1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden azidi kujizatiti kuelekea uteuzi wa Democratic

Sylvia Mwehozi
11 Machi 2020

Aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani Joe Biden amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mchujo ndani ya chama cha Democratic, katika jimbo la Michigan na mengine matatu wakati Sanders akishinda North Dakota.

https://p.dw.com/p/3ZDr1
US-Präsidentschaftskandidat Biden im Gespräch mit Arbeitern in einem Werk in Detroit
Picha: Reuters/B. McDermid

Ushindi wa Biden kwenye kura za mchujo zilizofanyika siku ya Jumanne zinamuweka hatua moja mbele kuelekea uteuzi wa kugombea urais kupitia chama cha Democratic, akipambana na Donald Trump katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Muda mchache baada ya kujizolea ushindi huo Biden ametoa wito wa mshikamano ndani ya chama chake na wafuasi wa mshindani wake mkuu, Seneta Bernie Sanders. Akizungumza mjini Philadelphia baada ya ushindi huo, Biden amemshukuru Sanders na wafuasi wake, akisema sasa ni wakati wa kushikamana ili kumng'oa Donald Trump kwenye uchaguzi wa Novemba 3 mwaka huu.

"Lakini kushinda kunamaanisha kuiunganisha Marekani, sio kuongeza mgawanyiko zaidi na hasira. Inamaanisha kuwa na rais ambaye si tu anajua kupigana lakini pia kuponya. Inamaanisha kumbadilisha rais mwenye kudharau na kuwafanya watu kuwa duni na rais ambaye ana huruma na kuheshimu kila mtu", alisema Biden.

Ushindi wa Biden kwenye majimbo ya Idaho, Michigan, Missouri na Mississipi, umechangiwa kwa kiasi kikubwa na makundi ya wanawake, Wamarekani wenye asili ya Afrika, wapigakura wenye umri mkubwa na vyama vya wafanyakazi. Sanders kwa upande wake ambaye ana umri wa miaka 78 ameshinda jimbo la North Dakota.

Präsidentschaftskandidat Bernie Sanders in Dearborn Heights, Michigan
Bernie Sanders mgombea anayewania kuteuliwa na DemocraticPicha: Reuters/L. Jackson

Mara baada ya ushindi huo, Sanders alirejea nyumbani kwake Vermont usiku wa Jumanne, na hakutoa kauli yoyote kuhusu matokeo hyo yanayozidi kuififisha nafasi yake. Wapiga kura kwenye majimbo hayo walisema wanamuamini zaidi Biden katika kushughulikia migogoro mikubwa, kulingana na utafiti uliofanywa. Wagombea wote wamesitisha mikutano iliyokuwa imepangwa kufanyika usiku wa Jumanne, katika kukabiliana na janga la mripuko wa virusi vya Corona.

Michigan lilikuwa ndio jimbo kubwa na la ushindani zaidi miongoni mwa majimbo sita kwenye uchaguzi wa Jumanne. Ushindi wa Biden unaweza kuwa ni pigo kwa Sanders hususan sasa uchaguzi huo unapoelekea kwenye majimbo makubwa likiwemo Florida, Ohio na Georgia, ambako Biden anaonekana wazi kuwa mtu anayependwa. Hadi kufikia Jumatano Biden ameshinda wajumbe 153 dhidi ya 100 wa Sanders na kumpatia ushindi jumla katika kinyang'anyiro cha wajumbe 1,991 wanaohitajika kwa ajili ya utuezi.

Licha ya kwamba bado haijakuwa wazi endapo Biden mwenye umri wa miaka 77 ataongoza hadi mwishoni, lakini kampeni ya Seneta Sanders inaonekana kurudi nyuma kwa kasi, baada ya ushindi wake wa awali.

Vyanzo: AP/AFP