1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChad

Chad yatangaza serikali mpya baada ya utawala wa kijeshi

28 Mei 2024

Waziri Mkuu mpya wa Chad Allamaye Halina ametangaza serikali yake ya kwanza. Hii inaashiria kumalizika kwa miaka mitatu ya utawala wa kijeshi katika taifa hilo la jangwa.

https://p.dw.com/p/4gM5n
Rais Mahamat Idriss Deby
Rais mpya wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno, jenerali wa kijeshi aliapishwa mjini N'djamenaPicha: Israel Matene/REUTERS

Balozi huyo wa zamani nchini China aliteuliwa wiki iliyopita muda mfupi tu kabla ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno, kuapishwa kuwa rais baada ya ushindikatika uchaguzi uliopingwa na upinzani.

Mawaziri waandamizi, wengi wao washirika wa Rais Deby, walijumuishwa katika baraza la mawaziri lililotangazwa kwenye televisheni ya taifa. Serikali hiyo itakuwa na mawaziri 35, ambapo 23 kati yao walihudumu katika serikali ya awali ya Idriss Deby.

Mtangulizi wa Halina, Succes Masra, aligombea urais mapema mwezi huu lakini akashindwa na Deby. Mchumi huyo alikuwa amemaliza miezi minne pekee katika wadhifa huo. Hakuna mawaziri kutoka chama cha Masra cha Transformers waliobakishwa katika serikali mpya. Deby alishinda asilimia 61 ya kura katika uchaguzi wa Mei 6 ambao mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali yalisema haukuwa huru na wa haki.