1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Fatima al-Fihri: Mwasisi wa chuo kikuu kikongwe duniani

Yusra Buwayhid
28 Aprili 2020

Katika mji wa Fez nchini Morocco, Fatima al-Fihri alijenga msikiti uliokuja kuwa Chuo Kikuu maarufu cha al-Qurawiyyin. Leo hii kinatambuliwa kama chuo kikuu kikongwe zaidi ulimwenguni kinachoenedelea kutoa masomo.

https://p.dw.com/p/3bVFO
Projekt African Roots

Fatima al-Fihri: Mwasisi wa chuo kikuu kikongwe duniani

Fatima al-Fihri ni nani ?

Fatima al-Fihri alizaliwa mwaka 800 BK. Alikuwa ni binti wa Mohammed Bnou Abdullah al-Fihri – mfanyabiashara tajiri aliyehamia mjini Fez na familia yake wakati wa utawala wa Idris II. Hadi hii leo, maisha ya Fatima ni yenye siri kubwa hata kwa wanahistoria. Siri moja wapo ni tarehe yake ya kifo ambayo inadhaniwa huenda ilikuwa mnamo mwaka 878.

Wakati wa uhai wake, Fatima alipewa jina la ‘Mama wa wavulana'. Kulingana na mwanahistoria Mohammed Yasser Hilali, ‘jina hili la utani yumkini limetokana na ukarimu wake na tabia yake aliyokuwa nayo ya kuwalinda na kuwatunza wanafunzi wake.'

Kwanini Fatima al-Fihri aliamua kujenga msikiti ?

Fatima alikuwa ni muumini. Aliporithi kiwango kikubwa cha fedha baada ya baba yake na mume wake kufariki, aliamua kujenga msikiti uliokuwa ukihitaji katika jamii yake ya Waislamu mjini Fez, ambao utakuwa na nafasi ya kutosha kujaza idadi kubwa ya waumini.

Baada ya kununua ardhi kutoka kwa mtu wa kabila la "Hawaara", Fatima alianza ujenzi mwanzoni mwa mwezi wa Ramadhani mwaka 254 Hijra ambao sawa na 859 BK.

Kuanzia karne ya 10 msikiti huo maarufu wa al-Qarawiyyin ukawa taasisi ya kwanza ya kidini duniani, na chuo kikuu kikubwa cha Kiarabu eneo la Afrika Kaskazini. Ulivutia wanafunzi wengi na wanasayansi mashuhuri.

Majadiliano ya kidini ya mara kwa mara yalifanyika katika msikiti huo. Kulingana na ushahidi wa nyaraka zilizopatikana, viti vya kukalia wakati wa mafundisho viliwekwa kwenye chuo hicho na katika majengo mengine madogo ya elimu kote mjini Fez. Nyaraka hizo pia zinataja kuwepo kwa idadi kubwa ya maktaba wakati huo katika mji wa Fez.

Projekt African Roots
Asili ya Afrika | Fatima al-Fihri

Kwanini chuo cha al-Qarawiyyin kikapata umaarufu mkubwa ?

Chuo kikuu cha al-Qarawiyyin kinachukuliwa kuwa ni chuo kikuu cha zamani zaidi duniani ambacho bado kinafanya kazi, kabla ya vyuo vikuu vya kwanza vya Ulaya. Kulingana na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, tarehe ya kumbukumbu inayotumiwa ni mwaka al-Qarawiyyin ulipoanzishwa kama msikiti, na hilo linamaanisha kwamba msikiti huo ulitumika kwa ajili ya kutoa elimu tangu kufunguliwa kwake. Kwa mantiki hii, unautangulia kwa zaidi ya karne moja hata msikiti mkongwe wa Sankore huko Timbuktu (uliofunguliwa mwaka 989 BK) na kwa zaidi ya karne mbili Chuo Kikuu cha Bologna (kilichoanzishwa mwaka 1088 BK).

Wahitimu wake ni pamoje na mshairi, Faqîhs (mtaalamu wa sheria za Kiislam), wanafalaki (wasomi wa matukio ya ulimwengu kwa ujumla nje ya anga ya dunia) na wanahesabati kutoka katika kila pembe ya eneo hilo. Majina mengine ya watu mashuhuri waliohitimu katika chuo cha al-Qarawiyyin ni pamoja na mwanahistoria, Abdurahman Ibn Khaldun, daktari na mwanafalsafa Abu Walid Ibn Rushd, daktari mwengine kutoka Andalusia, Uhispania Musa Ibn Maimonou na Gerbert of Aurillac aliyekuja kuwa Papa Sylvester II.

Fatima al-Fihri: Mwasisi wa chuo kikuu kikongwe duniani

Fatima al-Fihri anakumbukwa vipi ?

Fatima al-Fihri alikuwa ni mchamungu na akiheshimiwa miongoni mwa waumini wa Kiislam hasa mjini Fez. Mnamo mwaka 2017, kulianzishwa tuzo maalumu nchini Tunisia iliyopewa jina lake. Tuzo hiyo inatunukiwa miradi inayohimiza upatikanaji wa mafunzo na majukumu ya kitaalam kwa wanawake. Aidha, kumeanzishwa programu ya masomo na ufadhili wa masomo hayo kwa jina la Fatima al-Fihri, inayotolewa kwa wanafunzi wa Afrika Kaskazini na Ulaya ili kuiendeleza kumbukumbu ya mwanamke huyo mashuhuri.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.