Fedha yatumika kuwashawishi wapigakura - ACFIM | Uganda Yaamua 2016 | DW | 25.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Uchaguzi Mkuu Uganda 2016

Fedha yatumika kuwashawishi wapigakura - ACFIM

Matokeo ya uchunguzi uliofanywa kuhusu matumizi ya pesa katika kampeni za uchaguzi nchini Uganda yanadhihirisha kuwa wagombea wote kwenye ngazi ya urais na ubunge wanawashawishi wapigaji kura kwa kuwahonga fedha.

Chama tawala cha NRM kinatajwa na uchunguzi huo kuwa hadi sasa ndicho kilichotumia kiasi kikubwa zaidi cha pesa, kwani katika kipindi cha miezi miwili pekee ya Novemba na Desemba kilitumia takribani dola milioni 33 za Kimarekani.

Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia matumizi ya pesa katika kampeni, ACFIM, kampeni zote zinazoendeshwa nchini Uganda zinagharimu kiasi kikubwa cha pesa. Wadau wa shirika hilo wakiwemo wale kutoka Transparency International wanasema wanasiasa wanatumia kiwango cha juu cha umasikini miongoni mwa watu hasa vijijini kuwahonga kwa pesa badala ya kunadi sera zao.

Henry Muguzi, ambaye ni mratibu wa kitaifa wa shirika hilo, anasema utafiti huo huenda ukawa umeshusha idadi kamili ya fedha zinazotumika, kwani wanasiasa na vyama hawana madaftari yanayohifadhi jinsi wanavyotumia pesa hizo. Rais Yoweri Museveni anayegombea tena nafasi hiyo ndiye aliyetumia kiasi kikubwa cha pesa kuliko wapinzani wake. Kulingana na utafiti huo, yeye na chama chake NRM walitumia kiasi cha shilingi bilioni 127 takribani sawa na dola milioni 33.

Kundi la wangalizi wa Umoja wa Ulaya liliahidi kufuatilia matumizi ya pesa za kampeni pamoja na kule zinakotoka, lakini kwa mtazamo wa mratibu huyo wa ACFIM si rahisi kubaini pesa anazotumia Rais Museveni kama mgombea na pia kwa mujibu wa nafasi yake kama rais wa sasa.

Ingawa baadhi ya watu waliozungumza na DW mjini Kampala wanamshutumu zaidi Rais Museveni kwa kutumia kiasi hicho kikubwa cha pesa, lakini wafuasi wake wanasema kiongozi wao huyo anatimiza ahadi zake kwa wananchi.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com