1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DR Congo: Vifo kutokana na ugonjwa wa surua vyapindukia 6000

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
8 Januari 2020

Shirika la Afya Duniani WHO limesema nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo mlipuko wa ugonjwa wa surua mkubwa zaidi ulimwenguni umesababisha vifo vya maelfu ya watu ijapokuwa ugonjwa huo unaweza kukingwa kwa chanjo

https://p.dw.com/p/3Vsa4
DR Kongo 2016 | Impfung gegen Masern in Otjiwarongo
Picha: Imago Images/Xinhua Afrika

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mlipuko wa maradhi ya surua imepindukia 6,000 katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la afya duniani WHO, ugonjwa huo unasambaa kwa kasi kubwa kabisa nchini humo kuliko kwingineko duniani. Shirika la WHO limesema mikasa ipatayo 3,100 imeripotiwa tangu mwanzoni mwa mwaka uliopita.

Kutokana na hali hiyo serikali ya Congo kwa kushirikiana na shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa zilianzisha mpango wa chanjo mnamo mwezi Septemba mwaka jana. Watoto zaidi ya milioni 18  wamepatiwa chanjo. Hata hivyo juhudi za kuzuia kuenea kwa maradhi hayo zinatatizwa na mashammbulio yanayofanywa kwenye vituo vya  afya, kushindikana watu kufika kwenye vituo vya afya na uhafifu wa miundo mbinu.

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetangaza kwamba idadi hiyo ya vifo kutokana na ugonjwa huo wa surua katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumeifanya hali hiyo kuwa ni janga miongoni mwa majanga makubwa ya milipuko mibaya zaidi ya magonjwa yanayoambukiza kuwahi kutokea duniani.

Kila jimbo nchini Congo yenye jumla ya majimbo 26 ,llimeripoti mikasa ya surua tangu kutangazwa kuzuka kwa maradhi hayo mwezi juni mwaka uliopita. Idadi ya watu waliokufa kutokana na surua imezidi mara mbili ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa homa ya Ebola nchini humo.

Waziri wa Afya wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo Oly Ilunga
Waziri wa Afya wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo Oly IlungaPicha: picture-alliance/AP Photo/Al-Hadji Kudra Maliro

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limesema ukosefu wa fedha, kukosekana chanjo kama inavyopasa na utapiamlo ni sababu zinazokwamisha shughuli za kuokoa maisha, kukabiliana na ugonjwa huo na pia kudhibiti maambukizi mapya nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya WHO imesema takriban visa 310,000 vinavyoshukiwa kuwa ni ugonjwa huo vimeripotiwa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati tangu mwanzoni mwa mwaka 2019. WHO imefanya kazi pamoja na serikali za mitaa kuwapa chanjo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Hata hivyo katika sehemu zingine za nchi, haswa katika maeneo yanayokabiliwa na vurugu, chanjo bado  inatolewa kwa kiwango cha chini huku asilimia 25% ya visa vya ugonjwa wa surua ni kwa watoto walio zaidi ya umri wa miaka mitano, ambao ndio walio hatarini zaidi.

Kwa mujibu wa WHO karibu Dola milioni 28 zimekusanywa za kupambana na ugonjwa huo, lakini Shirika hilo limesema Dola milioni 40 zinahitajika ili kufanikisha mpango wa miezi sita wa kutoa chanjo kwa ajili ya watoto wakubwa walio na umri kati ya miaka 6 na 14.

Ugonjwa wa surua unaweza kusababisha kifo, unaweza kusababisha kichomi, uvimbe wa ubongo au ulemavu wa muda mrefu. Daktari Matshidiso Moeti, Mkurugenzi Mkuu wa WHO kanda ya Africa amesema WHO inafanya kila linalowezekana ili kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo ambao unaweza kuzuilika kwa urahisi kwa chanjo.

Chanzo:/https://p.dw.com/p/3VrrU