1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yarejea kwa kishindo na mashabiki

21 Septemba 2020

Kurejea kwa mashabiki viwanjani katika mechi za ufunguzi wa msimu mpya wa kandanda Ujerumani ilikuwa ni habari njema kwa ligi na vilabu lakini itachukua muda kabla ya kushuhudia umati kamili Ujerumani

https://p.dw.com/p/3inUw
Fussball Bundesliga RB Leipzig vs. 1. FSV Mainz 05
Picha: Maja Hitij/Getty Images

Na kwa waliopata fursa ya kushabikia timu zao viwanjani, ilikuwa ni furaha kubwa kama anavyoeleza shabiki huyu wa Union Berlin ambao aliyeshuhudia timu yake ikikaangwa kwa mabao matatu kwa moja dhidi ya Ausgburg "Bila shaka inapendeza kwenda uwanjani tena na kuishangilia timu yako. Tatizo letu, ni kuwa mashabiki wengine wote watabaki nje na hawawezi kuingia. Bila shaka ni mazingira tofauti uwanjani. Mashabiki 5,000 au 22,000 huwa na mchango mkubwa. Kwa vyovyote vile ni hatua moja mbele na kitu kizuri." Soma pia: Bayern yaikaanga Schalke 8 - 0 katika ufunguzi wa msimu

Wakati wachezaji wa Chelsea Kai Havertz na Timo Werner walikuwa wanapambana na mabingwa watetezi wa Premier League Liverpool, RB Leipzig na Bayer Leverkusen walianza maisha katika Bundesliga bila nyota wao. Swali ni je, waliwakosa?

Fussball Bundesliga RB Leipzig vs. 1. FSV Mainz 05 | Emil Forsberg
Emil Fosberg alifurahia uwepo wa mashabiki dimbaniPicha: Picture Point LE/Imago Images

Nadhani kwa sasa bado ni mapema kujibu swali hilo. Lakini katika mechi ya jana, Leipzig haikuonekana kumkosa Werner, wakati ikiichabanga Mainz 3 - 1 ikiwa ni msimu wa pili chini ya kocha Julian Nagelsmann. Hadi mashabiki 8,500 waliruhusiwa na mamlaka za eneo hilo kuingia katika uwanja wa Leipzig. Emil Forsberg ni mmoja wa waliofunga mabao ya Leipzig "Nimejisikia vizuri kwa muda mrefu. Niko katika hali nzuri. Nataka tu kuisaidia timu. Nadhani tulicheza vizuri leo. Ilikuwa vyema kucheza tena mbele ya mashabiki, mashabiki wetu. Pia tulitaka kuwapa ushindi. Ilikuwa ni hisia nzuri mno kucheza tena mbele ya mashabiki"

Ikiwa Leverkusen itakuwa sawa bila Havertz huenda ni swala lenye wasiwasi mkubwa. Leverkusen ilitoka sare tasa dhidi ya Wolfsburg na hakika pengo la Havertz liliokena kwa sababu vijana hao wa kocha Peter Bosz waliyumba katika kufanya mashambulizi. Msikilize kocha Bosz "Hatudhani ingekuwa 0 - 0. Tulikuja hapa kushinda mchezo. Lakini kama umeuona mchezo, hakika utakubaliana kuwa matokeo ya sare yalistahili. Timu zote zilijaribu kushinda, zikashambulia na kupata nafasi moja au mbili za kufunga. Mwishowe ikawa tu sawa." Nani atamfunga paka kengele Bundesliga?

Bayern watuma ujumbe, Dortmund makidna wa Dortmund wavutia

Bayern huenda walituma ujumbe wa mapema wa kubeba taji la tisa mfululizo, lakini ushindi wa Dortmund wa 3 - 0 dhidi ya Borussia Moenchegladbach uliwaonyesha kuwa timu yenye kuvutia sana ya kutizamwa. Kinda Giovanni Reyna alifunga bao katika mechi yake ya kwanza ya ligi na mwenzake mwenye umri wa miaka 17 Jude Bellingham akatoa asisti yake ya kwanza. Erling Haaland mwenye umri wa miaka 20 alifunga mawili huku Jadon Sancho akitoa asisti.

Bundesliga - Borussia Dortmund vs. Borussia Moenchengladbach
Makinda wa Dortmund waliwasha moto Signal Iduna ParkPicha: Leon Kuegeler/Reuters

Bayern hawakuonekana kumkosa Thiago Alcantara ambaye alihamia Liverpool, maana waliinyeshea Schalke mvua ya magoli 8 - 0 licha ya kuwa mechi hiyo ilichezwa bila mashabiki baada ya mipango yao ya kuwa na mashabiki 7,500 kupingwa na mamlaka za Munich kutokana na kupanda maambukizi ya corona. Msikilize Serge Gnabry ambaye aliongoza mashabili ya Bayern pamoja na Leroy Sane "Najisikia vizuri kabisa, lakini muhimu zaidi ni kuwa tulipiga hatua ya kwanza kama timu, tulionyesha mchezo mzuri sana leo, kwamba hatukusita kuongeza kasi. Kwangu binafsi, bila shaka, ni kuwa nilifunga hat trick ya kwanza ya Bundesliga."

Kocha wa Schalke David Wagner hakuamini alichokiona uwanjani lakini akakiri kuwa wapinzani wao walikuwa moto wa kuotea mbali "likuwa mbaya sana. Hatukucheza vizuri. Bayern walikuwa katika hali nzuri sana. Tunapaswa kujinyanyua sasa, tukubali kipigo hiki cha uchungu na sasa ni juu yetu sisi  dhidi ya Werder Bremen kuonyesha mchezo tunaotarajia kutoka kwetu"