Anthony Ujah kujiunga na Bremen kutoka Cologne | Michezo | DW | 06.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Anthony Ujah kujiunga na Bremen kutoka Cologne

Mshambuliaji wa FC Cologne Anthony Ujah atajiunga na Werder Bremen mwishoni msimu huu. Ujah amesaini mkataba wa miaka minne hadi 2019 kwa kiasi cha fedha ambacho hakijafichuliwa

Ujah mwenye umri wa miaka 24, ambaye ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Nigeria ameamua kuihama Cologne mwishoni mwa msimu baada ya kipengele cha kufidia uhamisho wake kukubaliwa na Werder Bremen.

Mkurugenzi wa michezo wa Werder Bremen Thomas Eichin amesema mazungumzo na Anthony yalikuwa makali na marefu, na walihakikisha kuwa walikua na picha kamili kumhusu. Alimsifia mchezaji huyo kuwa mwenye kasi, hatari mbele ya mlango na anayeweza kuendelea kuimarika katika klabu ya Bremen.

Kuna uwezekano Ujah amesajiliwa kuvaa daluga za Davie Selke, ambaye anajiunga na klabu ya Red Bull Leipzig mwishoni mwa msimu huu kwa kiasi cha euro milioni nane.

Ujah, mfungaji bora wa Cologne msimu huu, (magoli 10), alijiunga na klabu hiyo kwa mkopo mwaka wa 2012 kutoka Mainz kabla ya kusaini mkataba wa kudumu msimu uliopita kwa euro milioni mbili. Kufikia sasa, katika maisha yake na Cologne, mshambuliaji huyo ameichezea klabu hiyo mechi 100 katika divisheni mbili za ligi Ya Ujerumani – Bundesliga na Kombe la Shirikisho DFB Pokal, ambapo amefunga magoli 36 na kutoa pasi za mwisho zilizochangia kufungwa magoli 10.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo