Bandari na uwanja wa ndege Yemen kufunguliwa kwajili ya misaada | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bandari na uwanja wa ndege Yemen kufunguliwa kwajili ya misaada

Muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen unasema utafungua bandari muhimu za bahari ya Sham na uwanja wa ndege wa Sanaa baada ya kuzifunga kwa muda kufuatia shambulio la kombora mjini Riyadh. 

Muungano huo umesema utaifungua bandari ya Hodeida kupokea vifaa muhimu vya misaada vinavyohitajika kwa haraka na uwanja wa ndege wa Sanaa kwa ndege za Umoja wa Mataifa mchana wa alkhamisi.

Haukutaja wakati au kama ungeweza kuondoa hatua ya kuzuia safari za meli za kibiashara kutoka na kuingia Yemen.

Hodeida, mji ambao unadhibitiwa na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran - mpinzani mkuu wa Saudi Arabia, ni njia muhimu ya bidhaa za chakula na madawa zinazohitajika sana Yemen.

Muungano huo uliweka kizuizi cha bandari za Yemen na viwanja vya ndege siku mbili baada ya Wahouthi kufyetua kombora kwenye ardhi ya Saudi Arabia mnamo Novemba 4.

Kombora hilo lilizuiwa karibu na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid mjini  Riyadh, na kusababisha vita vya maneno kati ya Iran na Saudia Arabia, ambayo ililaumu Iran kwa "ukatili wa moja kwa moja" na kwa kuwapa silaha kwa waHouthi.

Umoja wa Mataifa ulisema siku ya Jumatano kuwa ulijulishwa na Saudi Arabia juu ya  uamuzi wa kuzifungua  tena bandari za Yemeni za Hodeida na Saleef, pamoja na uwanja wa ndege wa mji mkuu Sanaa.

"Tunafuatilia maendeleo haya na kujaribu kuona ikiwa kweli yatafanyika, "msemaji wa Umoja wa Mataifa  Farhan Haq aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja huo mjini  New York."     

"Bila shaka, kama hilo likitokea itakua hatua ya maendeleo ,ya kukubalika na muhimu sana."

Shirika la Msaada la Save the Children liliupongeza uamuzi wa muungano huo  lakini lilisema ufunguzi wa bandari na uwanja wa ndege hautatoshi kukabiliana na  ukame unaoweza kutokea  nchini Yemen".

Taswira ya mi wa San´aa Yemen

Taswira ya mji wa San´aa Yemen

Misaada  ya kibinadamu inatoa tu sehemu ndogo ya bidhaa muhimu zinazohitajika Yemen - vifaa vya kibiashara ni muhimu kulisha idadi ya watu na kuhakikisha huduma za msingi zinaendelea kupatikana," alisema.

Mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa Mark Lowcock aliomba vikwazo hivyo viondolewe mnamo Novemba 8, akionya kuwa Yemen ingeweza kukabiliwa na "baa kubwa la njaa ulimwenguni kwa miaka mingi"

Serikali ya wahouthi mnamo siku ya  jumanne ilitangaza kwamba uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa unafanya kazi tena wiki moja baada ya shambulizi la muungano wa kijeshi  unaongozwa na Saudia kuuharibu mtambo wa kuongoza safari za ndege.

Uwanja huo wa ndege ulikuwa wazi tu kwa ajili ya ndege zinazopeleka msaada wa kibinadamu.

Wakishirikiana na  rais wa zamani  Ali Abdullah Saleh, waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wanadhibiti mji mkuu wa Sanaa pamoja na maeneo  ya Yemen Kaskazini.

Mnamo mwaka wa 2015, Saudia Arabia na washirika wake walijiunga na mapigano ya serikali ya Yemen dhidi ya waasi hao.

Zaidi ya watu 8750 wameuawa.

Taifa hilo pia linakabiliwa na mlipuko wa  kipindupindu na mamilioni wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na ukame.

Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef   

     

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com