Afrika katika magazeti ya Ujerumani | NRS-Import | DW | 11.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya matukio na masuala ya barani Afrika wiki hii ni pamoja na hali ya nchini Mali wiki tatu baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kuchukua madaraka.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung juu ya hali ya nchini Mali. Gazeti hilo linasema wiki tatu baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kutwaa madaraka na kuiangusha serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita wajumbe 500 wanaowakilisha jeshi, asasi za kiraia na vyama vya siasa wamekutana katika mji mkuu wa Mali, Bamako kuujadili mustakabal wa nchi yao. Gazeti la die tageszeitung linasema yapo matumaini lakini pia wasiwasi. Limemnukulu kiongozi wa jumuiya ya Tibital Pulaaku,bwana Abou Sow inayowakilisha maslahi ya kabila la wapeul. Kwa muda wa miaka mingi jumuiya hiyo imekuwa inaiokosa vikali serikali pamoja na jeshi. Gazeti  la die  tageszeitung linakumbusha juu  ya mauaji ya watu wa kabila hilo yaliyofanywa  pia na wanajeshi. Mauji hayo ni miongoni mwa matukio yaliyosbabisha kuangushwa kwa serikali ya Ibrahim Keita. Gazeti linasema kiongozi huyo wa jumuiya ya Tibital Pulaaku anatumai kwamba kamati ya kitaifa, iliyoundwa na jeshi ya kuwaokoa watu wa Mali italeta mabadiliko.

Süddeutsche Zeitung.

Gazeti la Süddeutsche wiki hii linatathmini pande mbili za Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague, ICC. Gazeti hilo linasema Bensouda amewafikisha mbele ya mahakama madikteta, wakandamizaji na wanajeshi waliopora madaraka. Hata hivyo gazeti linaeleza, mwanasheria huyo ambaye sasa amewekewa vikwazo na Marekani, ameingia katika wadhifa huo baada ya yeye mwenyewe kuishi katika dunia iliyozungukwa na watu kama hao.

Njia iliyomfikisha kwenye wadhifa wa mwendesha mashtaka mkuu haiwezi kufananishwa na ile ya watetea haki za binadamu wa kawaida. Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba aliwahai kuwa waziri wa sheria na mwanasheria mkuu wa nchi yake Gambia. Ni wakati ambapo afisa mmoja kijana wa jeshi, Yahya Jammeh alipopora madaraka nchini humo na kuahidi kuleta haki na usasa lakini Jammeh alibadilika na kuwa dikteta.

Gazeti la Süddeutcshe linasema mtu anaweza kumtetea Bensouda kwa sababu alichaguliwa kuwa waziri wa sheria wakati Jammeh alipotoa ahadi nzuri lakini kwa upande mwingine mtu anaweza kuuliza kwa nini  aliendelea kuitumikia serikali ya Jammeh kabla ya kuondoka mnamo mwaka 2000. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Bensouda siyo muhubiri wa maadili bali ni mwanasheria anayezingatia misingi halisi ya kazi yake. Alitaka kuanzisha uchunguzi juu ya uhalifu uliotendwa na askari wa Marekani nchini Afghanistan. Marekani wamemwekea vikwazo. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linasema anayemjua vizuri Bensouda atatambua kwamba mwanasheria huyo atashikilia uzi ule ule.  

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linamzungumzia rais wa Guinea Alpha Conde ambaye linasema amegeuka kuwa dikteta baada ya kuwa ishara ya matumaini. Conde ameteuliwa na chama chake kugombea muhula wa tatu madarakani baada ya katiba kufanyiwa marekebisho. Hata hivyo kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 bado hajatoa kauli rasmi iwapo atasimama katika uchaguzi. Aliposhinda uchaguzi wa rais kwa njia ya kidemokrasia mnamo mwaka 2010 Conde alikuwa mjumbe wa matumaini. Hata hivyo mnamo mwezi Februari katiba ya Guinea ilibadilishwa na hivyo kumwezesha Conde agombee muhula wa  tatu.

Kwa muda wa miezi kadhaa sasa watu wamekuwa wanaandamana kupinga uamuzi huo. Gazeti la Neue Zürcher linafahamisha kwamba mpaka sasa watu 30 wamekufa kutokana na ghasia. Rais Alpha Conde amewajibu wanaomkosoa hasa kutoka nje ya Guinea kwa kueleza kwamba anao uhuru wa kukaa madarakani jinsi anavyopenda. Gazeti hilo limemnukulu mpinzani mmoja akisema kwamba hapo  mwanzoni rais Conde alikuwa anajiona kama Mandela lakini baadaye aliamua kugeuka na kuwa Bokassa.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linatahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka kwa uharamia. Gazeti hilo linasema hali  siyo mbaya kwenye pwani ya pembe ya Afrika tu. Limeikariri ripoti ya shirika la usafiri wa baharini IMB inayofahamisha kwamba idadi ya meli zilizotekwa na maharamia mwaka uliopita iliongezeka. Pana taarifa juu ya matukio 162 ya meli kutekwa nyara duniani kote. Gazaeti la Die Welt linatilia maanani kwamba hali ni mbaya kwenye ghuba ya Guinea.

Gazeti linakumbusha kwamba mwaka uliopita mabaharia zaidi ya 120 walitekwa nyara. Hilo ni ongezeko kulinganisha na mwaka uliotangulia. Mnamo mwaka huu Die Welt linasema mabaharia wapatao 50 wametekwa na maharamia kwenye pwani ya Afrika magharibi. Gazeti hilo linatahadharisha kwamba hali inaweza kwenda mrama ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen