1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ALGIERS : Rais Sarkozy agoma kuiomba radhi Algeria

10 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBkG

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye anatarajiwa kuanza ziara yake ya siku moja nchini Algeria leo hii ametetea kugoma kwake kuomba radhi kwa maovu ya wakati wa ukoloni kwa nchi hiyo kwa kusema kwamba viongozi wanapaswa kuangalia mbele na sio kulalamika.

Algeria mshirika mkubwa wa biashara kwa Ufaransa barani Afrika kwa muda mrefu imekuwa ikidai Ufaransa iombe radhi kwa mauaji wakati wa miaka 132 ya utawala wake wa kikoloni ambao ulimalizika kwa uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1962 baada ya vita vya miaka minane.

Sarkozy akisisitiza msimamo wake wa muda mrefu ameyambia magazeti ya Algeria ya El Watan na El Akhbar kwamba vijana walioko katika pande zote mbili za bahari ya Mideterranean wanaangalia mustakbali zaidi kuliko kipindi cha zamani na kwamba kile wanachokitaka ni vitu vya uhakika.

Hiyo ni ziara ya kwanza ya Sarkozy nje ya bara la Ulaya tokea achaguliwe kuwa rais hapo mwezi wa May na atakutana na Rais Abdelaziz Bouteflika kabla ya kwenda Tunis kukutana na Rais Zine al Abidine ben Ali.