1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yakosoa ripoti kuhusu ukiukaji, Xinjiang

Lilian Mtono
1 Septemba 2022

China imeushutumu Umoja wa Mataifa kwa kuwa kibaraka wa Marekani na magharibi baada ya kuchapisha ripoti inayoonya kwamba huenda China ilifanya uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika jimbo lake la Xinjiang.

https://p.dw.com/p/4GKDY
Uiguren China
Picha: Kyodo News/IMAGO

China inaushutumu Umoja huo, wakati Umoja wa Ulaya ukiisifu ripoti hiyo na kulaani vikali madai ya uhalifu huo. 

Ripoti hiyo ya kwanza ya Umoja wa Mataifa kuhusu Xinjiang inaelezea kwa kina visa vya ukiukwaji wa haki vikiwa ni pamoja na mateso na watu wa jamii ya Uyghur na Waislamu, ambao ni jamii ya walio wachache kulazimishwa kufanya kazi, sasa inapigilia msumari wa mwisho wa madai ya muda mrefu yaliyotolewa na makundi ya wanaharakati wa haki za binaadamu, mataifa ya magharibi na watu wa jamii Uyghur wanaoishi uhamishoni.

China inakana vikali madai ya mateso katika jimbo la Xinjiang na imetoa ripoti ya kurasa 131 kujibu ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kurasa 48.

Ripoti hiyo iliyotolewa na mkuu wa shirika la haki za binaadamu anayeondoka Michelle Bachelet imesema kwamba hatua ya China ya kuwazuia kiholela vizuizini watu wa jamii ya Uyghur na Waislamu wengine katika jimbo la Xinjiang inaweza kuchukuliwa kama uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Soma Zaidi: Bachelet akosolewa kwa ziara ya China

Beijing kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Wang Wenbin imekosoa vikali ripoti hiyo ambayo imeandaliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na kuendeleza msimamo wake wa kupinga kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

China I Wang Wenbin I Sprecher des chinesischen Außenministeriums
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin asema ni uongo mtupu na inalenga kuifurahisha Marekani na magharibiPicha: Kyodo/picture alliance

"Hiyo inayoitwa ripoti ya tathmini uliyotaja ilipangwa na kutengenezwa na Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi, na ni kinyume cha sheria na ni batili kabisa. Ripoti hiyo ni mkusanyiko wa taarifa za uongo. Ni chombo cha kisiasa cha kutumikia malengo ya Marekani na magharibi kujaribu kuifitini China. Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa aliibuni ripoti hiyo kwa kuzingatia njama za kisiasa za baadhi ya mataifa yanayopambana na China nje ya nchi. Inathibitisha kwa mara nyingine kwamba Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa mhalifu na mshirika wa Marekani na magharibi." alisema Wenbin.

Huku China ikitoa shutuma kali, Halmashauri ya Umoja wa Ulaya yenye imelaani vikali ukiukwaji wa haki za binaadamu baada ya Umoja wa Mataifa kuchapisha ripoti hiyo na kusema kwa sasa unasoma kwa kina maudhui wa ripoti hiyo na utatoa tamko rasmi katika wakati muafaka.

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja huo amewaambia waandishi wa habari kwamba Umoja huo unalaani vikali ukiukwaji wa haki za binaadamu katika jimbo hilo la Xinjiang na maeneo mengine nchini China, lakini hasa akiangazia mateso ya watu wa jamii ya Uyghurs na wengine wanaotokea katika jamii ya walio wachache, baadhi ya mataifa na imani.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International Agnes Callamard amesema matokeo yake yanakaribiana mno na yale yaliyovumbuliwa na shirika hilo pamoja na la Human Rights Watch.

Amesema ripoti hiyo imebadilisha pakubwa mkondo kuhusiana na madai hayo dhidi ya China.

Uingereza kwa upande wake imesema itaendelea kushirikiana na washirika wa kimataifa kujaribu kubadilsha hatua za China, hii ikiwa ni kulingana na waziri wake wa mambo ya nje Liz Truss hii leo.

Soma Zaidi: China yaidhinisha makambi ya kuwazuilia jamii ya Uighur

Mashirika: RTRE/DW/AFPE