Bayern Munich wateteleka | Michezo | DW | 26.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern Munich wateteleka

Bayern Munich waliteteleka kidogo katika harakati zao za kulinyakua kwa mara nyengine taji la Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga baada ya kuzuiwa sare ya kutofungana na Hertha Berlin.

Mechi hiyo ilichezwa Jumamosi katika uwanja wao wa nyumbani Allianz Arena.

Msimu huu karibu kila kitu kimekuwa kikiwaendea vizuri Bayern kwa kuwa waliingia katika mechi hiyo na Hertha baada ya kuwacharaza Besiktas wa Uturuki magoli matano mnamo katikati ya wiki katika ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya, lakini Hertha ambao hawajashinda huko Munich katika Bundesliga hawakukubali rahisi ingawa Bayern walipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga katika mtanange huo.

Ushindi dhidi ya Hertha wanaotoka Mji Mkuu Berlin ungekuwa ni wa 15 mfululizo kwa Bayern Munich na wangekuwa wameivunja rekodi ya kocha Pal Csernai aliyeiweka na kikosi chake mwaka 1980.

"Haikuwa mechi rahisi, Hertha Berlin wamecheza vizuri sana, wamekuwa na nidhamu na wakajilinda vizuri sana," alisema Hummels. "Hatukuweza kupata nafasi nyingi za kucheza mchezo wetu. Tulikuwa tunajaribu mara kwa mara lakini hakuna nafasi ya wazi iliyojitokeza."

Frankfurt walitandikwa 1-0

SV Hamburg wako katika hatari kubwa ya kushushwa daraja kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya klabu hiyo baada ya kubwagwa moja bila walipokuwa wakipambana na Werder Bremen ugenini. Bremen walipata goli lao dakika nne kabla mechi kwisha baada ya Rick van Drongelen kufunga katika lango lake na kuwafanya kupata afueni katika harakati zao za kuzuia kushushwa daraja ingawa wamewazidi Mainz kwa pointi mbili tu na tisa mbele ya Hamburg.

Fußball | 1. Bundesliga 24. Spieltag | VfB Stuttgart - Eintracht Frankfurt (Getty Images/AFP/T. Kienzle)

Beki wa Eintracht Frankfurt Marco Russ akiwania mpira kwa kichwa

Eintracht Frankfurt walizabwa moja bila na Borussia Moenchengladbach kisha TSG Hoffenheim walikuwa nyumbani Rhein Neckar Arena ila walishindwa kupata alama tatu walipowakaribisha SC Freiburg kwani walitoka sare ya bao moja. Hoffenheim ndio waliotangulia kufunga katika kipindi cha pili kupitia frikiki iliyopigwa na mshambuliaji wao Andrej Kramaric ila Freiburg walisawazisha zilipotimu dakika sitini na sita ambapo nahodha Nils Pietersen aliposawazisha kupitia mkwaju wa penalti. Ni mechi tuliyoitangaza moja kwa moja hapa DW na hivi ndivyo mambo yaliyvokuwa.

Jumapili RB Leipzig walikosa nafasi ya kusonga hadi kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Bundesliga waliposhangazwa na FC Cologne kwa kufungwa mbili moja uwanjani kwao Red Bull Arena. Leipzig walionekana kana kwamba wanaelekea kupata ushindi mwembamba baada ya kuingia uongozini mwa mechi hiyo mapema katika dakika ya tano kupitia kwa goli la Jean-Kevin Augustine lakini Cologne walijizatiti na kucheka na wavu katika dakika ya 70 na 77 kupitia kwa Vincent Koziello na Leonardo Bittencourt.

Schalke waliwachapa Leverkusen 2-0

Huo ulikuwa ushindi wa nne msimu huu kwa FC Cologne ambao bado wanasalia kuwa mkiani mwa jedwali la Bundesliga.

Schalke walipata ushindi wa mbili bila mikononi mwa Bayer Leverkusen Guido Burgstaller na Nabil Bentaleb wakiwa wafungaji katika mechi hiyo ya jana na sasa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza msimu miongoni mwa timu nne bora.

Heiko Herrlich ni kocha wa Bayer Leverkusen.

Fußball Bundesliga FC Schalke Leon Goretzka und Max Meyer (Imago/Jan Huebner)

Mchezaji wa Schalke Max Meyer akisherehekea bao

"Bila shaka hili limekuwa pigo leo sitaki kulizungumzia. Kwa sasa inatubidi tuangalie tulipokosea na tuone tutakaporekebisha," alisema Herrlich. "Tulipata nafasi finyu sana katika mechi hii ukilinganisha na ilivyokuwa katika mechi iliyopita, kwa hiyo sasa ni lazima tuendelee kulifanyia kazi hilo."

Borussia Dortmund watakuwa wanaingia uwanjani usiku wa Jumatatu ambapo watakuwa wanawaalika FC Augsburg.

Bayern Munich licha ya kutoka sare wanaongoza wakiwa na alama 60 kisha walio kwenye nafasi ya pili ni Borussia Dortmund na alama 40 sawa na Schalke ila uchache wa mabao unawadunisha Schalke.

Eintracht Frankfurt nafasi yao ni ya nne wakiwa na alama 39 alama moja mbele ya Bayer Leverkusen wanaofunga orodha ya tano bora. Chini ya jedwali Mainz wana alama 24 katika nafasi ya kumi na nne kisha Hamburg wanawafuata na alama 17 sawa na FC Cologne ila wamewashinda Cologne kwa wingi wa mabao.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters/DPAE

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com