1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EAC yakanusha kudumaa kiuchumi

Mohammed Khelef
13 Agosti 2019

Jumuiya ya Afrika Mashariki imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la kila wiki la "The East African" kwamba jumuiya hiyo inapitia kipindi kigumu kiuchumi huku baadhi ya wafanyakazi wakiacha kazi kwa kutolipwa.

https://p.dw.com/p/3NqXX
Tansania Amtseinführung Pombe Magufuli
Picha: picture alliance/AP Photo/K. Said

Jumamosi ya Agosti 10, gazeti hilo linalochapishwa kwa lugha ya Kiingereza nchini Kenya liliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari: "EAC staff desert duty, return home as cash crunch bites", yaani "Wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wayakacha maofisi yao, wakirudi majumbani kutokana na ukata" unaoikabili jumuiya hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba kwa sasa jumuiya hiyo inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi inayosababisha kushindwa kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wake, huku baadhi ya miradi ikisogezwa mbele.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne 8Agosti 13), Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Stivine Mlote, amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote.

Taarifa zinazodai kuwepo kwa ukata katika jumuiya hiyo kongwe barani Afrika zinaeleza kwamba wafanyakazi hasa ambao sio Watanzania wamerudi nchini mwao kutokana na kutolipwa mishahara, hali ambayo jumuiya hiyo imeikanusha.

Mlote alisema kuna wafanyakazi 14 ambao walikuwapo likizo, wafanyakazi 11 wakiwa nje ya ofisi kwa shughuli mbalimbali za kikazi na mfanyakazi mmoja yupo likizo ya uzazi na "si kweli kwamba watu hao wameondoka kazini kwa sababu ya kutolipwa mishahara".

Jumuiya ya Afrika Mashariki inatimiza miaka 20 tangu ilipofufuliwa upya ikizihusisha sasa nchi sita za ukanda wa Maziwa Makuu ambazo ni Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini iliyojiunga mwaka 2016.

Naibu Katibu Mkuu Mlote alisema kamwe jumuiya hiyo haiwezi kutetereka wala kufa na itaendelea kuwa jumuiya ya mfano Afrika na duniani kwa ujumla.

Veronica Natalis/DW Arusha