1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BVB yarejesha mvuto wa Bundesliga

Sekione Kitojo
29 Oktoba 2018

Borussia Dortmund inaongoza ligi ya Ujerumani lakini Bayern Munich washindi mara nyingi wa ligi ya Bundesliga wanakaribiana na viongozi wa ligi hiyo, wakipishana kwa pointi 2 tu.

https://p.dw.com/p/37LYV
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Hertha BSC
Picha: Reuters/L. Kuegeler

Sare dhidi ya Hertha  Berlin huenda  imekuja  katika  wakati  muafaka kwa  Borussia  Dortmund.  Kikosi  hicho  kimeshindwa  mara  hii kupachika  mabao  manne  ama  zaidi katika  mchezo  wake  pekee katika  michezo  yake  sita  iliyopita, mabao 3-0  dhidi  ya AS Monaco na iliongoza  kwa  pointi  tatu  baada  ya  kusakata kandanda  safi msimu  huu.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Hertha BSC
Jadon Sancho akishangilia bao kwa timu yake ya BVBPicha: Reuters/L. Kuegeler

Ghafla  baada  ya  Bayern Munich kutamalaki  katika  ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga, Dortmund inasaidia  kulifanya  soka  la  Ujerumani  kuvutia  kwa  mara  nyingine tena.

Kikosi  cha  kocha  Lucien Favre kinafananishwa  sasa  na  kikosi alichounda  kocha  nyota  Juergen  Klopp kilichoshinda  ligi  ya Bundesliga  mwaka  2011 na  kufuatiwa  na  ubingwa mwingine mwaka  uliofuatia  na  kushinda  kombe  la  shitikisho  DFB Pokal mwaka  uliofuatia. Kikosi  cha  sasa , kama  kilivyokuwa  cha  Klopp , ni  cha  vijana, kinachofanyakazi  kwa  nguvu, wachezaji  wenye kasi  na  ufundi, kikijiamini  baada  ya  ushindi  wa  kupendeza.

Fussball Bundesliga - BVB Trainer Lucien FavreSaison 2018/2019, 1.Bundesliga: BVB, Borussia Dortmund - Stade Rennes, Trainingslager, Testspiel,
Kocha wa BVB Lucien FavrePicha: picture alliance / augenklick/firo Sportphoto

Lakini  pia  kuna ishara  za  kuimarika  baadhi  ya  timu  hali  ambayo inaifanya  ligi  ya  Bundesliga  kuvutia  kwa  mara  nyingine  tena. Werder  Bremen  ambayo  imekuwa  ikipata  mafanikio  katika michezo  yake  ya  hivi  karibuni, ilijikuta  ikikubali  kipigo  cha  mbwa koko  mbele  ya  Bayer Leverkusen  cha  mabao 6-2  matokeo ambayo  yamewashangaza  wapenzi  wa  kandanda. Werder Bremen ambayo  ilikuwa  nyumbani  ilipata  kipigo  hicho  wakati  ilikuwa ikishikilia  nafasi  ya 2  katika  msimamo  wa  ligi, na  sasa imeporomoka  hadi  nafasi  ya  4.

Fußball Bundesliga Werder Bremen - TSG 1899 Hoffenheim
Kocha wa Werder Bremen Florian KohfeldtPicha: picture-alliance/dpa/C. Jaspersen

Kohfeldt aelezea  kuhusu kipigo

Kocha  wa  Werder  Bremen Florian Kohfeldt ameelezea  kipigo hicho  kuwa  kinatokana  na  kosa  la  uchaguzi  wa  mbinu kuingia katika  mchezo  huo. Lakini  amesema  pia  kwamba  kulikuwa  na sababu  maalum  kuchagua  mbinu ya  kuwa  na  walinzi  watatu  kwa mchezo  huo.

Bayern Munich  ilipata  ushindi  wa  kibarua  dhidi  ya  Mainz wa mabao 2-1  na  kuwa  nyuma  ya  Borussia  Dortmund  kwa  pointi mbili  tu ikiwa  na  pointi 19 ambapo BVB ina  pointi 21.

Schalke 04  imesogea  hadi  nafasi  ya  15 baada  ya  kutoka  sare ya  bila  kufungana  na  RB Leipzig jana  Jumapili  na Nuerenberg ilitoshana  nguvu  na  Eintracht  Frankfurt  kwa  kufungana  bao 1-1 pia  jana  Jumapili.

Kocha  wa  zamani  wa  timu  ya  taifa  ya  vijana  chini  ya  miaka 21  ya Ujerumani  Horst Hrubesch  amelikosoa  shirikisho  la  taifa  la kandanda  DFB  kwa  jinsi  ya  kuwapa  mafunzo  vijana  wenye vipaji, akisema  chama  hicho kiko  nyuma  ya  mataifa  mengine baada  ya  mafanikio  ya  hapo  awali. "Nimekuwa  nikisema  kwa miaka  mitano  kwamba  ni  lazima  tufanye  kitu," Hrubesch ameliambia  toleo  ya  Jumatatu  la   jarida  la  michezo  la  Kicker.

Horst Hrubesch
Horst Hrubesch kocha wa zamani wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21Picha: Imago/J. Huebner

"Tuko vizuri  hapa  DFB lakini  tunaweza  kufanya  vizuri  zaidi. Hilo linapaswa  kuwa  lengo  letu , kila  mara  tuko  nyuma  hatua  moja wakatu  tunapaswa  kuwa  hatua  tano  mbele. "Chombo  cha kutusafirisha  tumekikosa  lakini  tumejibweteka kwa  muda  mrefu baada  ya  kizazi  cha  kila  Jerome Boateng, Mats Hummels, Manuel Neuer  na  Mesut Oezil. Hrubesch mshambuliaji  wa  zamani  wa Hamburg na  mshindi wa  kombe  la  mataifa  ya  Ulaya  mwaka 1980 , aliwafunza  wachezaji  hawa  na  kupata  ubingwa  wa  vijana chini  ya  umri  wa  miaka  21  barani  Ulaya  mwaka  2009 na  kuleta mafanikio  makubwa  kwa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / dpae /  ape / afpe

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman