Ballon d′Or 2014: Neuer, Messi au Ronaldo? | Michezo | DW | 12.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ballon d'Or 2014: Neuer, Messi au Ronaldo?

Cristiano Ronaldo ndiye anayeonekana kushinda tuzo ya mchezaji bora ulimwenguni ya Ballon d'Or kwa mwaka wa pili mfululizo katika hafla itakayoandaliwa baadaye leo mjini Zurich.

CR7 anatazamiwa kuwabwaga Manuel Neuer na Lionel Messi. Messi amekuwa katika nafasi mbili za kwanza za tuzo hiyo kwa miaka saba iliyopita, lakini licha ya mwaka mwingine mzuri wa 2014, anaonekana mara hii kujikokota nyuma ya wapinzani wake hao wawili.

Baada ya kuwa na matokeo mabaya katika Kombe la Dunia, ambapo Ureno iliondolewa katika awamu ya makundi, hali hiyo haijamzuia Ronaldo kudhihirisha kuwa anastahili kupata zawadi hiyo kwa mara ya tatu. Nyota huyo wa Real Madrid, amefunga magoli 61 katika mashindano yote ya msimu uliopita baada ya kuisaidia klabu yake kunyakua Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Copa del Rey na UEFA Super Cup kabla ya kuufunga mwaka wa 2014 kwa kubeba Kombe la Klabu Bingwa Ulimwenguni. alifunga mabao 17 katika Champions League msimu uliopita na tayari ana magoli 26 katika mechi 16 za La Liga msimu huu.

Cristiano Ronaldo Statue

Nyota wa Real Madrid na Ureno CR7 anapigiwa upatu kunyakua tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka wa pili mfululizo

Hata hivyo Neuer – ambaye ndiye mchezaji pekee kati ya wachezaji sita wa Ujerumani waliokuwa kwenye orodha ya mwanzo, kufikia orodha ya tatu bora – ana nafasi nzuri ya kuwa kipa wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu Lev Yashin wa Muungano wa Kisovieti mwaka wa 1963, na Mjerumani wa kwanza tangu Lothar Matthaeus mwaka wa 1990, mwaka ambao iliyokuwa Ujerumani Magharibi ilishinda Kombe la Dunia nchini Italia.

Baada ya kuisaidia timu yake Pep Guardiola ya Bayern kushinda mataji mawili ya Ujerumani, Neuer mwenye umri wa miaka 28, aling'aa sana langoni mwa timu ya Ujerumani iliyonyakua Kombe la Dunia ilipoibwaga Argentina goli moja kwa sifuri baada ya muda wa ziada katika fainali iliyochezwa uwanjani Maracana.

Licha ya sifa yake, na ukweli kwamba alifunga mabao 58 katika mechi 66 za klabu yake ya Barca na taifa lake la Argentina katika mwaka wa 2014, nafasi ya Messi inatilisha shaka kuwa alishindwa kushinda taji lolote la Barcelona.

Na wakati akiwa nahodha wa Argentina katika Kombe la Dunia, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alishindwa kudhihirisha usogora wake katika hatua ya mwondowano hata kama alitunukiwa tuzo ya Mpira wa Dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa dimba hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com