1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Farook alijifunza itikadi kali

4 Desemba 2015

Mzaliwa wa Marekani aliye kuwa pia Muisilamu ambaye pamoja na mkewe waliwaua watu 14 kwa kuwapiga risasi huko Carlifornia,huenda walijifunza itikadi kali na pia kuwasiliana na washukiwa wa ugaidi wanaofahamika.

https://p.dw.com/p/1HHhr
schießerei san bernardino kalifornien usa
Picha: picture-alliance/dpa

FBI ambayo imeonya kuwa ni mapema kuhusisha shambulizi hilo na ugaidi,inaongoza uchunguzi huo wa mashambulizi ya siku ya Jumatano San Bernardino.

Maajenti walifuatilia ushahidi ili kubaini kilichomfanya Syed Farook wa umri wa miaka 28 na mke wake mwenye umri wa miaka 27 kutoka Pakistan Tashfeen Malik kufanya mashambulizi ambayo pia yalisababisha watu 21 kujeruhiwa.

Maafisa wa usalama walionukuliwa na gazeti la New York Times walisema FBI wanachukulia shambulizi hilo kama tukio la kigaidi,ingawa shirika hilo halijakamilisha uchunguzi na nia ya tukio hilo halijabainika.

CNN imenukuu maafisa,wakisema Farook alikuwa akiwasiliana na washukiwa wa Ugaidi katika nchi za ng´ambo na alikuwa amejifunza itikadi kali baada ya kumuoa Malik nchini Saudi Arabia mwaka uliopita,ingawa Imamu mmoja katika msikiti alikohudhuria anasema Farook hakuonyesha dalili zozote za aina hiyo.

FBI watafuta ushahidi

FBI ambao walipekua simu na tarakilishi za watu hao wawili,walipata ushahidi kuwa Farook alikuwa amewasiliana na watu hao wakereketwa nchini humo na ng`ambo miaka michache iliyopita, gazeti la Times lilisema huku likiongeza kuwa maafisa wa congress wamefahamishwa kuhusu uchunguzi huo.

Huku likinukuu afisa mkuu wa serikali ya majimbo,Gazeti la Lose Angeles Times limesema Farook aliwasiliana na washukiwa wachache wakereketwa.Afisa huyo amesema kuna ushahidi kuwa aliwasiliana na mtu mmoja ambaye anafuatiliwa kama mtuhumiwa wa ugaidi.

Maafisa wamesema uhusiano wa Farook na mtu huyo ni wa kumhusisha naye lakini uhusiano huo unadhihirisha kuwa huenda kukawa na mpango wa kina wa kigaidi katika shambulizi hilo la Carlifornia.

Karibu watu 3000 walihudhuria ibada siku ya Alhamisi kwa ajili ya wahanga hao,huku wakiwasha mishumaa na kusikiliza hotuba za maombolezo.

Ibada ya kuwakumbuka waliouawa California
Ibada ya kuwakumbuka waliouawa CaliforniaPicha: Reuters

Rais Barack Obama wa Marekani ambaye aliamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti hadi siku ya Jumatatu,alisema shambulizi hilo linaweza kuwa la kigaidi lakini akaonya dhidi ya kufanya uamuzi huo haraka.

"Hadi sasa hatujui ni kwanini tukio hilo baya lilitokea"amesema Obama ambaye mara kwa mara ametoa mwito kwa bunge la Marekani,Congress linalodhibitiwa na Republican kupitisha sheria kali za kudhibiti bunduki baada ya msururu wa mashambulizi ya bunduki nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Sababu za kuamini lilikuwa tukio la kigaidi

Baadhi ya sababu zinazofanya mamlaka kuamini tukio la Jumatano ni la kigaidi ni pamoja na silaha nyingi ambazo watu hao walikuwa wamehifadhi,safari zao za nchi za nje,na kuonekana kwamba walikuwa wamepanga kutekeleza shambulizi hilo.

Naibu mkurugenzi wa FBI anayehusika na ofisi ya Los Angeles amesema baada ya kutokea mauji hayo kuwa lazima tukio hilo lilipangwa, lilotokea wakati wa sherehe ya wafanyikazi wa kaunti katika kituo cha huduma za kijamii.

Mkuu wa Polisi katika eneo la San Bernardino Jarrod Burguan amesema Farook na mke wake walimuacha mtoto wao wa miezi sita kwa mamake Farook,walifyatua karibu risasi 150 ndani ya kituo hicho wakati wa ufyatulianaji wa risasi na polisi ambapo waliweza kuawa baada ya kutafutwa na polisi.

Amesema uchunguzi umebaini risasi elfu 5000 katika nyumba ya watu hao wawili na mabomu 12 pamoja na bidhaa za kutengeneza mabomu.

Mwandishi:Bernard Maranga/AFP

Mhariri:Josephat Charo