Barrow kuapishwa kama ilivyokuwa imepangwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Barrow kuapishwa kama ilivyokuwa imepangwa

Msemaji wa rais mteule wa Gambia Adama Barrow amesema kuwa rais mteule ataapishwa Januari 19 kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwa kusema kuwa utawala wa Jammeh utakamilika Januari 19 siku ambayo rais mteule Barrow ataanza rasmi awamu yake ya uongozi.  "Ataapishwa na atachukua ofisi tarehe hiyo hiyo bila kushindwa" alisema  Mai Fatty

Sherehe za kuapishwa zinatarajiwa kufanyika Januari 19 lakini rais anayemaliza muda wake Yahya Jammeh, anapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Disemba 1 mwaka jana katika mahakama ya juu nchini humo.

Shirika la habari la APS limemnukuu rais wa Senegal Macky Sall  akisema kuwa, amekubali kumpokea Barrow katika nchi yake kufuatia ombi la nchi wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Maghabiri, ECOWAS, makubaliano ambayo yalifikiwa katika mkutano wa viongozi wa Ufaransa na Afrika uliofanyika katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

ECOWAS iliiweka Alhamisi wiki iliyopita kuwa ndio tarehe ya mwisho ya kujaribu kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Gambia, radio ya kimataifa ya Ufaransa RFI ilimnukuu rais wa Togo Faure Gnassingbe akisema, kitendo cha Jammeh kukataa kukubali kushindwa kinachochea hofu ya kuwepo kwa machafuko katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Adama Barrow Präsident von Gambia (Getty Images/AFP)

Rais mteule wa Gambia Adama Barrow

Rais mteule Barrow alihuduria mkutano huo wakati Jammeh hakuhudhuria, mkutano huo unafuatia mazungumzo kati ya wapatanishi wa ECOWAS na viongozi hao wawili yaliyofanyika nchini Gambia.

Taarifa kutoka katika ofisi ya rais mteule Barrow inasema kuwa  mkutano kati ya rais Jammeh, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na wawakilishi wengine wa ECOWAS haukuwa na matokeo mazuri.

Mazungumzo ya ECOWAS yalianza saa kadhaa baada ya chama kikuu cha upinzani nchini Gambia kufungua mashitaka katika mahakama ya juu kupinga kuapishwa kwa rais mteule Januari 19.

Awali ECOWAS iliahidi kutuma vikosi nchini Gambia kuhakikisha kuwa kunakuwa na kubadilishana madaraka kwa amani, iwapo Jammeh ataendelea kushikilia msimamo wake wa kukataa kuachia madaraka baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miongo miwili.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com