1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bartomeu kushughulikia suala la ufadhili wa Barca

20 Julai 2015

Kandarasi ya ufadhili wa klabu ya Barcelona na Qatar ni mojawapo ya masuala nyeti ambayo rais Josep Maria Bartomeu lazima ayashughulikie kufuatia kuchaguliwa kwake tena mwishoni mwa wiki.

https://p.dw.com/p/1G1mO
FC Barcelona Rücktritt Präsident Sandro Rosell
Picha: Reuters

Ufadhili huo wa jezi ya Barca, unaotarajiwa kukamilika mwaka ujao, ulikuwa mada kuu wakati wa kampeni za uchaguzi na Bartomeu ameubadilisha msimamo wake kutoka ule wa kuwa mfuasi mkubwa wa Waqatari hadi ule wa kuwa mwepesi kwa wafadhili wengine mbadala.

Aliwaambia waandishi wa habari mapema mwezi huu kuwa wamezungumza na kampuni muhimu ya teknolojia barani Asia ambayo inataka kuifadhili jezi ya Barca badala ya Shirika la Ndege la Qatar.

Wagombea wenzake katika uchaguzi huo, Joan Laporta na Agusti Benedito waliwaongoza wanaopinga klabu hiyo kuwa na mkataba na Qatar, wakihoji kuwa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta na gesi haionyeshi maadili ya kiutu ya klabu hiyo. Chini ya urais wa Laporta, Barca ilifikia makubaliano ya kuiweka nembo ya Shirika la Umoja wa Kimataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF kwenye jezi na mashabiki wengi hawakufurahia wakati mikataba ilifikiwa kuiweka nembo ya UNICEF nyuma ya jezi na nafasi yake mbele kuchukuliwa na Qatar Foundation na kisha Qatar Airways.

Bartomeu sasa ataongoza Barca kwa miaka sita ijayo, na ameahidi kuwa klabu hiyo itaendelea kutamba duniani. Alisema "Tutaendelea kukua, tutaendelea kushinda, ikiwa tutaendelea kumpa kocha Luis Enrique na mafundi wake wachezaji wazuri na mazingira mazuri ya kazi ili kuendelea na mtindo wao wa kushinda walioanza kwa kunyakua mataji matatu. Tutaendelea kuimarika ikiwa tutatunza akademi yetu ya vijana ili iendelee kuwa msingi wa timu ya kwanza".

Bartomeu alichukua usukani Januari 2014 kutoka kwa Sandro Rosell aliyejiuzulu kufuatia uchunguzi kuhusiana na usajili wenye utata wa nyota wa Brazil Neymar.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/APE/DPA/Reuters
Mhariri:Josephat Charo