1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Ukraine, Urusi zathibitisha mazungumzo mapya UAE

2 Februari 2026

Mashambulizi ya droni za Urusi yameua raia na kulenga hospitali nchini Ukraine, huku Ukraine ikishambulia Belgorod nchini Urusi. Haya yanajiri wakati pande hizo mbili zikithibitisha duru nxingine ya mazungumzo nchini UAE

https://p.dw.com/p/57uRe
UAE Abu Dhabi 2026 | Rais Mohammed bin Zayed awapokea wajumbe wa mazungumzo ya Ukraine
Duru ya kwanza ya mazungumzo yanayoratibiwa na Marekani ilifanyika mjini Abu Dhabi Januari 23, 2026.Picha: Ryan Carter/UAE Presidential Court/REUTERS

Mashambulizi mapya ya droni za Urusi yameua raia nchini Ukraine, yakiashiria kuendelea kwa vita kali licha ya maandalizi ya mazungumzo mapya ya amani yanayopatanishwa na Marekani.

Takriban watu kumi na wawili waliuawa katika mji wa Pavlohrad, katikati mwa Ukraine, baada ya droni ya Urusi kulipiga basi lililokuwa likiwabeba wafanyakazi wa mgodini wakirejea nyumbani.

Kampuni ya nishati ya DTEK ilisema shambulio hilo pia liliacha watu 16 wakiwa wamejeruhiwa, tisa kati yao wakiwa katika hali mbaya.

Mashambulizi mengine ya droni yalilenga eneo la mgodi wa makaa ya mawe, yakiongeza hofu ya kulengwa kwa miundombinu muhimu ya kiraia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alilaani mashambulizi hayo, akiyataja kuwa uhalifu na dalili ya kuongezeka kwa mapigano.

Ukraine, Mkoa wa Dnipro | Shambulio la droni la Urusi lalenga basi
Droni ya Urusi ililipiga basi la kampuni ya DTEK katika wilaya ya Pavlohrad, mkoa wa Dnipro nchini Ukraine. Kulingana na taarifa za awali, watu 12 waliuawa na wengine 7 walijeruhiwa.Picha: State Emergency Service of Dnipro Region

Mashambulizi ya raia na miundombinu

Zelenskyy alisema mashambulizi hayo yalikuwa sehemu ya wimbi kubwa la droni, huku jeshi la anga la Ukraine likiripoti takriban mashambulizi 90 kwa usiku mmoja.

Kusini mwa nchi, droni za Urusi zilishambulia hospitali ya wajawazito katika mji wa Zaporizhzhia, na kujeruhi wanawake na mtoto mdogo.

Picha zilizotolewa na maafisa wa eneo hilo zilionyesha uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na madirisha yaliyopasuka na vyumba vilivyoharibiwa.

Awali, mashambulizi ya usiku katika Dnipro yaliua watu wawili na kuharibu nyumba ya makazi. Ukraine inasema mashambulizi haya yanaonyesha kuwa Urusi haina dhamira ya kweli ya kusitisha vita.

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

Mazungumzo ya amani yakumbwa na changamoto

Licha ya mashambulizi hayo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametangaza kuwa mazungumzo mapya ya amani kati ya Ukraine, Urusi na Marekani yatafanyika Abu Dhabi.

Mazungumzo hayo sasa yamehakikishwa rasmi na Kremlin, baada ya kuahirishwa kutoka mwishoni mwa wiki hadi katikati ya wiki hii.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema kuwa mazungumzo hayo awali yalipangwa kufanyika Jumapili, lakini yalicheleweshwa kutokana na changamoto za uratibu wa ratiba za pande zote tatu.

"Kwa hakika yalipangwa kufanyika Jumapili iliyopita, lakini ilihitajika uratibu zaidi wa ratiba za pande tatu,” Peskov aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa duru ya pili ya mazungumzo sasa itafanyika Jumatano na Alhamisi.

Kremlin imethibitisha kuwa mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yatafanyika Abu Dhabi, ikiwa ni duru ya pili ya majadiliano yanayopatanishwa na Marekani kuhusu kumaliza karibu miaka minne ya vita.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Rais Zelenskiy alikuwa tayari ametangaza Jumapili kuwa mazungumzo hayo ya pande tatu yatafanyika Jumatano na Alhamisi katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hata hivyo, licha ya ratiba hiyo kuthibitishwa, mazungumzo hayo yanaendelea kukabiliwa na vikwazo vikubwa, hususan suala la eneo la ardhi, huku Urusi ikidhibiti takriban asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine na kudai udhibiti kamili wa eneo la mashariki la Donetsk.