1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
16 Oktoba 2020

Yaliyoandikwa juu ya Afrika kwenye magazeti ya Ujerumani ni pamoja na janga la moto kwenye mlima Kilimanjaro nchini Tanzania na juu ya uchaguzi wa nchini Guinea ambako rais Alpha Conde anawania muhula wa tatu wa urais.

https://p.dw.com/p/3k144
Guinea Präsidentschaftswahl 2020 l Kampagne des Präsidenten Conde
Picha: Cellou Binani/AFP/Getty Images

die tageszeitung      

Na tunaanza na makala ya gazeti la die tageszeitung juu ya uchaguzi wa nchini Guinea ambako rais Alpha Conde anawania muhula wa tatu wa urais hatua ambayo imesababisha mgogoro nchini. Die tageszeitung linasema wakati Guinea inafanya uchaguzi, eneo lote la Afrika Magharibi linagwaya.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hatua ya rais Conde kuwania muhula wa tatu imesababisha ghasia na chuki miongoni mwa watu wa Guinea. Gazeti linaarifu kwamba uamuzi wa rais Conde umemtia wasiwasi mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague Fatou Bensouda. Gazeti hilo linasema hali nchini Guinea imeendelea kuwa ya utata kadri siku ya uchaguzi ilivyokuwa inakaribia na linakumbusha kilichotokea nchini Mali ambako wanajeshi wametwaa mamlaka kwa kushangiliwa na wananchi waliokuwa wamefadhaishwa na utawala wa Ibrahim Boubacar. Gazeti la die Tageszeitung linaeleza kwamba rais Alpha Conde mwenye umri wa miaka 82 anagombea muhula wa tatu baada ya katiba kubadilishwa mnamo mwezi wa Februari.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya janga la moto kwenye mlima Kilimanjaro nchini Tanzania. Linasema juhudi zinafanyika kupambana na janga hilo ambapo helikopta pia zinatumika. Gazeti linasema moto huo unawaka katika sehemu ya mashariki ya mlima. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba mlima Kilimanjaro wenye urefu wa mita 5965 ndio mrefu kabisa barani Afrika ni fahari ya Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine moto huo ulizuka Jumapili iliyopita.

Mpaka sasa hakuna taarifa juu ya kilichosababisha moto huo. Hata hivyo gazeti limamnkulu mtaalamu wa taaluma ya viumbe hai Andreas Hemp alisema kwamba mabadiliko ya tabia nchi ni sababu mojawapo ya janga lililoukumba mlima Kilimanjaro. Mtaalamu huyo kutoka Ujerumani amekuwa anafanya utafiti kwenye mlima huo kwa miaka 30 sasa.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba moto pia ulizuka kwenye mlima huo mnamo mwaka 2016. Gazeti hilo limemkulu mtaalamu huyo wa Ujerumani akieleza kwamba kipindi 

cha mvua kilichoanza kitasaidia juhudi za kuuzima moto huo mkubwa.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linatahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka idadi ya watu wasiopata chakula cha kutisha duniani. Limemnukulu mwenyekiti wa shirika la misaada ya chakula duniani Marlehn Thieme akitanabahisha kuwa dunia haitalifikia lengo la kukidhi mahitaji ya chakula kwa wote hadi mwaka 2030 kama ilivyokusudiwa hapo awali. Mwenyekiti huyo aliwaambia waandishi habari mjini Berlin kuwa idadi ya watu milioni 690 waliokuwa hawapati chakula cha kutosha mwaka uliopita inatarajiwa kuongezeka pia kutokana na majanga ya asili. Hata hivyo katika ripoti aliyowasiliswha kwa waandishi habari mwenyekiti huyo hakujumisha maafa ya mafuriko na nzige kwenye upembe wa Afrika.   

Gazeti hilo limemnukulu mwenyekiti wa shirika la Ujerumani la misaada ya chakula duniani Marlehn Thieme akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na juhudi za kupambana na njaa duniani. Na ndiyo sababu, gazeti la Neues Deutschland linasema mwenyekiti huyo amefurahishwa kwamba tuzo ya amani ya Nobel mwaka huu imetolewa kwa shirika la chakula duniani WFP. Hata hivyo mwenyekiti huyo amesisitiza ulazima  wa kuwapo dhamira ya kisiasa katika kufanikisha juhudi za kupambana na baa la njaa.

Der Tagesspiegel

Tunakamilisha na makala ya gazeti la Der Tagesspiegel kuhusu sera ya ulinzi ya Ujerumani juu ya Mali baada ya serikali ya nchi hiyo kuangushwa na wanajeshi hivi karibuni. Gazeti hilo linasema serikali ya Ujerumani inafanya tahadhari ya kujiweka mbali na utawala wa kijeshi. Hata hivyo wanajeshi wa Ujerumani wataendelea kuwapo nchini Mali. Gazeti la Der Tagesspiegel linasema Mali si sawa na nchi nyingine za Afrika kwa Ujerumani. Mali ni mshirika wa karibu wa serikali ya Ujerumani na kwamba nchi hiyo inatoa mchango muhimu katika kufanikisha mkakati wa Ujerumani barani Afrika.

Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba hatua iliyochukuliwa na wanajeshi nchini Mali inasumbua vichwa vya wanasiasa kadhaa nchini Ujerumani. Wanasiasa kadhaa wa Ujerumani wanasema hali ya nchini Mali inawaweka njia panda. Gazeti la Der Tagesspiegel limemnukulu msemaji wa masuala ya ulinzi wa chama cha SPD Siemtje Möller akieleza kwamba kuwapo kwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali ni njia mojawapo ya kutimiza wajibu wake wa kimataifa kwa sababu Ujerumani si mwanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Gazeti linasema wanajeshi wa Ujerumani wataendelea kuwapo nchini Mali lakini pia linauliza jee ni sawa kwa Ujerumani kuunga mkono utawala wa kijeshi nchini humo?

Vyanzo: Deutsche Zeitungen