Dunia yaomboleza kifo cha Mandela | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Dunia yaomboleza kifo cha Mandela

Viongozi mbalimbali wa dunia wakiwemo rais Barack Obama wa Marekani, katibu Mkuu wa Umoja wa Mazaifa ban Ki-Moon na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, wametoa hisia zao juu ya kifo cha mzee Nelson Mandela.

Marehemu Nelson 'Madiba' Mandela.

Marehemu Nelson 'Madiba' Mandela.

Wamefariki mabingwa wa kuendesha shughuli za serikali, viongozi wa mavuguvugu ya upinzani, washindi wa tuzo ya Nobel na watu wengine maarufu hapoa kabla. Lakini haijawahi kutokea katika historia, mtu mmoja akaiunganisha dunia katika kumkumbuka baada ya kifo chake kama alivyofanya Mandela.

Rais Barack Obama.

Rais Barack Obama.

Katika kuashiria orodha ya wageni wa utakaokuwa msiba muhimu zaidi katika kipindi cha miongo kadhaa, viongozi wa dunia wamejipanga moja baada ya mwingine, kutoa heshima kwa kiongozi huyo ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, aliefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Si wa kwetu tena
"Alipata mafanikio makubwa zaidi kuliko ambavyo ingetarajiwa kwa mtu yeyote, na leo amerudi nyumbani. Alikuwa mmoja wa watu waliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi, wazuri zaidi na wenye uthubutu kuwahi kuwepo katika wakati wetu. Si wa kwetu tena, ni wa zama.

Kutokana na utayari wake kutoa uhuru wake kwa ajili ya uhuru wa wengine, Madiba aliibadilisha Afrika Kusini na kutuhamasisha sisi. Safari yake kutoka gerezani hadi kuwa rais, ilituonyesha kwamba wanadamu na mataifa yanaweza kubadilika kuwa bora.

Dahmira yake ya kukabidhi madaraka, na kufanya maridhiano na wale waliomfunga, viliweka mfano ambao binaadamu wote wanafaa kuiga," alisema rais wa Marekani Barack Obama katika hotuba yake kwa waandishi wa habari baada ya kupata habari za kifo cha Mandela.

Mara kwa mara, viongozi walikuwa wakizungumzia heshima alioionyesha wakati wa kifungo kirefu alichopewa na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini na baadaye, alipoliongoza taifa lake kutawaliwa na walio wengi. Huenda tusipate tena watu kama Mandela, alisema Obama, rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika, akielezea kuachiwa kwa Mandela kutoka gerezani kama moja ya mambo yaliyomhasisha kisiasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Bingwa wa haki
Akizungumza na niaba ya Umoja wa Mataifa, katibu Mkuu Ban Ki-Moon alimtangaza Mandela kama bingwa wa haki. "Nelson Mandela alionyesha nini kinawezekana kwa dunia yetu, na dani ya kila mmoja wetu, kama tunaamini kwamba tunaweza kutembe pamoja kwa ajili ya haki na ubinaadamu." Katibu Mkuu Ban alisema watu wengi duniani walihamasishwa na mapambano yake ya kujitolea kwa ajili ya kuheshimu utu, kuwepo na usawa na uhuru.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema daima jina la Nelson Mandela litakuwa nembo ya mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi- Apartheid. Merkel amemsifu Mandela kama shujaa ambaye dhamira yake njema haikuvunjwa na minyororo ya jela, na kuongeza kuwa ujumbe wake wa maridhiano utaendelea kuwa nuru ya kuhamasisha vita dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji kote duniani.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Naye waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye mwaka 2006 aliomba radhi kwa kile alichosema ni makosa ya chama chake cha kihafidhina katika kushughulikia ubaguzi wa rangi katika koloni la zamani la Uingereza, alikuwa na haya ya kumuelezea Mandela.

"Usiku huu, moja wa mianga inayoingarisha zaidi dunia yetu umezimika. Nelson Mandela hakuwa tu shujaa wa wakati wetu, bali shujaa wa wakati wote. Rais wa kwanza wa Afrika Kusini iliyo huru, mtu ambaye aliteseka sana kwa ajili ya uhuru ya haki, namtu ambaye kupitia heshima yake na ushindi, aliwahamasisha mamilioni. Usiku huu, familia nchini Uingereza zitaomboleza pamoja na familia yake na kila mmoja nchini Afrika Kusini," alisema waziri Mkuu Cameron.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Hisia nzito
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius alimuelezea Mandela kama mtu haiba ya kipekee, na kuongeza kuwa baba wa taifa la Afrika Kusini amefariki, mnara wa uhuru kiongozi wa maridhiano. Viongozi wastaafu ambao walimkumbuka Mandela wakati wa kifungo chake cha miaka 27, au waliowahi kufanya naye kazi pia walikuwa na hisia kali.

Rais wa zamani wa Marekani George Bush, ambaye alimualika Mandela katika ikulu ya White House baada ya kuachiwa kwake, alimuelezea kama muumini mkubwa zaidi katika uhuru aliebahatika yeye na mkewe Barbra kumfahamu. Alisema akiwa rais, aliangalia kwa kustajaabu, wakati Mandela akiwasamehe watu waliomfunga.

Rais mwingine mstaafu wa Marekani Bill Clinton, aliweka picha aliyopiga pamoja na Mandela kwenye mtandao wake wa twitter, na kuiongezea maneneo yasemayo: Leo dunia imempoteza mmoja wa viongozi wake mahiri binaadamu wa kipekee.

Alikuwa kipenzi cha Waafrika Kusini na ulimwengu mzima.

Alikuwa kipenzi cha Waafrika Kusini na ulimwengu mzima.

Ni hisia za dunia nzima
Barani Afrika na sehemu nyingine za dunia zilizopambana na ukoloni, kulikuwepo na hisia kali. Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, alimuelezea Mandela kuwa ni mmoja wa wakombozi wakubwa zaidi wa binaadamu, na rais Enrique Piena Nieto wa Mexico, alisema dunia imempoteza mpiganaji mahiri wa amani, uhuru na usawa.

Rais wa Brazil Dilma Rousseff alisema mfano wa kiongozi huyo mkubwa utawaongoza wale wote wanaopigania haki za kijamii na mani duniani. Wafannyabishara wakubwa duniani, akiwemo tajiri nambari moja Bill Gates, wakuu wa mashirika ya kimataifa, waandishi wa vitabu, waburudishaji, wanamichezo na wanaharakati, nao wameeleza hisia zao juu ya kifo cha Mandela.

Mandela alikumbukwa pia na wasanii wa Hollywood, ambako filamu mpya inayoelezea maisha ya kiongozi huyo wa Afrika Kusini iliyopewa jina la "Long Walk to Freedom" imezinduliwa muda mfupi uliyopita.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre, dpae
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com