema kuwa jeshi lilianzisha mashambulio kwenye ghala za silaha nje ya maeneo ya miji, na alikanusha kuwa jeshi liliyaripuwa miji ya Tripoli na Benghazi.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Afpe
Mhariri: Josephat Charo