FAO yatoa ripoti ya chakula 2012 | Masuala ya Jamii | DW | 06.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

FAO yatoa ripoti ya chakula 2012

Ripoti kuhusu hali ya chakula duniani kwa mwaka 2012 iliyotolewa leo na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa-FAO, imeonyesha kuwepo makadirio mapya ya hali ya ukosefu wa chakula duniani.

Nembo ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa

Nembo ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa

Ripoti hiyo ya mwaka inayosisitiza zaidi juu ya umuhimu wa kuongeza kiwango cha uwekezaji katika kilimo ili kusaidia kupunguza njaa na umasikini duniani iliyozinduliwa leo mjini Roma, imeonyesha kwamba mafanikio katika kupunguza tatizo la njaa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita yameongozeka kuliko ilivyokuwa ikiaminika hapo kabla. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, huenda malengo ya Maendeleo ya Milenia kuhusu kupunguza njaa na umaskini yatafikiwa ifikapo mwaka 2015, kutokana na makadirio mapya ya lishe kuboreshwa kwa mbinu na mikakati mbalimbali. Mafanikio mengi yalipatikana hasa katika kipindi cha mwaka 2007 na 2008 na tangu wakati huo, mafanikio ya kupunguza njaa yalianza kupungua. Hata hivyo, idadi ya watu wanaokabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa chakula cha kutosha bado iko juu na jitihada za kumaliza tatizo la njaa bado linabakia kuwa changamoto kubwa duniani.

Watu 870 wanakabiliwa na njaa duniani

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa idara ya Kilimo, Maendeleo na Uchumi katika Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, Kostas Stamoulis amesema kuwa kiasi watu milioni 870 duniani wanakabiliwa na njaa na kati ya hao, milioni 852 ni kutoka mataifa yanayoendelea. Stamoulis amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 12.5 ya watu duniani kote wanaokabiliwa na njaa. Ripoti ya mwaka huu pia inaelezea mchango wa ukuaji wa uchumi katika kupunguza tatizo la ukosefu wa chakula cha kutosha. Ukuaji endelevu wa kilimo mara nyingi umekuwa na ufanisi kwa watu maskini kwa sababu wengi wao wanaishi katika maeneo ya vijijini na wanategemea kilimo kama sehemu kubwa ya maisha yao. Hata hivyo, ukuaji huo haumaniishi kwamba ni lazima uongeze lishe bora kwa watu wote. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sera na mipango ambayo itahakikisha ukuaji wa lishe bora, ni pamoja na kusaidia kuongeza malazi tofauti, kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, usafi wa mazingira na huduma nzuri za afya pamoja na kuwaelimisha watumiaji kuhusu lishe bora ya kutosha na suala la kutoa malezi bora kwa watoto.

Ukuaji wa uchumi unachukua muda kuwafikia maskini

Mahindi yakiwa yameanikwa juani ili kuhifadhiwa

Mahindi yakiwa yameanikwa juani ili kuhifadhiwa

Aidha, ripoti hiyo ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2012 inafafanua kwamba ukuaji wa uchumi unachukua muda kuwafikia watu maskini na kwamba huenda usiwafikie kabisa wale walio maskini zaidi duniani. Kutokana na hali hiyo, ulinzi wa kijamii ni muhimu katika kutokomeza tatizo la njaa haraka iwezekanavyo. Ripoti hiyo imebaini kuwa maendeleo ya haraka katika kupunguza tatizo la njaa na utapiamlo yanahitaji serikali kuchukua hatua na kuweka mikakati ili kuhakikisha zinatoa huduma nzuri za kijamii ndani ya mfumo wa utawala kwa kuzingatia uwazi, ushirikishwaji, uwajibikaji, utawala wa sheria pamoja na haki za binaadamu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/FAO Website,RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com