Dunia yamuaga Kofi Annan | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Dunia yamuaga Kofi Annan

Waombolezaji wanatoa heshima zao za mwisho kwa katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kabla ya mazishi yake. Annan alifariki dunia Agosti 18 akiwa na umri wa miaka 80 katika hospitali nchini Uswisi.

Ghana Trauer um Kofi Annan

Wanajeshi wakilinda jeneza ya Kofi Annan katika kituo cha kimataifa ya mikutano mjini Accra.

Viongozi wa sasa na wastafu wa dunia, watawala wa kijadi na watu wengine mashuhuri wanahudhuria sherehe ya kumuaga Annan, inayofanyika katika jumba la mikutano ya kimataifa mjini Accra, ikiashiria mwisho wa siku tatu za maombolezi kwa mwanadiplomasia huyo anaeheshimika kote duniani.

Annan aliuongoza Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1997 hadi 2006 na alikuwa mtu wa kwanza kutoka kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kushika wadhifa huo. Katibu Mkuu wa sasa wa chombo hicho cha kimataifa, Antonio Guterres, alitarajiwa kuhudhuria tukio la kumuaga mtangulizi wake, ambalo litafuatiwa na mazishi ya faragha katika makaburi ya kijeshi ya mji mkuu Accra.

Rais wa nchi jirani ya Cote di'Voire pamoja na viongozi wa Liberia, Namibia, Ethiopia, Niger na Zimbabwe, pia wamethibtisha kuhudhuria hafla ya kumuaga Annan kwa mujibu wa waziri wa mamwasiliano wa Ghana. Wakuu wa zamani wa mataifa kuanzia Ujerumani had Mauritius pia wamewasili Ghana kuhudhuria sherehe za kumuaga Annan.

Ghana Trauer um Kofi Annan

Machifu ya kikabila na wanafamilia wakisubiri kutoa heshima zao kwa Kofi Annan.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo ameitaja sherehe hiyo kuwa tukio muhimu kwa nchi hiyo, na kumuelezea Annan kama mmoja ya watu mashuhuri zaidi wa kizazi hiki. Wa Ghana wa kawaida na wageni wametoa heshima zao kwa Annan tangu jeneza lake liliporejeshwa kutoka Geneva na kupokelewa kwa heshima kamili siku ya Jumatatu.

Safari yake ya maisha

Annan alizaliwa Aprili 8, 1938, na alikulia mjini Kumasi na dada yake pacha Atta na alitumia miaka yake ukuaji katika mji wake wa nyumbani. Lakini licha ya maisha yake ya kikazi kumpeleka mbali kabisaa na nyumbani, hakupoteza mawasiliano na familia yake.

Familia ya Anna aliamini pakubwa katika maadili ya elimu, na kama mtoto, Annan alikuwa mwanafunzi mwenye shauku. Harakati zake za kujiendeleza zilimfikisha nchini Marekani, amabko alisomea uchumi jimboni Minnesota, na menejimenti katika taasisi ya teknolojia ya Massachusetts.

Baadae alihamia nchini Uswisi na kusomea Uhusiano wa kimataifa. Alijiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 962 ambako alifanya kazi katika ofisi ya Geneva ya shirika la afya duniani WHO, kabla ya kupanda hadi nafasi ya juu kabisaa ya Umoja wa Mataifa.

Annan alijijengea sifa kama mwanadiplomasia wa juu kabisaa duniani na aliufufua Umoja wa Mataifa katika milenia mpya. Juhudi zake zilipelekea umoja huo kupewa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2001, kutokana na kazi yao ya kuleta amani duniani.

Ghana Trauer um Kofi Annan

Jeneza la Kofi Annan lilipowasili Ghana kutoka Uswisi siku ya Jumatatu. Anna anazikwa Alhamisi 13, 09, 2018.

Haki za binadamu na mustakabali wa vijana

Annani pia aliweka msisitizo juu ya masuala ya haki za binadamu, huku akiwa na maono ya mustakabali bora kwa vijana kote duniani. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kilele wa One Young World mjini Johanneburg mwaka 2013, Annan alisema:

"Mna upeo mpana. Hakuna mipaka kwa mnachoweza kufanikisha. Nyinyi ndiyo kizazi bora tulichowahi kuwa nacho."

Wakati akimaliza muhula wake wa ukatibu mkuu wa UN, Anna alikuwa kiongozi maarufu na anaetambulika wa Umoja wa Mataifa, na alichukuliwa kama nyota wa diplomasia katika duru za kimataifa. Aliendeleza kazi yake ya diplomasia, akichukuwa majukumu nchini Kenya na Syria, na hivi karibuni zaidi alikuwa kiongozi wa tume ya ushauri nchini Myanmar kuhusu mgogoro katika jimbo la Rakhine.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, rtrv,dpae

Mhariri: Mohammed Khelef