1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAF kuamua mwenyeji wa Kombe la Afrika

Admin.WagnerD13 Novemba 2014

Shirikisho la Kandanda barani Afrika – CAF linatarajiwa kutangaza nchi itakayokuwa mwenyeji mpya wa dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kuibandua nje na kuipiga marufuku Morocco

https://p.dw.com/p/1DmVu
Werbeball für den Afrika-Cup 2010
Picha: picture-alliance/dpa/B. Fonseca

Lakini bila kujali mahali mashindano hayo yatakapofanyika, Afrika Kusini, Cameroon na Tunisia zitakuwa na kibali cha kucheza katika tamasha hilo la mwaka ujao, kama watashinda mechi zao za kufuzu wikendi hii.

Algeria na Cape Verde tayari zimefuzu katika dimba hilo la mwaka wa 2015 ambalo Morocco ilipokonywa kibali cha kuwa mwenyeji wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Januari 17 hadi Februari 8. Morocco ilisema uamuzi wa kukataa kuwa mwenyeji ulitokana na kitisho cha ugonjwa wa Ebola ambao umewauwa maelfu ya watu katika mataifa ya Afirka Magharibi.

Afrika Kusini inaongoza Kundi A ikiwa na points nane na itacheza mchuano wake wa kwanza tangu mauaji ya nahodha wake Senzo Meyiwa. Kama itaizaba Sudan kesho Jumamosi mjini Durban – mji anakotokea mlinda lango wa klabu ya Orlando Pirates marehemu Meyiwa – utaipa jumla ya points 11.

Senzo Meyiwa Torhüter Südafrika
Aliyekuwa nahodha wa Bafana Bafana, na mlinda lango wa Orlando Pirates marehemu Senzo MeyiwaPicha: Lefty Shivambu/Gallo Images/Getty Images

Kocha Shakes Mashaba ambaye timu yake inaweza bado kupata kibali cha moja kwa moja cha kucheza dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika, kama nambari tatu Nigeria itashindwa kuibwaga Congo mjini Pointe Noire, amesema mchuano huo utakuwa muhimu sana kwa sababu ushindi utakuwa njia nzuri ya kumuaga nahodha wao. Bafana Bafana iliifunga Sudan magoli matatu kwa sifuri mjini Omdurman katika mechi ya kwanza baina ya pande hizo mbili.

Congo na mabingwa wa Afrika Nigeria wanawanasia nafasi katika Kundi hilo la A huku The Super Eagles wakikabiliwa na hatari ya kukosa kufuzu katika dimba hilo lenye nchi 16 baada ya kushindwa na Congo na Sudan katika mechi za awali.

Cameroon ambao wana points kumi, wanatarajiwa kujikatia tikiti kutoka Kundi D kama watapa ushindi mjini Yaounde dhidi ya nambari mbili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Cote d'ivoire inatarajiwa kuirejesha kampeni yake kwenye mkondo sahihi katika kundi hilo wakati ikichuana na Sierra Leone mjini Abidjan baada ya kuwabwaga Leone Stars magoli mawili kwa moja katika mkondo wa kwanza.

Marokkanische Fußballnationalmannschaft
Morocco wamepigwa marufuku baada ya kukataa kuandaa dimba hilo kwa hofu ya kusambaa virusi vya EbolaPicha: AFP/Getty Images/F. Senna

Tunisia pia inaongoza katika Kundi G ikiwa na points 10 na kama itaishinda Botswana hii leo basi itajiwekea nafasi ya kushiriki katika Kombe la Afrika kwa mara ya 17. Senegal na Misri zitakabana koo kesho mjini Cairo, wakati Senegal ikiwa na points saba nayo Misri points sita. Katika mchuano wa kwanza Simba hao wa Teranga waliwashinda wanaFaraoh magoli mawili kwa sifuri.

Wakati Cape Verde ikiwa tayari imefuzu katika Kundi G, mapambano ya tikiti ya pili yatakuwa baina ya mabingwa wa 2012 Zambia na Msumbuji, ambao wote wana points tano kila mmoja. Ni kinyang'anyiro kikali katika Kundi C, huku viongozi Gabon wakiwa mbele ya Burkina Faso na pengo la point moja tu, na timu zote mbili zitacheza ugenini dhidi ya Angola na Lesotho wikendi hii.

Katika Kundi E, Ghana wanaongoza wakiwa na points nane, na watakuwa na mchuano mgumu ugenini dhidi ya Uganda ambao wana points nne. Pia kesho Jumamosi, nambari mbili Togo na points sita wanawakaribisha washika mkia Guinea, ambao wana points nne kufikia sasa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu