1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dresden yakumbuka maangamizi ya 1945

Abdu Said Mtullya13 Februari 2015

Unatimu mwaka wa 70 tokea majeshi ya nchi yaliyofungamana dhidi ya fashisti Hitler kuushambulia kwa ndege mji wa Dresden, mashariki mwa Ujerumani. Maalfu ya watu walikufa kutokana na mashambulio hayo.

https://p.dw.com/p/1EbGH
BdT Bildkombo Dresden Bonitas Skulptur EINSCHRÄNKUNG
Picha: picture-alliance/dpa/Deutsche Fotothek/Richard Peter sen.

Habari juu ya idadi ya vifo zinatafautiana. Baadhi wanasema watu 70,000 walikufa ,wengine wanasema watu 35,000 waliuliwa na wengine wanasema waliouawa walikuwa 25,000 kutokana na mashambulio ya ndege yaliyofanywa tarahe 13,14 na 15 katika mji huo wa Dresden.

Mwanzo wa mashambulio

Mashambulio ya mji huo yalianza tarehe 13. Ndege 245 aina ya Lancaster ziliruka kutokea Uingereza kuelekea mji wa Dresden. Wakati huo mji huo ulikuwa na wakaazi 630,000 na maalfu ya wakimbizi. Lakini mji huo haukuwa na umuhimu kijeshi wala kiuchumi hata kidogo.Na hatahivyo hatima ya vita ilikuwa tayari imeshajulikana mnamo mwaka wa 1944. Majira ya saa tatu na dakika 39 usiku, ving'ora vilisikika katika mji wa Dresden.

Gedenken an die Zerstörung Dresdens
Mji wa Dresden ulivyokuwa baada ya mashambulizi hayoPicha: picture-alliance/dpa

Maalfu kwa maalfu ya mabomu yalidondoshwa katika mji huo uliokuwa maarufu kutokana na majengo yake mazuri na tunu zake za kitamaduni.

Mji uliwaka moto. Katika muda mfupi wa dakika 23 mji huo uliwaka moto kiasi kwamba marubani wa Uingereza waliripoti kutokea umbali wa kilometa zaidi ya mia tatu kwamba mji huo ulikuwa unawaka moto.

Marubani waliweza kuuona mji ukiungua kutokea angani umbali wa mita 6700. Joto lilikuwa kubwa la kuyeyusha kioo.cEneo la kilometa 15 za mraba liliteketezwa na mabomu yaliyodondoshwa na ndege za Ungereza na kufuatia baade na ndege za Marekani.

Sir Arthur ndiye aliesimamia mashambulizi

Mamia kwa mamia ya marubani wa Uingereza na Marekani walishiriki katika mashambulio ya kuuteketeza mji wa Dresden, lakini ni mtu mmoja tu aliekuwa msimamizi, Arthur Harris,aliekuwa mkuu wa kikosi cha anga cha Uingereza Royal Air Force. Alikuwa mtekelezaji mkuu wa mpango wa Waziri Mkuu Winston Churchil wa kuishambulia Ujerumani ya mafashisti, yaani mkakati wa kuwavunja ari kabisa maadui.

Kwa nini mji wa Dresden ulishambuliwa?

Baadhi ya wataalamu wa historia walitathmini kushambuliwa kwa mji wa Dresden kuwa ni sehemu ya kuimarishwa uhusiano wa kijeshi baina ya nchi za magharibi na Umoja wa Kisoviet. Mashambulio ya nchi za magharibi dhidi ya Ujerumani ya Hitler yalikuwa yamekwama, katika upande wa magharibi, wakati majeshi ya Umoja wa Kisoviet yalipokuwa yanasonga mbele kwa kasi kubwa , katika upande wa mashariki.

Kanisa na Frauen lililojengwa upya baada ya mashmbulizi.
Kanisa na Frauen lililojengwa upya baada ya mashmbulizi.Picha: picture-alliance/dpa

Palikuwapo na mawazo juu ya kuishambulia miji mingine kama Berlin.Lakini mkuu wa kikosi cha anga cha Uingereza,Royal Air Force , Harris aliyaekeleza macho yake katika mji wa Dresden. Nchi zilizofungama kijeshi dhidi ya Hitler ziliuona mji wa Dresden kuwa na uwezekano mkubwa wa kugeuka maficho ya fashisti Adolf Hitler na manazi wengine.

Jemadari Shukov wa Umoja wa Kisoviet na majeshi yake alikuwapo umbali wa kilometa 80 tu kutoka mji wa Dresden,wakati ndege za Uingereza na za Marekani zilipokuwa zinaupiga mabomu mji huo.

Suala la utatanishi: Mpaka leo mashambulio hayo ni suala la utatanishi kihisia pia nchini Uingereza kwenyewe.

Mwandishi:Wagner Volker
Tafisri:Mtullya Abdu.
Mhariri: Iddi Ssessanga