Bayern mabingwa wa Bundesliga kwa mara ya tano mfululizo | Michezo | DW | 01.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern mabingwa wa Bundesliga kwa mara ya tano mfululizo

Bayern Munich wameshinda kombe lao la Bundesliga kwa msimu wa tano mfululizo na kufikisha  idadi  ya  mataji  27  ya  ligi  hiyo  kwa  ushindi mnono  wa  mabao  6-0 dhidi  ya  kikosi  dhaifu  cha  VFL Wolfsburg

Kikosi  hicho  cha  kocha  Carlo Ancelotti kimepanua  mwanya  kwa  ushindi  huo dhidi  ya  timu  ya pili  katika  msimamo  wa  ligi  RB Leipzig  hadi  pinti  10  na kwa  hiyo  katika  michezo  mitatu  iliyosalia  katika  msimu huu  wa  ligi  haitawezekana tena  kuzifikia  pointi  hizo  na kuwapiku  mabingwa  hao.

Huyu  hapa mwenyekiti  wa  Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge. "Kwa  bahati  mbaya , katika  Champions  dhidi  ya  Real Madrid  kulikuwa  na uamuzi fulani  wa  refa  haukuwa mzuri. Na  katika  kombe  la  Ujerumani  pia  dhidi  ya Dortmund  bahati  haikuwa  upande  wetu. Pia tunacheza katika  wiki  za  mwisho  vizuri , lakini kwa  bahati  mbaya pamoja  na  hayo tumetolewa. Ni ubingwa  wa  Bundesliga tu ndio unawezekana, ambapo  katika  mchezo wa  34 haitakuwa furaha , ama bahati mbaya. Kwamba  unastahili ushindi  ama  la. Na  nafikiri , timu yetu imethibitisha , kwamba  wanastahili  kuitwa  mabingwa  halisi  wa Ujerumani  msimu  huu  kwa  mara  nyingine tena.

China | Karl Heinz Rummenigge eröffnet ersten Bayern München Standort in Shanghai (Getty Images/AFP/J. Eisele)

Mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz ZRummenige

"Si rahisi , kwamba  katika  Bundesliga  unaweza  kushinda tu, "  amesema  nahodha  wa  Bayern  akiwa  na  furaha tele  Philipp Lahm  baada  ya  ushindi  wa  jumla  ya  mataji manane  ya  ubingwa  wa  Ujerumani. Nahodha  huyo anatundika  madaluga baada  ya  msimu  huu.

RB Leipzig iliyotarajiwa  kuahirisha  sherehe  za  ubingwa wa  Bayern , iwapo  ingeishinda  timu  iliyoko  mkiani  mwa ligi  Ingostadt,ilishindwa  kufanya  hivyo  na  iliridhika  na sare  ya  bila  kufungana  na  kuipa  matumaini  Ingolstadt angalau  kwa  muda tu kuweza  kubakia  katika  daraja  la kwanza. Kwa  sare  hiyo Ingolstadt imeongeza  katika matumaini  yake kwa  kuwa na  pointi 29  pointi nne  tu kutoka  nafasi  ya 16  ambayo  inatoa  matumaini  ya kucheza  na  timu  ya  tatu  ya  daraja  la  pili  kuamua  nani anaingia   ama  kubaki  katika  daraja  la  kwanza. Nahodha wa  Ingoltadt Marvin Matip ameonesha  matumaini.

"Ndio , nafikiri  mtu akiangalia  kwamba  katika  dakika kumi za  mwisho tulicheza  tukiwa  pungufu , hii  ni  pointi  moja tuliyoipata  kutokana  na  ari. Tuna  bado  michezo  miwili nyumbani , na  mchezo  mmoja  ugenini  dhidi  ya Freiburg. Nadhani  bado  tuko  hai. Nimefarijika , kwamba tunaishi na  dhidi  ya  timu  ngumu  kama  Leipzig kupata pointi moja , ni  sawa  kabisa."

Timu  iliyoko  katika  nafasi  ya  mwisho  kabisa  katika Bundesliga  msimu  huu  SV  Darmstadt  98 ilijitutumua nayo  katika  mchezo  huu  wa  31  na  kuikaba  koo  FC Freiburg  na  kuishinda  bila  kutarajiwa kwa  mabao 3-0, na kufufua  pia  matumaini  yao  ya  kubakia  katika  daraja  la kwanza.

1. Bundesliga RB Leipzig v FC Ingolstadt 04 (Getty Images/AFP/R. Michael)

RB Leipzig wamedhamiria kujihakikishia nafasi ya pili

Hata  hivyo karibu nusu  ya  timu  za  Bundesliga  zinajikuta baina  ya  kuwania  nafasi  ya  kucheza  katika  ligi  ya Ulaya  na  hofu  ya  kushuka  daraja. Hamburg SV imejikuta  tena  wiki  hii  ikirejea  katika  madhila yaliyowakuta  misimu  miwili  iliyopita  ya  kukaribia  kusuka daraja. Msimu  huu  pia  hali  imeanza  kujitokeza  kuwa hivyo. Hamburg  iliangushiwa  kipigo  cha  mabo 4-0  dhidi ya  Augsburg   katika  mchezo  ambao  timu  zote zilikuwa katika  eneo  la  hatari  ya  kushuka  daraja. Kwa  ushindi huo Augsburg  imechupa  kutoka  nafasi  ya  16  hadi nafasi  ya  13 ,ikiwa  na  pointi  35 , ikizivuta  chini Mainz 05, Wolfsburg  na  Hamburg SV  ambazo  zote  zina  pointi 33.

Michezo  mitatu  iliyobaki  katika  Bundesliga  itaamua  nani anashuka  daraja  miongoni  mwa  timu  hizo. Lakini  pia wasi  wasi  umetanda  miongoni  mwa  timu  saba  za Bundesliga, ambazo  kila  moja  inaweza  kuliaga  daraja hilo. Timu  hizo  ni  Schalke 04 , Eintracht  Frankfurt, Bayer 04 Leverkusen , Augsburg, Mainz 05 , Wolfsburg  na Hamburg  ambazo  zinaweza  kushuka  daraja.

wakati  huo  huo  timu  za Borussia  Moenchengladbach, FC Koloni, Freiburg, Werder Bremen na Hertha Berlin zote  zina  nafasi  kuingia  katika  kinyang'anyiro cha  ligi ya  Ulaya  mwakani  zikiwa  na  pointi zinazotofauti  kwa kiasi  kidogo  tu  kabla  ya  michezo  hii  mitatu  ya  mwisho kufikia  mwisho.

Fußball Bundesliga 1899 Hoffenheim - Eintracht Frankfurt (Getty Images/AFP/A. Querfurth)

Hoffenheim wanatafuta kucheza Champions League

Mfutano  hata  hivyo  uko  baina  ya  makamu  bingwa msimu  uliopita Borussia  Dortmund  na  1899  Hoffenheim. Wazee  wa  kijijini  Hoffenheim wakiwa  katika  msimu  wao bora  kabisa  tangu  timu  hiyo  kuingia  katika  Bundesliga , wameipiku  Borussia  Dortmund  jana  katika  nafasi  ya  3 ambayo  inawahakikishia  kucheza  katika  awamu  ya makundi  ya  Champions League  msimu  ujao moja  kwa moja. Hoffenheim  iliikandika  Eintracht Frankfurt  jana Jumapili  kwa  bao 1-0  na  kufikisha  pointi 58  dhidi  ya  56 za  Borussia  Dortmund  ambayo  iliambulia  sare  ya  bila kufungana  na  FC Kolon siku  ya  Jumamosi.

Kocha  wa Frankfurt Nico Kovac alichooka sana: "Inauma  sana , wakati  unashindwa  katika  dakika  za mwisho  kutokana  na  mpira wa adhabu , wakati  kila  kitu kimsingi  kilikuwa  katika  hali  nzuri kabisa . Kikosi changu kilitoa  kila  kitu , ambacho  mwili  unacho. Bahati  mbaya haikuwezekana kufaidika  na  hilo, kwasababu tulifumba jicho kwa sekunde tu."

Katika  mchezo wa 32  wa  Bundesliga , vumbi  litatimka katika  uwanja  wa  Signal Iduna Park  mjini  Dortmund wakati Borussia  Dortmund  itakapowakaribisha  wazee  wa kijijini Hoffenheim  katika  kinyang'anyiro  cha  kuwania nafasi  ya  tatu  na  pia  Koln ikiikaribisha  Werder  Bremen katika  kuwania  nafasi  ya  kucheza  Ulaya. lakini  pia Hamburg iliyoko  katika  nafasi ya 16 inatafuta  kujinasua kutoka  katika  hatari  ya  kushuka  daraja  wakati itakapoikaribisha  nyumbani  Mainz 05  ambayo  nayo  ina pointi  sawa  na  Hamburg zitakapooneshana  kazi kuepuka  kushuka  daraja.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga