Bahrain yaripuka tena | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bahrain yaripuka tena

Siku moja baada ya kutangazwa kwa hali ya hatari na kuingia kwa majeshi ya Jumuiya ya Nchi za Ghuba nchini Bahrain, jeshi limeuvamia uwanja wa Pearl walipokusanyika waandamanaji wanaoupinga utawala wa Al Khalifa.

Mwandamanaji akiwa katikati ya moshi wa mabomu

Mwandamanaji akiwa katikati ya moshi wa mabomu

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, kiongozi wa chama cha Waislamu wa Madhehebu ya Shia bungeni, Abdel Jalil Khalil, kinachotokezea hivi sasa ni "mauaji ya kuteketeza".

"Jambo hili halitokezei hata katika uwanja wa vita, seuze kwenye uwanja ambapo watu wamekusanyika kwa amani, na hili halikubaliki". Amesema Khalil.

Inaripotiwa kuwa usiku wa kuamkia leo, vikosi vya jeshi na polisi, viliuvamia uwanja wa Pearl, vikawashambulia waandamanaji waliokuwa ndani ya mahema yao na walio mitaani, vikilazimisha kulisafisha eneo hilo, ambalo limekuwa kitovu cha maandamano ya karibuni wiki tatu sasa dhidi ya utawala wa Al Khalifa.

Mwanamke wa Kibahrain akilia baada ya kuvamiwa na wanajeshi

Mwanamke wa Kibahrain akilia baada ya kuvamiwa na wanajeshi

Haijafahamika bado ikiwa wanajeshi walioshiriki kwenye operesheni hii ni pamoja na wale wa kigeni kutoka Saudi Arabia na Imaraat, lakini Khalil anasema kuwa wanajeshi na polisi wamejaa kila sehemu mitaani, wakikamata na kufyatua risasi kwa mtu yeyote anayejaribu kukaidi amri yao.

Kuna taarifa za nyumba za watu binafsi na sehemu za kufanyia shughuli za maziko kupokea mamia ya wahanga, kwani vikosi vya jeshi vinaripotiwa kuzizunguka hospitali kuzuia ama majeruhi kupelekwa huko na au madaktari kuwahudumia.

Kiasi ya watu 200 wamejeruhiwa kwa mabomu ya machozi na daktari mmoja kutoka hospitali ya Salmaniya, amekiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, kwamba hali ni ya kuvunja moyo sana.

"Wanajeshi wa Bahrain na Saudi Arabia wanafanya uhalifu dhidi ya binaadamu kwenye ardhi ya Bahrain. Kuna majeruhi wengi hapa. Huko Sitra pia majeruhi wamelala barabarani, hatujui wanaendeleaje, kwa sababu hatuwezi kufika huko. Polisi wameyazuia magari ya kuhudumia wagonjwa, maji yamefungwa, mmoja ametufia hapa hapa." Amesema daktari huyo.

Waandamanaji wakimbeba majeruhi

Waandamanaji wakimbeba majeruhi

Vilivyothibitishwa hadi sasa ni vifo vya watu watatu. Televisheni ya taifa ya nchi hiyo inasema kwamba, hapo jana, waandamanaji walimuua kwa kumpiga risasi mwanajeshi mmoja wa Saudi Arabia.

Jamii ya Washia nchini humo imeutaka ulimwengu wa Kiislamu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusaidia haraka iwezekavyo ili kuzuia mauaji zaidi.

Hapo jana, maelfu ya watu waliandamana kutoka uwanja wa Pearl kuelekea ubalozi wa Saudi Arabia kupinga kitendo cha majeshi ya nchi hiyo kuingia Bahrain.

Maandamano hayo, hata hivyo, hayakuzuiwa na polisi na yalikuwa ya amani. Nabil Rajab wa Kituo cha Haki za Binaadamu anasema, raia wa Bahrain hawapendelei hata kidogo nchi yao kuingiliwa na mataifa ya nje, hata kama ni Waarabu wenzao.

"Hali ni tete na mbaya sana. Watu wamekasirishwa na Saudi Arabia na nchi nyengine za Ghuba kuleta majeshi yao hapa, kuja kukandamiza maandamano ya amani, ambayo watu wanadai tu haki zao za kisiasa na kuheshimiwa kwa haki za binaadamu. Hili hatulikubali kabisa na tutalipinga mpaka majeshi haya yaondoke." Amesema Rajab.

Wafuasi wa upinzani wanahsi kuwa Marekani imewasaliti, kwa kuinyamazia kimya serikali ya Bahrain inapowakandamiza waandamani. Hadi sasa Marekani haijaonesha kupinga majeshi ya nchi za Ghuba kuingia Bahrain.

Mwandishi: Carsten Kuhntopp/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com