1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buriani rais wa pili wa Kenya Mzee Moi

Amina Mjahid
11 Februari 2020

Hayati rais Daniel Arap Moi atakumbukwa kwa kuchangia amani duniani na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki huku akiwa kielelezo cha uongozi kwa baadhi yao. Hayo yamesemwa na viongozi waliohudhuria ibada ya wafu Nairobi.

https://p.dw.com/p/3Xc1A
Kenia | Nyayo Stadium Nairobi | Requeim-Messe des ehemaligen Präsidenten Daniel Toroitich Arap Moi
Picha: DW/S. Wasilwa

Tofauti na miaka 18 iliyopita, alipokuwa akikabidhi mikoba ya uongozi kwa rais mstaafu Mwai Kibaki, ambapo wengi walikuwa wakiimba ‘yote yawezekana bila Moi', ibada ya mazishi yake, iliwaunganisha marafiki na maadui wa kiongozi huyo mwendazake.

Huku jeshi likiongoza hafla hiyo iliyodhuriwa na marais wa mataifa mbali mbali na zaidi ya wakenya elfu 30, uwanja wa Nyayo alioujenga katika utawala wake wa miaka 24, ulifurika waombolezaji. Rais Uhuru Kenyatta aliongoza hafla hiyo ya kitaifa iliyodumu kwa zaidi ya saa tano.

Katika utawala wake, Moi alialikwa kusaka amani katika mataifa ya Somalia, Chad, Uganda, Namibia, Msumbiji, Iran-Iraq, Kuwait, Yugoslavia, Liberia, Morocco, Angola, Serbia-Croatia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sierra Leone na Timor ya Mashariki.

Hata hivyo ni dhima yake ya kuleta utangamano kwenye mzozo wa Sudan uliokuwa umedumu kwa kipindi cha miaka 50 kati ya Kusini na Kaskazini ambao utakumbukwa.

Hata baada ya kuachia madaraka, rais Mstaafu Mwai Kibaki alimteua Moi mwaka 2007 kuwa balozi maalumu wa masuala ya Sudan kutokana na uwelewa wake mpana wa masuala ya Afrika kabla ya kuzaliwa kwa taifa hilo jipya kabisa ulimwenguni. Rais wa Uganda Yoweri Museveni pia alituma risala zake.

Mchango wa Moi kwa kuanzisha shirika la IGAD watambuliwa

Kenia 1992 | Daniel Arap Moi, ehemaliger Präsident
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Aidha mchango wake Moi wa kuanzisha Shirika la Maendeleo la IGAD linalohusika na amani na maendeleo ya kanda hii ulitambuliwa. Baadhi ya marais wengine waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Sahrawi- Brahim Ghali, Paul Kagame wa Rwanda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Sahle Work-Zewde wa Ethiopia, rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh miongoni mwa wengine.

Licha ya kuacha historia iliyoshiba sifa ndani na nje ya Kenya, mahasimu wa mzee Moi watamkumbuka kwa kubinya demokrasia pamoja na kuzima sauti ya upinzani miaka ya themanini na tisini kabla ya kubadilisha katiba na kuruhusu vyama vingi baadaye.

Mzee Moi alikuwa na wana wanane, watano wa kiume na binti watatu, mkewe aliaga dunia mwaka 2004.  Hayati Moi atazikwa kesho nyumbani kwake katika jimbo la Nakuru.

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi