1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yapata uhakika kunyakua ngao ya ubingwa mara ya nane

Sekione Kitojo
8 Juni 2020

Ni  wale  wale  tunaowafahamu  wakiwa  kileleni  tena katika msimamo  wa  ligi  ya Bundesliga, FC Bayern Munich. Ina  pointi saba  mbele  ya  Borussia  Dortmund iliyoko  katika  nafsi  ya  pili.

https://p.dw.com/p/3dSIb
Bayer Leverkusen - FC Bayern München | Jubel Goretzka
Wachezaji Leon Goretzka , Serge Nabry na Joshua Kimmich wakikusanyika kushangiria bao la timu yao ya Bayern Munich Picha: Reuters/M. Hangst

Ikiwa  ni  michezo minne tu imebakia  kabla ya kumalizika  kwa  ligi, na  na  ni  dhahiri  pengo  hili haliwezi  kuponyoka  mkononi.  Hii ilionekana  wazi  tangu  ushindi  wa  Bayern  katika  mpambano  wa vigogo  BVB dhidi  ya  Bayern karibu  wiki  mbili  zilizopita. Mchezo huo ulileta matumaini kwa wapinzani wa Bayern kwamba  huenda ikapoteza  pointi  na  kufanya mbio za kuelekea  ubingwa  kuwa za mvutano. Matumaini  haya  yaliporomoka. Hata Bayer Leverkusen , ambao  siku  ya  Jumamosi walianza kwa  kushambulia  sana  lakini wakiwa  wanafanya  makosa  kadhaa  na  upande  wa  ulinzi  kukiwa wazi  mno, hawakuweza  kuwa  kizingiti kwa  Bayern. Bayern ilishinda  kwa  kishindo mabao 4-2.

Fußball Hansi Flick
Kocha wa Bayern Munich Hans FlickPicha: picture-alliance/SvenSimon/F. Hoermann

Huyu  hapa  kocha  wa  Bayern Hans Flick.

"Katika  soka  suala  muhimu  ni  kwamba lazima ushinde mchezo. Hicho  ndicho tulichokionesha  katika  mwaka huu 2020. Timu hailegezi  kamba. Leo  pia  imerudi katika  hali ya kawaida  baada ya mwanzo wenye matatizo, ambapo Leverkusen  walitangulia  kwa bao 1-0. Kama  ilivyokuwa  katika  kipindi  cha  kwanza, tulionesha uwezo  wetu, katika  kipindi  cha  pili, lakini  pia mpangilio na dhamira. Kwa hilo nimefarijika sana. Kwetu sisi kitu cha  kwanza  ni  kwamba tunataka  ubingwa. Kuna michezo minne iliyobaki. Hilo ndio lengo letu, na chochote kingine hakina maana."

Na  hata  katika  msimu  ujao kuna matumaini  yasiyo  na  mipaka, kuhusiana  na  ubingwa  wa  tisa wa  Bayern mfululizo. Bayern imejiimarisha kwa  kumpatia  mkataba  wa  kudumu  kocha  Hans Flick, pamoja  na  mlinda  mlango  mahiri Manuel Neuer, mshambuliaji Thomas Mueller na  Alphonso Davies. Na Robert  Lewandowski  kila mmoja  anafahamu  kuwa  ni  mshambuliaji  bora  kabisa  wa Bundesliga na  pia  mshambuliaji  anayetarajiwa  kujiunga  na mabingwa  hao  kutoka  Manchester City Leroy Sane. Kwa  kikosi hicho, kuna  uwezekano  ubingwa  ukawa mali  ya  Bayern kwa muda  mrefu  katika  Bundesliga.

Manuel Neuer - Torwart
Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel NeuerPicha: Imago/F. Hoermann

Pamoja  na  hayo  katika  Bundesliga  Wolfsburg imepanda, Bremen imeporomoka , Schalke  inazidi  kudidimia.  Katika  michezo  ya mwishoni  mwa juma  jana  Jumapili . Bao  la  dakika  za  mwisho kwa  kichwa  la  Wout Weghorst liliipa  Wolfsburg  ushindi  wa  bao 1-0 dhidi  ya  Werder  Bremen  na  kuimarisha  nafasi  yake  ya kucheza  katika  kikombe  cha  ligi ya Ulaya  na  kupandikiza  mbinyo mkubwa  dhidi  ya  wenyeji  Bremen  ambao wana  hofu  ya kutumbukia  katika  daraja  la  pili.

Kocha  wa  Werder Bremen Florian Kohfeldt  hajakata tamaa:

"Kwa mara  nyingine  tena  tumetoka  patupu. Inakera sana, kwa msingi  wa  matokeo  ya jana. Tunapaswa  kujinyanyua na kujifuta baada  ya kuanguka, na  kisha katika  michezo minne  iliyobakia kujaribu  kila  tulichonacho, ili tufikie  katika  nafasi  ya  mchujo. Kuhusu hilo bado  nina matumaini, kwasababu naamini, timu leo haijacheza kama maiti, tulishuhudia  timu, ikipambana, ikijituma, na wachezaji kukimbia  kila  mahali, hadi  dakika  ya  mwisho, tulipobaini kwamba  haiwezekani tena. lakini sifikiri kwamba itatokea  tena."

Deutschland Bundesliga - Werder Bremen v VfL Wolfsburg
Kocha wa Werder Bremen Florian KohfeldtPicha: picture-alliance/Witters/gumzmedia/nordphoto

Bremen kwa sasa  iko  nafasi  ya  17  ikiwa  na  pointi 25, pointi 3 nyuma ya  Dusseldorf  iliyoko  katika  nafasi  ya  16 ya mchujo.

Union Berlin iliyopanda  daraja  msimu  huu  imesogea  karibu na eneo  la  usalama  katika  msimamo  wa  ligi katika  msimu  wake  wa kwanza  wa  Bundesliga kwa  kupata  sare  ya  bao 1-1  nyumbani dhidi  ya  Schalke 04, ambayo  sasa  imefikia  rekodi  yake  ya ndani  ya  michezo 12 bila  ushindi. Kwanini  Schalke  imerejea baada  ya  mapumziko  ya  corona  katika  hali  dhaifu  huyu  hapa kocha  wa  Schalke David Wagner:

"Unapokuwa  uko  nyuma kwa kufungwa  bao, kwa mara  nyingine tena  kutokana  na  makosa  makubwa ya  mchezaji, na kisha ukapambana  katika  mchezo  kama  huo  na  kusawazisha,  katika kipindi  kigumu  kabisa, kama  tulichomo kwa sasa, unaweza kimsingi  kufanya  subira tu, kwamba  vijana waweze kujiamini na kupambana. Na  nafikiri , hicho  ndio walichofanya. Wamejaribu. Niseme wazi  hata  hivyo , kwamba katika  hali ya sasa  ukomo wetu unaonekana  katika  kucheza  kandanda."

DFB Pokal | Schalke 04 vs FC Bayern München | David Wagner
Kocha wa Schalke 04 David WagnerPicha: AFP/S. Schürmann

Augsburg ilitoka  sare  ya  bao 1-1  dhidi  ya  FC Koeln . Borussia Dortmund  ilipata ushindi  mwingine siku  ya  Jumamosi nyumbani kwa  kuishinda  Hertha  BSC Berlin kwa bao 1-0 na  kujiimarisha katika  nafasi  yake  ya  pili. RB Leipzig  ilishindwa kutamba  mbele ya SC Paderborn nyumbani  kwa  kutoka  sare ya bao 1-1 na Dusseldorf  na  TSG Hoffenheim zilitoshana  nguvu  kwa  kufungana mabao 2-2.

Timu nne  zaidi  za  Bundesliga zilipiga  goti kabla  ya  michezo  yao jana  Jumapili. Borussia  Dortmund  na  Hertha  Berlin zilipiga  goti kwanza  kabla  ya  mchezo  wao  siku  ya  Jumamosi  katika ishara ya  kupinga  ubaguzi  kufuatia  maandamno  dhidi  ya  ukatili  wa polisi  na  ubaguzi nchini  Marekani kuhusiana  na  mauaji  dhidi  ya George Floyd mjini Minneapolis siku  ya  Mei 25.

Wolfsburg  na  Werder Bremen  walifuatia , Union Berlin  na Schalke, nazo zikafuatia.