1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Beckenbauer: Mechi ya Bayern na Dortmund itaamua ubingwa

Bruce Amani
5 Machi 2019

Rais wa Bayern Munich Franz Beckenbauer anaamini kuwa taji la msimu huu la Bundesliga litaamuliwa katika mtanange wa nyumbani wa mabingwa hao dhidi ya vinara wa sasa Borussia Dortmund

https://p.dw.com/p/3EU1I
Franz Beckenbauer
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Rose

Dortmund inaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya mabao baada ya Bayern kupambana na kuziba kabisa mwanya wa pointi tisa uliokuwepo katika wiki za karibuni. Beckenbauer anaamini kuwa kutetea ubingwa wa Bundesliga msimu huu yatakuwa mafanikio makubwa kuliko kushinda Ligi ya Mabingwa kwa Bayern.

"Ubingwa wa Bundesliga kwa maoni yangu utaamuliwa Aprili 6 katika mpambano wa moja kwa moja dhidi ya Dortmund na kwangu mimi ndio taji lenye thamani Zaidi,” Beckenbauer mwenye umri wa miaka 73 ameliambia gazeti la Bild.

Kuna mechi 10 zilizosalia katika Bundesliga. Bayern watawaalika Liverpool wiki ijayo katika mechi yao ya mkondo wa pili wa hatua ya 16 za mwisho ya Champions League huku matokeo yakiwa 0 – 0 kutokana na mkondo wa kwanza.

Gnabry aurefusha mkataba wake na Bayern

Bundesliga - Borussia Moenchengladbach gegen Bayern München Tor zum 1:4
Gnabry amesaini mkataba hadi 2023Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Winga wa Ujerumani Serge Gnabry ameurefusha mkataba wake na klabu ya Bayern Munich hadi 2023, kwa kuongeza miaka mitatu zaidi kwenye mkataba wake. Mabingwa hao watetezi wanaendelea kukiimarisha kikosi chake.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 anaandaliwa kuchukua nafasi ya mawinga wakongwe wa Bayern Arjen Robben na Franck Ribery, ambao wote wana umri wa miaka 35 na mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu.

Gnabry, chipukizi wa Canada Alphonso Davies mwenye umri wa miaka 18, na Mfaransa Kingsley Coman, mwenye umri wa miaka 22 ndio kizazi kijacho cha mawinga wa Bayern.

Bayern walilpa Werder Bremen euro milioni nane kumnunua Gnabry mzaliwa wa Stuttgart mnamo mwaka wa 2017, lakini wakampeleka Hoffenheim kwa mkopo msimu uliopita, kwa hiyo huu ni mwaka wake wa kwanza katika Bayern. Ameifungia Bayern mabao nane katika mechi 29.