Bayern na Dortmund zatoshana nguvu | Michezo | DW | 07.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern na Dortmund zatoshana nguvu

Bayern Munich , mabingwa wa Ligi ya Ujerumani, Bundesliga msimu huu, na timu iliyoko katika nafasi ya pili , mabingwa wa zamani Borussia Dortmund wametoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya ligi

DORTMUND, GERMANY - MAY 04: Nuri Sahin of Dortmund shoots a free-kick over the wall of Bayern during the Bundesliga match between Borussia Dortmund and FC Bayern Muenchen at Signal Iduna Park on May 4, 2013 in Dortmund, Germany. (Photo by Christof Koepsel/Bongarts/Getty Images)

Fußball Bundesliga 32. Spieltag Borussia Dortmund FC Bayern München Rote Karte

Mchuano huo wa Jumamosi ulichezwa wakati zikiwa zimesalia wiki tatu kabla ya mpambano wao wa fainali ya Champions League katika uwanja wa Wembley mjini London. Wakati timu hizo zikiwa suluhu ya bao 1-1, Borussia walipata mkwaju wa Penalti ambao mlinda mlango wa Bayern Manuel Neuer alifanikiwa kuokoa mkwaju wa Robert Lewandowski katika kipindi cha pili na mlinzi wa kulia wa kikosi hicho cha kocha Jupp Heynckes Rafinha alitolewa nje kwa kadi nyekundu muda mfupi baadaye wakati Bayern wanaendelea kuongoza ligi hiyo kwa points 20 zaidi ya timu inayofuata Borussia Dortmund.

Mchezo ulijaa hisia kali wakati mchezaji wa Bayern Rafinha akioneshwa kadi nyekundu

Mchezo ulijaa hisia kali wakati mchezaji wa Bayern Rafinha akioneshwa kadi nyekundu

Dortmund tayari imefanikiwa kucheza katika awamu ya makundi ya Champions League mwakani, na Bayer Leverkusen ikijiunga nao pia baada ya kujihakikishia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nuremberg.

Nilizungumza na mchambuzi wa masuala ya soka na mhariri wa zamani wa michezo idhaa ya Kiswahili ya DW , Ramadhan Ali, tulizungumzia mengi kuhusu Bundesliga lakini pia nilitaka kujua iwapo mchezo kati ya Borussia Dortmund dhidi ya Bayern hapo Jumamosi unaakisi kile kitakachotokea hapo tarehe 25 siku ya fainali ya Champions League uwanjani Wembley.

Chelsea kukuana na Spurs

Katika Premier League Chelsea iliikaba koo Manchester United kwa kuipa kipigo cha bao 1-0 nyumbani wakati Huan Mata alipoihakikishia timu yake ushindi katika dakika ya 87 ya mchezo huo. Mlinzi wa Manchester Rafael alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumpiga ngware mchezaji mwenzake wa Brazil David Luiz na matokeo hayo yamekiweka kikosi hicho kilichoingia katika fainali ya kombe la ligi ya Europa katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na points 68 kutokana na michezo 35.

Chelsea watalenga kuwashinda Tottenham Hotspurs na kutwaa nafasi ya tatu kwenye Premier Legaue, England

Chelsea watalenga kuwashinda Tottenham Hotspurs na kutwaa nafasi ya tatu kwenye Premier Legaue, England

Arsenal London ambayo iliiangusha QPR kwa bao 1-0, wako katika nafasi ya nne, point moja nyuma ya Chelsea lakini kikosi cha mzee Wenger kimecheza mchezo mmoja zaidi. Tottenham Hot Spurs wako katika nafasi ya 5 wakiwa na points 65.

Mlinzi Tiago Silva wa Paris St. Germain alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika sare iliyoifadhaisha timu hiyo ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Valenciennes hali ambayo imepunguza kasi ya mbio zao kuelekea kupata ubingwa wa kwanza wa ligi ya Ufaransa tangu mwaka 1994. PSG ina points 74, saba zaidi ya Olympique Marseille timu ambayo iliangusha Bastia kwa mabao 2-1. Juventus Turis imenyakua ubingwa wake wa pili mfululizo katika ligi ya Italia Serie A wakati ikisalia michezo mitatu baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Palermo.

Messi atamba Barca

Huko Uhispania ; Lionel Messi akitokea benchi alipachika mabao 2 na kuhakikisha ushindi wa mabao 4-2 kwa Barcelona dhidi ya Real Betis na kuiweka timu hiyo katika nafasi ya kulinyakua taji la ubingwa wa ligi ya Uhispania msimu huu.

Zikiwa zimesalia mechi 4 kumalizika msimu huu ulioshuhudia misuko suko mingi kwa Barcelona, timu hiyo ina point 11 zaidi ya Real Madrid, ambao nao waliiangusha Real Valladolid kwa mabao 4-3 nyumbani. Barca inaweza kutawazwa mabingwa wa La Liga mara ya nne katika kipindi cha miaka mitano siku ya Jumatano iwapo Real Madrid itashindwa kuipa kibano Malaga katika uwanja wake wa Bernabeu.

Lionel Messi amethibitisha tena kuwa ni nguzo muhimu ya Barcelona kwa kuingia na kufunga magoli mawili

Lionel Messi amethibitisha tena kuwa ni nguzo muhimu ya Barcelona kwa kuingia na kufunga magoli mawili

Ajax Amsterdam imenyakua ubingwa wake wa tatu mfululizo ikiwa umebakia mchezo mmoja kumalizika msimu huu wa ligi baada ya kuicharaza Willem 11 Tilburg kwa mabao 5-0 jana Jumapili.

CECAFA kuandaliwa Darfur na Kordofan

Majimbo mawili yanayokabiliwa na vita ya Darfur na Kordofan kusini nchini Sudan ndiko kutakakofanyika mashindano ya vilabu vya Afrika mashariki na kati , CECAFA mwezi ujao. Nilizungumza na katibu mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye ambaye amesema kuwa majimbo hayo yana nia ya kufanikisha michezo hiyo. Nilitaka kujua pia iwapo suala la usalama lilitiliwa maanani katika maamuzi hayo.

Timu 16 zimefanikiwa kuingia katika michuano ya makundi katika kombe la shirikisho barani Africa, CAF Confederation Cup . Timu hizo ni washindi ENPPI na Ismailia zote za Misri, Etoile Sahel na CS Sfaxien zote za Tunisia, Lydia Academic ya Burundi, US Bitam ya Gabon, Liga Muculmana ya Msumbiji na FAR Rabat ya Morocco. Timu zilizoshuka kutoka Champions League baada ya awamu ya timu 16, ni pamoja na JSM Bejaia, Entente Setif za Algeria, CA Bezertin ya Tunisia, Enugu Rangers ya Nigeria , Saint George ya Ethiopia, Stade Malien ya Mali, TP Mazembe ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, na FUS Rabat ya Morocco. Timu hizo zitapangwa katika makundi Mei 14 mjini Cairo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / reuters /

Mhariri:Yusuf Saumu