1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bodo/Glimt yaiondoa Inter kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya

25 Februari 2026

Klabu ya Bodo/Glimt ya Norway imeandika moja ya matokeo ya kushangaza katika historia ya kisasa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne usiku, kwa kuwapiga Inter Milan ambao walicheza fainali ya msimu uliopita.

https://p.dw.com/p/59LtR
Mchuano kati ya Inter Mailand vs. Bodø/Glimt katika dimba la San Siro
Klabu ya Bodo/Glimt ya Norway imeandika historia kwa kuwaondoa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Inter MilanPicha: Marius Simensen/Bildbyran/IMAGO

Bodo/Glimt waliwafunga mabao 2 - 1 katika dimba la San Siro na kutinga hatua ya 16 bora kwa jumla ya magoli 5 - 2 baada ya mikondo miwili ya mechi yao ya mchujo. Timu hiyo iliingia dimbani ikilenga kuendeleza kwenye ushindi wao wa 3 - 1 katika mkondo wa kwanza nchini Norway. Inter, mabingwa mara tatu wa Ulaya na ambao wanaongoza msimamo wa ligi kuu ya Italia - Serie A na pengo la pointi 10, walitarajiwa kuwagaragaza wageni wao katika jaribio la kuyapindua matokeo. Lakini Bodo/Glimt walihimili kishindo katika kipindi cha kwanza kabla ya kumaliza kazi katika kipindi cha pili cha mchezo. Watawafahamu wapinzani wao wa hatua ya 16 bora Ijumaa lakini tayari wanajua itakuwa Sporting ya Ureno au Manchester City -- ambayo waliishinda 3-1 nyumbani mwezi uliopita katika awamu ya ligi.

Newcastle United waliendeleza ushindi wao wa 6 - 1 ugenini dhidi ya Qarabag nchini Azerbaijan katika mkondo wa kwanza wiki iliyopita, kwa kupata ushindi wa 3 - 2 kwenye mkondo wa marudiano dimbani St James' Park. Vijana hao wa kocha Eddie Howe walihakikisha kuwa kuna vilabu sita vya England katika duru inayofuata. Newcastle sasa inaweza kutarajia mechi kali katika raundi inayofuata dhidi ya Chelsea au Barcelona.

Atletico walikuwa wamelazimishwa sare ya 3-3 na Club Brugge nchini Ubelgiji wiki iliyopita lakini walishinda 4-1 katika mechi ya marudiano Jumanne katika mji mkuu wa Uhispania na kusonga mbele kwa jumla ya 7-4. Timu hiyo ya kocha Diego Simeone itacheza na Tottenham Hotspur au Liverpool katika raundi inayofuata.

Wakati huo huo, Bayer Leverkusen ilitoka sare tasa nyumbani dhidi ya Olympiacos baada ya ushindi wa 2 - 0 ugenini Ugiriki wili iliyopita. Mabingwa hao wa Ujerumani 2024 sasa watakuwa na mtihani mkubwa dhidi ya ama Arsenal au watani wao wa Bundesliga Bayern Munich.