Brahimi asema mzozo wa Syria waweza kutapakaa | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Brahimi asema mzozo wa Syria waweza kutapakaa

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi ameonya kwamba mgogoro huo unaweza kuenea katika eneo zima iwapo hautasimamishwa. Ndani ya Syria mapigano makali yanaendelea

Mpatanishi wa kimataifa kuhusu Syria, Lakhdar Brahimi

Mpatanishi wa kimataifa kuhusu Syria, Lakhdar Brahimi

Akizungumza katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, mpatanishi huyo wa kimataifa katika mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi, amesema iwapo mgogoro wa Syria hautasimamishwa, hautabakia ndani ya mipaka ya Syria. Amesema mambo ni mawili; ama mgogoro huo utasimamishwa, au utatapakaa na kuliacha eneo zima likiwaka moto.

Muda mfupi baada ya Brahimi kutoa kauli hiyo, mapigano makali yalifanyika kwenye mpaka baina ya Syria na Lebanon. Afisa mmoja wa usalama wa Lebanon amesema kwamba watu wenye silaha ndani ya Lebanon wamefyatua risasi ndani ya Syria, na mashambulizi yao yalijibiwa hapo hapo na jeshi la Syria, ambalo lilirusha makombora ya vifaru kulenga maeneo ndani ya Lebanon.

Hatari ya mzozo kutapakaa

Lebanon ni nchi ya sita kutembelewa na Lakhdar Brahimi katika ziara ya mashariki ya kati

Lebanon ni nchi ya sita kutembelewa na Lakhdar Brahimi katika ziara ya mashariki ya kati

Lebanon ni nchi ya sita ambayo Brahimi ameitembelea katika ziara yake ya Mashariki ya Kati, ambayo inalenga kupata usitishwaji wa mapigano mnamo siku nne za sikukuu ya Idd al-Adha mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba. Kabla ya kuondoka Lebanon alikuwa na ujumbe mzito kwa nchi majirani wa Syria.

''Mnapaswa kuelewa kwamba mgogoro huu ukiendelea hautabakia ndani ya Syria milele. Wakati utafika ambapo utaenea katika eneo zima, na utakula majani mabichi na makavu katika eneo hili''. Alisema mpatanishi huyo.

Tangu kuripuka kwa mgogoro huu ulioanza kama vuguvugu la maandamano dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad, kumekuwepo na mapigano kadhaa yanayovuka mpaka wa Syria. Lebanon imekwishailalamikia mara mbili serikali ya mjini Damascus juu ya kushambuliwa kwa maeneo yake, huku Syria ikiishutumu Lebanon kuruhusu silaha na wapiganaji kupita kwenye lake, kwenda kuunga mkono waasi.

Kwa upande wa kaskazini, makombora yanayovuka mpaka wa Syria na kuingia Uturuki yamezusha mvutano mkubwa baina ya nchi hizo mbili. Jana, kombora jingine lilitoka ndani ya Syria lilianguka nchini Uturuki bila kusababisha madhara yoyote, na Uturuki, kama ambavyo imekuwa ikifanya siku za hivi karibuni, ilijibu kwa kuvurumusha makombora ndani ya Syria.

Ahueni ya Idd el-Adha

Wakati Brahimi akitaka ahueni, mapambano nchini Syria yameendelea

Wakati Brahimi akitaka ahueni, mapambano nchini Syria yameendelea

Pendekezo la Lakhdar Brahimi la kuwepo kwa siku nne za ahueni wakati wa sikukuu ya Idd al-Adha limeungwa mkono na Uturuki, Irak na Iran. Brahimi anasema ikiwa pendekezo lake litafanikiwa, itakuwa hatua ndogo mbele.

Brahimi alisema,''Kila upande nchini Syria unazika watu zaidi ya 100 kila siku. Je si tunaweza tukataka iwepo ahueni wakati wa sikukuu? Hii haitakuwa sikukuu njema kwa wasyria, lakini angalau tunaweza kuwapunguzia shari.''

Serikali ya Syria imesema iko tayari kulizungumzia pendekezo la Brahimi, na Baraza la Kitaifa la upinzani nchini Syria limesema litasitisha mapigano, lakini, ikiwa serikali itachukua hatua hiyo kwanza.

Taarifa za hivi karibuni zimeeleza kwamba Lakhdar Brahimi atawasili mjini Damascus Jumamosi ijayo, na atafanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid Muallem.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com