Dunia yaungana na Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 03.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Dunia yaungana na Kenya

Dunia inaungana na Kenya kufuatia mauaji ya kikatili dhidi ya wanafunzi 147 wa Chuo Kikuu cha Garissa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo yaliyofanywa na wanamgambo wa kundi la al-Shabaab.

Wanajeshi wa Kenya kwenye eneo la tukio, Chuo Kikuu cha Garissa.

Wanajeshi wa Kenya kwenye eneo la tukio, Chuo Kikuu cha Garissa.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alituma salamu zake za rambirambi kwa serikali ya Kenya siku ya Ijumaa (Aprili 3) akiliita tukio hili kuwa la kinyama na kikatili, ambalo lazima lilaaniwe vikali. Mohamud amesema anaungana na Wakenya kwenye msiba huu mkubwa ambao umeondoka na maisha ya vijana wasio hatia.

"Nina hakika kwamba tutayashinda makundi haya ya kigaidi. Wakenya wamejitolea maisha yao kuleta amani kwenye nchi yetu na ninajuwa kuwa magaidi hawafurahikii msaada huu," alisema Mohamud kwenye salamu hizo, ambaye pia alitumia salamu hizo pia kutaka ushirikiano wa usalama kati ya Kenya na Somalia uimarishwe zaidi.

Mapema Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana-Dlamini Zuma, alisema kitendo kilichofanywa na al-Shabaab ni cha watu waoga, ambao hawawezi kukabiliana na wapinzani wao kwenye uwanja wa vita. Zuma ameisifu Kenya kwa kuendelea kuwa imara katika ushiriki wake kwenye Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye kupitia ofisi yake aliahidi kuendelea kushirikiana na Kenya kwenye jitihada zake za kukabiliana na ugaidi na upandikizwaji wa siasa kali.

Marekani kuisaidia Kenya

Kenia Attentat in Garissa

Baadhi ya wanafunzi waliofanikiwa kukimbia wakiwa hawana chochote zaidi ya nguo za mwilini.

Ikulu ya Marekani kupitia msemaji wake Josh Earnest imesema nchi hiyo inaungana na Wakenya ambao kamwe hawatayumbishwa na vitendo kama hivi vya kigaidi. Rais Barack Obama anatazamiwa kuizuru Kenya mnamo mwezi Julai, ikiwa ni ziara yake ya kwanza akiwa rais kwenye taifa hilo alilozaliwa baba yake mzazi.

Kwenyewe nchini Kenya, magazeti yameamka na vichwa vya habari vyenye mchanganyiko wa huzuni na lawama kwa serikali, kwa kile yanachosema ni kushindwa kwake kuzichukulia hatua taarifa za kijasusi zilizokwishaonesha mapema uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi hayo yaliyoangamiza hadi sasa roho za vijana 147.

Gazeti la The Star limeandika kwenye tahariri yake kwamba "mashambulizi hayo yalibashiriwa kwenye taarifa kadhaa za kijasusi" huku gazeti la The Standard likisema kwamba licha ya taifa kukabiliana na jinamizi la mashambulizi ya jana "Wakenya wanapaswa kujuwa kuwa adui yao anataka kuwachonganisha."

Awali ilisemekena kuwa washambuliaji wanne ambao waliingia kwenye jengo la chuo hicho kikuu cha Garissa waliwagawa mateka wao kati ya Waislamu na wasio Waislamu na kisha kuanza kuwauwa wale waliowaona kutokuwa Waislamu. Kwa mujibu wa gazeti la The Standard kitendo hicho kilikusudiwa kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambayo matokeo yake yatakuwa umwagakaji zaidi wa damu.

Wimbi la huzuni

Mtu anayeshukiwa kupanga mashambulizi hayo, Mohamed Mohamud.

Mtu anayeshukiwa kupanga mashambulizi hayo, Mohamed Mohamud.

Hadi asubuhi ya Ijumaa, bado jinamizi la mkasa huo lilikuwa linaendelea kuutawala mji wa Garissa. Idadi kubwa ya wanajeshi walionekana kwenye lango la kuingilia chuo kikuu hicho, huku marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku ikiendelea.

Wafanyakazi wa kujitolea waliendelea kukusanya miili ya wanafunzi iliyotapakaa ndani ya chuo, huku vikosi vya usalama vikiendelea kuhakikisha usalama wa eneo hilo ambalo lilikuwa uwanja wa mapambano kwa takribani siku nzima.

Wanafunzi kadhaa waliofanikiwa kukimbia wakiwa hawana chochote zaidi ya nguo zao mwilini, waliupitisha usiku wa kuamkia leo kwenye kambi za kijeshi, ambako walipewa chakula na nguo na wasamaria wema wa Garissa.

Kampuni kadhaa za usafiri zilijitolea kuwasafirisha wanafunzi hao, wanaoelezewa kuelemewa na fadhaa na khofu, kurudi majumbani kwao. Miili ya wenzao waliouawa inapelekwa kwenye jengo la kuhifadhia maiti jijini Nairobi, ambako baadhi ya wazazi na jamaa wamekusanyika wakingojea kuwatambua wapendwa wao.

Serikali iliwasihi wazazi kuwa na subira wakati wakifuatilia majaaliwa ya watoto wao, huku mwandishi wa shirika la habari la AFP akiripoti kundi kubwa la wazee na jamaa waliokusanyika kwenye jengo la chuo hicho.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa, Joseph Nkaissery, anasema kamwe Kenya haitapinda magoti mbele ya kundi la kigaidi la al-Shabaab, ambalo limekiri kufanya mauaji hayo. "Serikali ya Kenya haitatishwa na magaidi hawa ambao wamegeuza mauaji dhidi ya watu wasio hatia kuwa ndio njia ya kuidhalilisha serikali. Badala yake tuna dhamira ya dhati kupambana nao na nina hakika tutashinda," Nkaissery aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye eneo la tukio, ambaye pia alitangaza chuo hicho kufungwa kwa muda usiojuilikana.

Haya ni mauaji makubwa zaidi kuwahi kufanywa kwa wakati mmoja nchini Kenya tangu yale ya ubalozi wa Marekani jijini Nairobi mwaka 1998, ambapo watu 213 walipoteza maisha kufuatia mashambulizi ya mtandao wa al-Qaida.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com