1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
7 Agosti 2020

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na harakati za wananchi wa Zimbabwe za kupambana na udhalimu, ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka ndani ya serikali.

https://p.dw.com/p/3gbil
Simbabwe | Coronavirus | Protest
Picha: Zinyange Auntony/AFP

die tageszeitung

Tunaanza na makala ya gazeti la die tageszeitung juu ya harakati za wananchi wa Zimbabwe za kupambana na udhalimu, ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka ndani ya serikali. Harakati hizo zinazoendeshwa chini ya kauli mbiu inayosema maisha ya wazimbabwe yana thamani zinaungwa mkono na watu mashuhuri wa ndani na nje ya Zimbabwe.

Wanaharakati wamehamishia harakati zao kwenye mitandao ya kijamii baada ya polisi kuzuia maandamano yao na baada ya wanaharakati kadhaa kukamatwa. Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba juhudi hizo za watu wa Zimabwe zinaungwa mkono pia na rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera, kiongozi wa chama cha upinzani nchini Afrika kusini Julius Malema na mwanandishi maarufu wa Zimbabwe Tsitsi Dangaremgba. Gazeti la die tageszeitung linasisisitza kwamba rais wa Malawi amehiyari kukiuka itifaki ili kuwaunga mkono wanaharakati wa Zimbabwe. Ni desturi ya viongozi wa Afrika kunyamaza kimya badala ya kumkosoa  kiongozi wa nchi nyingine.

Der Tagesspiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel limeandika juu ya kashfa iliyoikumba serikali na chama tawala, ANC nchini Afrika Kusini. Kashfa hiyo imesababishwa na watu wanaojitajirisha kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti la Der Tagesspiegel linaeleza kwamba Wafanya biashara wenye uhusiano wa karibu na viongozi wa chama tawala cha ANC wanalitumia janga hilo kupandisha bei ya vitu muhimu vinavyohitaika kwa ajili ya kuzuia maambukizi, kama vile barakoa. Gazeti linasema wafanyabiashara hao wamepandisha bei ya barakoa kwa asilimia 900. 

Der Tagesspigel linaarifu kwamba pia viongozi wa serikali ya mtaa walikupua chakula cha msaada uliopaswa kutolewa kwa wananchi. Rais Cyril Ramaphosa amewaalani watu hao na kuwaita "mafisi" Gazeti la Der Tagesspiegel linasema viongozi kadhaa wa chama na serikali wanalitumia janga la corona, kuwa wakati wa mavuno, kwa sababu serikali imelegeza nati za udhibiti ili kupambana na maambukizi kwa ufanisi.

Serikali ya Afrika Kusini imetenga kiasi cha Euro bilioni 1,5 kwa ajili hiyo. Gazeti la Der Tagesspiegel linasema kashfa hizo siyo jambo jipya nchini Afrikka Kusini hasa mtu anapokumbuka yaliyojiri chini ya utawala wa rais wa hapo awali Jacob Zuma ambapo ufisadi ulikithiri.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu mauaji yaliyotokea tena katika jimbo la Sudan magharibi, la Darfur. Watu wapatao 500 waliokuwa na silaha walikivamia kijiji cha Masteru kilichopo kwenye jimbo hilo na kuwaua watu kwa muda wa siku mbili. Kwa mujibu wa ripoti, gazeti linasema watu zaidi ya 60 waliuliwa na wavamizi hao.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema maangamizi hayo yanakumbushia unyama uliotendeka kwenye jimbo la Darfur mnamo miaka iliyopita. Gazeti linafahamisha kwamba, mbali na kuwaua watu, wavamizi waliteketeza masoko na nyumba za watu. Gazeti hilo linasema kwa muda wa wiki kadhaa sasa damu imeendelea kumwagika katika jimbo hilo. Makundi fulani ya watu wenye silaha wanajaribu kuwatimua watu wa makabila fulani ili waweze kuyachukua maeneo yao kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo.

Die Welt

Na tunakamilisha kwa makala ya gazeti la Die Welt linalozungumzia juu ya suala la uzazi. Linasema idadi  ya watu inaongezeka duniani na linatoa mfano wa Niger ambako kwa wastani kila mwanamke anazaa watoto 7. Gazeti la Die Welt limemnukulu Mahamadou Abdoulaye kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey akisema kwamba familia kubwa ni jambo la fahari linaloleta heshima kwa mtu. Die Welt linaeleza kuwa Abdoulaye alioa mapema na tayari alikuwa baba alipokuwa na umri wa miaka 18. Idadi ya watu nchini Niger inaongezea kwa asilimia 3,8 kila mwaka. Hakuna nchi nyingine duniani yenye kiwango kama hicho.

Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba mnamo mwaka 1990 Niger ilikuwa na watu milioni 8 lakini sasa wako watu 24,206,644. Gazeti hilo linasema idadi kubwa ya watu katika nchi kama Niger inachangia katika kusababisha changamoto za kijamii kiuchumi na kisiasa. Kati ya mwaka 1974 na 2010 serikali zilipinduliwa mara nne kwa njia ya umwagikaji damu.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen