1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yarejea kwa kishindo kileleni katika Bundesliga

Sekione Kitojo
18 Machi 2019

Bayern Munich yafanya  kweli katika  mbio za  kuwania  ubingwa wake wa saba  mfululizo katika  Bundesliga,yairarua Mainz na kurejea kileleni kwa wingi wa magoli dhidi ya BVB

https://p.dw.com/p/3FGH5
Fußball Bundesliga FC Bayern München - Mainz 05
Picha: Reuters/M. Dalder

Tukianza  na  Bundesliga  Bayern Munich  imeelekeza  hasira yake ya  kuondolewa  katika  kinyang'anyiro  cha ligi ya  mabingwa  barani Ulaya  Champions League , na  FC Liverpool  katikati  mwa  wiki kwa  kuikandika  Mainz 05  kwa  mabao  6-0  wakati James Rodriguez  akisajili seti  yake  ya  kwanza  ya  mabao  matatu  katika Bundesliga  jana  Jumapili na  kukiweka  kikosi  hicho  cha  kocha Niko Kovac  kurejea  kileleni  mwa  msimamo  wa  ligi.

Fußball Bundesliga FC Bayern München - Mainz 05
James Rodriguez, akiwasubiri wachezaji wenzake Leon Goretzka (kushoto) na Kingsley Coman, (Kulia) wakishangiria baoPicha: Reuters/M. Dalder

Baada  ya  kukandikwa  mabao 3-1  na  Liverpool  katikati  ya  wiki katika  mchezo  wa  Champions League  katika  timu  16  bora , Mainz  ilikiona  kilichomtoa  kanga  manyoya  katika  uwanja  wa Allianz Arena  mjini  Munich.

"Tulionesha  kwamba  fadhaa  iliyotupata  kutokana  na  kipigo dhidi ya  Liverpool tumekwisha  sahau, ilikuwa  muhimu  kuchukua  hatua;" alisema  kocha  wa  Bayern Niko  Kovac.

Bayern  na  Dortmund ziko  sawa  katika  pointi 60 kila  mmoja, lakini kikosi  hicho  kutoka  jimbo  la  Bavaria  kinatofautiana  na  Dortmund kwa  wingi  wa  magoli. Dortmund  iliichapa  Hertha  Berlin siku  ya Jumamosi  kwa  mabao 3-2  na  kuchukua  uongozi wa  ligi  kwa masaa  kabla  ya  Bayern  kurejea  kileleni  jana. Huyu  hapa nahodha  wa  Dortmund Marco Reus.

Fußball Bundesliga Hertha BSC- Borussia Dortmund
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakishangiria bao lililofungwa na Thomas DelaneyPicha: Getty Images/Bongarts/M. Rose

"Kila mmoja  anafahamu  tunavyoelewana, lakini  haikuonekana kuwa  itakuwa  hivyo leo hadi katika  dakika ya 92. Hatukuweza kuonana. Lakini  tuliendelea  kujiamini na  hatimaye  alinipatia pasi sahihi na niliusukuma tu wavuni".

Tulitaka  kupambana  na  kurejea  baada  ya  ushindi  wa  Dortmund. Michezo  mitatu  iliyopita  ilikuwa ni  alama," mshambuliaji  wa Bayern Thomas Mueller  amesema , baada  ya  Bayern  kutupia nyavuni  mabao 17 katika  michezo  yake  mitatu  iliyopita.

Frankfurt haijafungwa

Hapo  mapema  Eintracht  Frankfurt, klabu  pekee  katika  Bundesliga ambayo  imebakia  katika  vikombe  vya  Ulaya , iliendelea  kuwania kupata  nafasi  ya  kucheza  katika  Champions League  msimu  ujao , kwa  ushindi  wa  bao 1-0  dhidi  ya  Nuremberg.

Frankfurt  haijafungwa  katika  michezo  yake 13 iliyopita, ikiwa  ni pamoja  na  tisa  katika  Bundesliga.

Hapo mapema  Werder  Bremen  iliionyesha cha  mtema  kuni Leverkusen  kwa  kuishindilia  mabao 3-1. Leverkusen  inabakia katika  nafasi  ya 6 ikiwa  na  pointi 42 ikipitwa  na  Frankfurt ambayo  iko  katika  nafasi  ya  5  ikiwa  na  pointi 46.

Fußball Bundesliga Werder Bremen Bayer Leverkusen
Wachezaji wa Werder Bremen wakishangiria bao dhidi ya LeverkusenPicha: imago/DeFodi

Schalke 04  baada  ya  kutengana  na  kocha  wake Domenico Tedesco katikati  ya  wiki  baada  ya  kubugizwa  mabao 7-0 katika Champions League  na Manchester  City ilimrejesha  kocha  wake wa  zamani  Hubb Stevens. Kocha  huyo  ambaye  alipata  mafanikio makubwa  na  Schalke 04  ikiwa  ni  pamoja  na  kutwaa  kombe  la washindi  barani  Ulaya 1997, hakuweza  kuzuwia  kuporomoka  kwa Schalke siku  ya  Jumamosi  baada  ya  kuchapwa kwa  bao 1-0 dhidi  ya  RB Leipzig.

Schalke imeporomoka  kutoka  nafasi  ya  13  na  sasa  inaelea katika  nafasi  ya 15 , ikiwa  na  pointi 3  tu  zaidi  ya  timu iliyoko katika  nafasi  ya  kushuka  daraja VFL Stuttgart ambayo  ilitoka sare  ya  bao 1-1 na  Hoffenheim siku  ya  Jumamosi na  kufikisha pointi 20.

Ligi ya Bundesliga  na  nyingine zote  za Ulaya zinasimama kwa wiki mbili kupisha  michuano  ya  kuwania  kufuzu kucheza katika  kombe la  mataifa  ya  Ulaya.

UEFA Nations League - Mats Hummels, Thomas Mueller und Jerome Boateng
Wachezaji Mats Hummels, (kushoto), Thomas Mueller(katikati) na Joreme Boateng ambao wameenguliwa kutoka kikosi cha Die MannschaftPicha: Imago/DeFodi/T. Hiermayer

Ujerumani  inapambana  na  Serbia  katika mchezo  wa  kirafiki  siku  ya  Jumatano  ikiwa  ni katika mchezo  wa kwanza  mwaka  huu  na  kocha  Joachim Loew analazimika  kupata matokeo  mazuri baada  ya  uamuzi  wake uliokosolewa  kwa  kiasi kikubwa  hapa  Ujerumani  baada  ya  kuwaondoa  kikosini wachezaji  wakongwe Mats Hummels, Jerome Boateng  na  Thomas Mueller  kutoka  Bayern Munich  na  kuteua  makinda  katika  kikosi chake.Anapaswa  hivi  sasa kuthibitisha  kuwa  ni mtu sahihi  kwa timu  hiyo  baada  ya  miaka  13 akiwa  kocha  wa  Ujerumani.