1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado waziri mkuu Italia hajapatikana

22 Mei 2018

Mazungumzo kati ya rais wa Italia na wakuu wa mabaraza ya bunge la nchi hiyo yamemalizika bila kutangazwa kwa uamuzi wa kumuidhinisha waziri mkuu mpya aliyeteuliwa na muungano wa vyama vya siasa kali.

https://p.dw.com/p/2y84c
Italien Staatschef Mattarella will "neutrale" Regierung
Picha: picture-alliance/dpa/ANSA/E. Ferrari

Mattarella, ambaye lazima amthibitishe mtu aliyependekezwa na vyama kuwa waziri mkuu ili aweze kuunda serikali, alikuwa na kikao cha mashauriano na viongozi wa mabaraza ya bunge mchana wa leo, lakini ofisi yake haijatoa hadi sasa undani wa mazungumzo hayo.

Giuseppe Conte, profesa wa sheria mwenye umri wa miaka 54 na mtu asiyefahamika sana kisiasa, alitajwa hapo jana Jumatatu na muungano wa Vuguvugu la Nyota Tano na chama cha kizalendo, League, kuwa ndiye chaguo lao kwa nafasi ya waziri mkuu.

Mattarella ndiye mwenye kauli ya mwisho juu ya nani ashikilie nafasi hiyo, lakini pendekezo la Conte lilionekana tangu awali kuzusha wasiwasi kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya, mjini Brussels, na hata masoko ya kifedha.

Viongozi wa muungano huo wa siasa kali za  mrengo wa kulia wanaomuunga mkono Conte, wameahidi makato makubwa ya kodi, kulegeza hatua za kubana matumizi, kuongeza matumizi kwenye mafao na pia kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali. 

Mipango hii ya matumizi ya serikali mpya inakuja hata katika wakati ambapo Italia ikitajwa kuwa na kiwango kikubwa kabisa cha deni la ndani . Vyama hivyo vinavyopingana na sarafu ya euro na Umoja wa Ulaya pia viliahidi kuupitia upya mkataba kati ya Italia na Umoja wa Ulaya.

Ikiwa Mattarella atamridhia Conte kuwa waziri mkuu na hivyo kuunda baraza lake la mawaziri, basi serikali mpya inatazamiwa kutangazwa ama wiki hii au ijayo.

Wasiwasi wazidi Umoja wa Ulaya

Kombobild Di Maio und Salvini
Viongozi wakuu wa muungano wa siasa kali: Luigi Di Maio wa Vuguvugu la Nyota Tano (kushoto) na Matteo Salvini wa cham cha siasa kali za mrengo wa kulia, Lega.Picha: AFP/T. Fabi

Kusuasua huku kuundwa kwa serikali na pia kitisho cha sera za muungano wa kisiasa wa Italia kumezusha wasiwasi kutoka kwa wawekezaji na mataifa mengine ya Ulaya. Wawekezaji wa Ujerumani, ambao mara kadhaa hushutumiwa kwa kulazimisha hatua kali za kubana matumizi na mataifa ya kusini mwa Ulaya, wameikosoa mipango hiyo ya serikali mpya wanayosema haitabiriki. 

"Serikali mpya ya Italia inahitajika kwa haraka sana kuunga mkono sera za kiuchumi na Ulaya, vyenginevyo naona kitisho cha kuwepo kwa mtafaruku kwenye masoko ya kifedha," alisema Marcel Fratzscher, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Ujerumani, DIW.

Msimamo kama huo umeelezwa na Mkuu wa Baraza la Biashara na Viwanda la Ujerumani, Achim Dercks.

Waziri wa Mambo ya Ulaya Nathalie Loiseau, ameonya hivi leo juu ya mustakabali wa serikali hiyo mpya ya Italia, akisema kwamba huenda ikajikuta peke yake. 

Deni la euro trilioni 2.3 la Italia ni asilimia 132 ya pato lake jumla la ndani, kikiwa ni kiwango cha juu kabisa ukiiondoa Ugiriki. Umoja wa Ulaya unabashiri kwamba deni la Ugiriki litaendelea kubakia hapo hapo kwa mwaka huu mzima, ambapo ni zaidi ya mara mbili ya ukomo wake wa kukopesheka wa asilimia 60. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman